Thursday, April 10, 2014

AZAM FC YAUKARIBIA UBINGWA,YAIBUGIZA RUVU SHOOTING 3


AZAM FC imeibwaga mabao 3-0 timu ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wake wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni hii.
 
Ushindi huo unaisogeza karibu kabisa na ubingwa wa Ligi Kuu Azam FC kwa kufikisha pointi 56 baada ya kucheza mechi 24, ikifuatia na mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 52 za mechi 24 pia.
 
Azam FC ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza mabao 2-0 yaliyotiwa kimiani na Gaudence Mwaikimba dakika ya tisa na Himid Mao dakika ya 36, wote wakimalizia kona za Erasto Nyoni.




Ruvu Shooting walipata pigo dakika ya 32 baada ya kipa wao wa kwanza, Abdul Seif kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo baada ya kugongana na John Bocco wa Azam, hivyo nafasi yake kuchukuliwa na Abdallah Rashid.
Kipindi cha pili, Azam ilirudi kwa kujiamini zaidi na kufanikiwa kupata bao la tatu dakika ya kwanza tu ya kipindi hicho, mfungaji Kipre Herman Tchetche akimalizia pasi pacha wake, Kipre Michael Balou.
Baada ya hapo, Ruvu wakaamua kucheza mchezo wa kujihami kuhofia mabao zaidi.
Mechi hiyo ilikuwa ifanyike jana kwenye Uwanja huo, lakini ikasogezwa mbele hadi leo sababu ya mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha Uwanja ujae maji.
Azam sasa itahitaji pointi tatu zaidi katika michezo yake miwili ya mwisho ili kutawazwa rasmi mabingwa wapya wa msimu wa mwaka 2014/ 2015.
Yanga yenye mechi mbili pia, inaweza kufikisha pointi 58 ikizifunga JKT Oljoro na Simba SC, wakati Azam ikiifunga Mbeya City itatimiza pointi 59 hivyo kuingia kwenye mechi yake ya  mwisho na JKT Ruvu wakiwa tayari mabingwa.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, David Mwantika, Aggrey Morris, Kipre Balou, Himid Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco/Brian Umony dk55, Gaudence Mwaikimba.Jabir Aziz na Kipre Tchetche/Kevin Friday dk67.
Ruvu Shooting; Abdul Seif/Abdallah Rashid dk32, Said Madega, Stefano Mwasyika, Renatus Kisase, Baraka Nyakamande, Hamisi Mohamed, Ally Mtanga, Juma Nade/Ayoub Kitala dk50, Elias Maguri, Said Dilunga na Raphael Kyara/Juma Mdindi dk66.    

No comments: