Mheshimiwa Spika, napenda
kuchuku nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema na kwa kunitumia
kama chombo cha mabadiliko hasa katika kutetea haki za wanahabari, vijana,
wanamichezo na wasanii. Namshukuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Mhe.
Freeman
A. Mbowe kwa kuendelea kuwa na imani nami katika kuisimamia Serikali katika wizara hii. Aidha, napongeza hatua ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuungana kwa pamoja kwa maslahi ya wananchi wa Tanzania. Napongeza UKAWA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwaelimisha wananchi nchi nzima. Napenda kuchukua nafasi hii kutoa salamu za rambirambi kwa wasanii nchini kwa vifo vya waigizaji Adam Kuambiana na Rachel Haule vilivyotokea hivi karibuni. Mungu azilaze Roho za Marehemu mahali pema peponi. Amen.
A. Mbowe kwa kuendelea kuwa na imani nami katika kuisimamia Serikali katika wizara hii. Aidha, napongeza hatua ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuungana kwa pamoja kwa maslahi ya wananchi wa Tanzania. Napongeza UKAWA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwaelimisha wananchi nchi nzima. Napenda kuchukua nafasi hii kutoa salamu za rambirambi kwa wasanii nchini kwa vifo vya waigizaji Adam Kuambiana na Rachel Haule vilivyotokea hivi karibuni. Mungu azilaze Roho za Marehemu mahali pema peponi. Amen.
Mheshimiwa Spika naomba
kuanza hotuba hii kwa kumnukuu kwa kirefu mmoja wa viongozi wetu ambao
wamejipambanua kwa namna ambayo wanastahili sifa za kuitwa ‘statesmen’, mtu
huyu si mwingine bali ni Jaji Mark Bomani, ambaye hivi karibuni wakati akitoa
hotuba kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo Duniani, alinukuliwa na vyombo vya
habari akisema;
“Inasikitisha
kuona kuwa hali ya Mtanzania inazidi kudidimia au kubaki pale pale katika
sehemu nyingi hasa vijijini katika kipindi cha miaka 40 iliyopita kwa kukosa
fursa muhimu za maendeleo na viongozi hawalioni hilo.”
Vyombo
vya habari vilimnukuu zaidi Jaji Bomani akisema “nchi itaendeshwa kwa kusimamia
haki na ukweli na kuwataka wanahabari wasichoke kuisimamia haki na uhuru wa
nchi yao bila woga kwani bila kufanya hivyo nchi itaongozwa kiimla.
“Ni aibu kuona mswaada wa sheria ya habari umekwama kwa zaidi ya miaka 10 kwa sababu ambazo hadi leo hazijaeleweka.”
Akawataka waandishi wa habari,
“wasikate
tamaa na badala yake waendelee na kupambana kuhakikisha kwamba harakati za
kupata Sheria ya Haki ya Kujua inafanikiwa ili kupunguza matukio ya manyanyaso,
kupigwa, kuteswa, kufungwa kwa vyombo vya habari na kuuwawa.”
“Haki haiombwi simamieni haki zenu na songeni mbele.”
“Haki haiombwi simamieni haki zenu na songeni mbele.”
2.0
MAENDELEO
YA SEKTA YA HABARI NCHINI
2.1 Miaka 10 ya mapambano na ahadi
za uongo uliofika ngazi ya kimataifa
Mheshimiwa Spika,
naomba kuchukua nafasi hii kuzungumzia vyombo vya habari. Kwanza napenda
kuvishukuru kwa kazi kubwa inayofanywa na ‘mhimili’ huu usio rasmi katika kuimarisha
demokrasia na kupigania umuhimu wa uongozi nchini kwetu.
Vyombo
vya habari vimekuwa mstari wa mbele kuibua na kuweka bayana vitendo vya rushwa,
ubadhirifu wa mali ya umma na matumizi mabaya ya madaraka licha ya sheria mbaya
na kandamizi ambazo zinaendelea kuminya uhuru wa habari na haki ya kupata
habari kwa wanahabari na wananchi kwa ujumla.
Mheshmiwa Spika,
kwa muda mrefu sasa Kambi ya Upinzani Bungeni tumezungumza kwa kirefu,
tukishauri, kutoa angalizo, kuonya na kuelekeza kwa mapana na marefu kuhusu
kufuta sheria kandamizi zilizopo zinazominya uhuru wa habari na kupata taarifa na
badala yake zitungwe sheria zingine ambazo zitaimarisha uhuru huo na kusaidia
kukomaza demokrasia nchini. Mapambano haya ya wananchi kupigania uwepo wa
Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari na Haki ya Kupata Habari si ya leo.
Yameanza tangu mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika, katika namna ya kipekee ambayo ilipaswa kuungwa mkono na serikali hii kama ingelikuwa ni sikivu, wadau wa habari kwa jitihada za kulisaidia taifa lao, walichukua jukumu la kukusanya mawazo na mapendekezo ya wadau mbalimbali wa habari kuhusu namna ya kuboresha miswada ambayo ilikuwa imeandaliwa na serikali. Mapendekezo hayo yaliwasilishwa serikalini tangu mwaka 2007 kwa sheria ya Haki ya Kupata habari na 2008 kwa sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari.
Hatuna
haja ya kurudia kusema juu ya danadana ambazo Serikali hii ya CCM imezifanya
tangu wakati huo hadi sasa nchi imeshindwa kuwa na sheria nzuri kama
ilivyopendekezwa na wadau. Mwaka jana
wananchi walifarijika walipomsikia Rais Jakaya Kikwete akitoa ahadi kwa maneno
mazito mbele ya mkutano wa kimataifa kuwa serikali ingeleta muswada wa Sheria wa
Haki ya kupata Taarifa ifikapo mwezi Aprili mwaka huu!
Mheshimiwa Spika, Rais Kikwete alikuwa akihutubia Mkutano wa Kimataifa wa Serikali Uwazi ulioitishwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroun ambao ulijadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwazi katika manunuzi ya umma, uwazi katika mikataba, haki ya kupata habari, uwazi katika ukaguzi wa fedha za umma, uwazi wa Serikali na vyombo vya habari, uwazi katika mikataba ya maliasili, uwazi katika maendeleo ya nchi zinazoendelea.
Akizungumza kwenye mkutano huo Alhamis ya Oktoba 31, Rais
Kikwete si tu kwamba aliwaahidi Watanzania bali pia alitumia jukwaa hilo la
kimataifa kuitangazia dunia nzima kuwa Serikali yake tayari inafanyia kazi
utungaji wa Sheria ya Kupata Taarifa, kwa ajili ya kuwapatia wananchi haki ya
kupata taarifa kutoka serikalini.
Vyombo vya habari mbalimbali, vya ndani na nje ya nchi,
vilimnukuu Rais Kikwete akitoa ahadi hiyo, kwa kusema;
"Kama watu wanataka kupata taarifa kuhusu namna gani dawa zinagawanywa, kama wanataka kupata taarifa kuhusu bajeti za shule zao za msingi, wanastahili kuwa na haki ya kuzipata. Kama watu wanataka kupata taarifa kuhusu lini watasambaziwa maji wanapaswa kuwa na haki hiyo. Pale watu wanapotaka kupata taarifa, haipaswi kuonekana kuwa wanaingia mahali ambapo hapawahusu.”
Gazeti la The Guardian likiandika kuhusu ahadi hiyo ya
Serikali ya CCM, lilisema hivi;
“Ahadi
hii inawakilisha moja ya hatua kubwa kuelekea haki ya kupata taarifa na suala
la Serikali Uwazi nchini Tanzania. Hata hivyo, kama ilivyo ada siku zote,
jaribio halisi litakuwa ni katika utekelezaji (wa ahadi hiyo).”
Watu wengi hawajui kuwa kabla ya kutoa ahadi hiyo nchini
Uingereza ambako Rais Kikwete aliitangazia dunia kuwa Tanzania itatunga sheria
ya uhuru wa habari na kupata taarifa yenye viwango vya kimataifa, pia aliwahi
kutoa ahadi ya namna hiyo hiyo kwenye mkutano kama huo, nchini Brazil mwaka
mmoja kabla ambako alisema hivi;
“Ninaahidi kuwa tutafanya kadri ya uwezo wetu wote kutimiza matarajio ya
ushirikiano huu ili kuhamasisha uwazi na uwajibikaji wa serikali yetu kwa
wananchi wa Tanzania. Napenda kuwahakikishia kwamba utashi wetu wa kisiasa
kufanikisha malengo ya OGP hayatakwama kwa sababu dhana ya Serikali Uwazi iko
kwenye moyo wa mkataba kati ya dola na wananchi.”
Mwandishi katika Gazeti hilo la The Guardian akamalizia kwa
kusema
“Je Tanzania inaweza kusimama imara
kutekeleza maneno haya mazito?”
Swali hilo linaweza kujibiwa na viongozi wa Serikali hii ya
CCM ambao sasa si kwamba wanaweza kutoa ahadi za papo kwa papo za kuwahadaa
Watanzania pekee, bali sasa wamevuka mipaka ya nchi na kutoa ahadi za uongo dunia
nzima ikiwasikiliza. Si tu kwamba
hawaoni tatizo kuahidi, bali sasa hawaoni shida hata kutotekeleza kila
wanachoahidi. Hii ni dalili ya wazi ya ukosefu wa dhamira na uwezo wa kukidhi
matarajio ya watu.
Mheshimiwa Spika, katika hali ambayo kwa kweli wadau
wa habari nchin wanapaswa kuanza kumjua adui yao halisi kwenye mapambano ya
kupata sheria hizi mbili muhimu, ni kitendo cha CCM kupitia kwenye vikao vyake
vya ndani kutoa maelekezo kwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokana na
chama hicho na washirika wake, ambayo kwa ujumla yanapingana na dhana nzima ya
uwepo wa sheria hizo.
Katika waraka wake wa siri ambao umeripotiwa mara kadhaa na
vyombo mbalimbali vya habari, CCM imeamua kujiandikia rasimu nyingine ambayo
chama hicho ndiyo kinataka eti Katiba Mpya ya nchi. Katika nyaraka hiyo, vikao
vya CCM ambavyo vinaongozwa na Mwenyekii wake Jakaya Kikwete, kimepinga dhana
za uwazi, uadilifu na uwajibikaji kama ambavyo zimependekezwa na wananchi ili
ziwe sehemu ya tunu za taifa ndani ya katiba.
Mheshimiwa Spika, hali hii si tu kwamba inawachanganya
wananchi, lakini inaibua munkari wa kuhoji iwapo Rais Kikwete kupitia serikali
yake, wanayo dhamira ya kuheshimu na kutambua mchango wa vyombo vya habari na
umuhimu wa wananchi kuwa na taarifa juu ya namna nchi yao inavyoendeshwa! Ni
suala linalochanganya na kuibua maswali mengi yasiyokuwa na majibu kuona Rais
Kikwete anatoa ahadi kimataifa kuhusu kukuza uwazi na uwajibikaji kwa
kuimarisha uhuru wa habari na kupata taarifa, lakini wakati huo huo akiwa hapa
nchini bali ya serikali yake kushindwa kutimiza ahadi hiyo, anasimamia vikao
vya chama chake ambacho kinapinga maoni ya Watanzania wanaotaka Katiba Mpya
izingatie uwazi, uadilifu na uwajibikaji!
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia majibu ya Serikali yaliyotolewa hapa bungeni kwenye mkutano huu wa 15 kikao cha 16 kuhusu miswada ya sheria hizi mbili na mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Ubungo John Mnyika na Serikali ikashindwa kutoa majibu ya kuridhisha, inazidi kudhihirisha kuwa hakuna dhamira ya dhati kutekeleza jambo hili. Sasa maelezo ya Mheshimiwa waziri wa Sheria na Katiba, Dr. Asha Rose Migiro katika hotuba ya Makadirio ya wizara yake ni kuwa waraka wa kupeleka kwenye Baraza la Mawaziri wa kupendekeza kutungwa kwa Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa umeandaliwa.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitarajia Serikali ya CCM kutambua umuhimu wa kutekeleza ahadi zake hapa bungeni kwa miaka 7 lakini zaidi ya hapo kutimiza ahadi iliyotolewa na Rais Kikwete ili kumwokoa na aibu ya kusema uongo kwenye mkutano mkubwa wa kimataifa wa Open Government Partnership, mjini London. Tulitarajia Serikali hii ingelikuwa sikivu, ingetambua kuwa sheria hizo ni mtambuka na inahusu wananchi wote katika haki ya kupata na kutoa taarifa kama ilivyoelekezwa na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inalaani kwa nguvu zote, sheria kandamizi zinazonyima vyombo vya habari uhuru wa kufanyakazi zake kwa ufanisi, za kufichua maovu kama rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na hujuma za raslimali za taifa. Sheria hizo zinatishia uhuru wa uhariri na kuleta woga wa kushtakiwa kwa makosa ya jinai.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa ahadi ya kuleta Bungeni muswada wa sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ambazo zitasimamia utendaji kazi wa vyombo vya habari nchini. Wote tunafahamu kuwa sheria zilizopo zinazosimamia vyombo vya habari ni mbaya, ni kandamizi na hazina nafasi katika nchi inayojinadi kuwa ni ya kidemokrasia. Sheria hizi zinavifanya vyombo vya habari na wanahabari kutekeleza majukumu yao katika mazingira magumu. Katika vikao vya bunge kwa takriban miaka saba sasa, tumekuwa tukisikia ahadi za serikali ya kubadilisha sheria hizi kandamizi ambazo kwa kiasi kikubwa zinakiuka Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, tunawasiwasi mkubwa wa nia ya serikali ya kufanya mabadiliko stahiki. Tunaona hakuna dhamira ya dhati ya kuleta sheria bora. Hili limedhihirishwa na hatua ya serikali ya mwezi Novemba mwaka 2013 ya kuleta mabadiliko ya sheria mbalimbali (Miscellaneous Ammendement Act) ambayo ndani yake ilikuwa na mapendekezo ya Sheria ya Magazeti 1976, Sheria ya Filamu na Michezo ya Jukwaa na Sheria ya Kanuni za Adhabu ambazo zilikuwa na lengo ya kuongeza adhabu kubwa kwa makosa ya kitaaluma.
Ni muhimu sana kwa Serikali kuacha kutoa ahadi hewa hapa Bungeni na kwingineko na badala yake tudhihirishe utashi wetu kwa kutekeleza kwa vitendo. Ahadi zinazotolewa na mawaziri miaka nenda miaka rudi hapa Bungeni bila kutekelezwa zinashusha hadhi ya Bunge na Taifa letu machoni mwa watanzania na dunia kwa ujumla. Ni jambo lisilopendeza na ni la aibu kwa kweli kwani inaonyesha dhahiri kuwa ama utendaji kazi ni hafifu sana katika serikali hii au la basi Serikali hii haina nia njema ya kufanya marekebisho ya kimfumo ili tuwe na sera na sheria nzuri ambazo zitastawisha demokrasia, uwazi na uwajibikaji.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani Bungeni inawataka mawaziri husika wawe jasiri na watimize
ahadi walizotoa kwenye Bunge hili tukufu za kuleta miswada ya sheria za Haki ya
Kupata Taarifa na ule wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari. Wadau wa habari wameshafanya kazi kubwa kwa
kutoa mapendekezo yao serikalini. Wayatumie mapendekezo hayo kuandika miswada
hiyo na kuileta hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, wenzetu wadau wa habari wamejipanga kuboresha na kuinua hali ya uwajibikaji na maadili katika vyombo vya habari. Tuwaunge mkono kwa dhati kwenye hilo. Kupitia Baraza lao la habari wamepitisha Azimio la Dar es Salaam ambalo linazungumzia haki na wajibu wa vyombo vya habari katika kuimarisha weledi, maadili na uhuru wa uhariri.
Napenda
niongeze kwa lengo ya kuweka msisitizo kuwa Haki ya Kupata Taarifa ni muhimu na
ya msingi sana, kwani ni
sheria mtambuka na inahusu haki ya msingi ya kupata habari ambayo ni haki
inayolindwa kikatiba. Ni ukweli wa uhakika kuwa utawala
ulioshamiri katika mila za usiri ndio ulioifikisha Tanzania yetu mahali hapa pabaya.
Ndio chanzo cha mikataba mibovu na kushindwa kwa uwajibikaji kwa sababu tu
watendaji wabovu wanaweza kujificha katika kinga ya usiri. Kambi Rasmi ya
Upinzani tunaitaka Serikali kuleta Bungeni muswada wa sheria ya Haki ya Kupata
Habari ndani ya mwaka huu kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasisitiza tena kuwa uwepo wa sheria nzuri za vyombo vya habari ambayo itakuwa kwa manufaa ya wananchi na serikali. Wakati wananchi wanasubiri sheria mpya ya Huduma za Vyombo vya Habari, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuleta Bungeni Muswada wa kufuta Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 pamoja na kufanyia marekebisho sheria nyingine 17 zenye vipengele kandamizi kwa vyombo vya habari kwa kuwa sheria hizo ni kinyume na Katiba ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Pia sheria hizo zinaendeleza utamaduni wa usiri ambao kama nilivyosema awali unasaidia sana kufanya viongozi wasiwajibike ipasavyo na kufanya mambo yasiyostahili kwa kujificha kwenye kinga ya usiri.
2.2 Uhuru wa uhariri, vitisho kwa
waandishi wa habari na utatu hatarishi
Mheshimiwa
Spika, katika hali ambayo imezidi kudhihirisha kuwa Serikali ya CCM
inawalazimisha Watanzania kuendelea kuishi ‘zama za mawe’, Mwezi Septemba mwaka
jana, tasnia ya habari ilipata dhahama kubwa baada ya Serikali kupitia wizara
husika na Habari Maelezo, katika hali ambayo hadi sasa haijulikani ilikuwa kwa
maslahi ya nani, iliamua kufungia magazeti mawili ya Mtanzania na Mwananchi. Tunasema
ni zama za mawe kwa sababu, vitendo vya kufungia vyombo vya habari kwa namna
ambayo imekuwa ikifanywa na Serikali ya CCM ikitumia sheria zilizopitwa na
wakati, ikiwa ni sehemu ya kubana uhuru wa maoni na utoaji wa fikra mbadala, vilifanywa
enzi zile ambapo dunia ilikuwa inaaminishwa kuwa ina muundo wa meza.
Mheshimiwa Spika, Kwa namna ambayo iliendelea kutuanika namna tunavyokumbatia ‘ukoloni na ukaburu’, Serikali ya CCM ilijigeuza mlalamikaji, polisi (mkamataji), mwendesha mashtaka, hakimu na kisha askari magereza (mfugaji) kisha kulifungia Gazeti la Mtanzania siku 90 na Mwananchi siku 14. Kambi ya Upinzani Bungeni inataka kujua kupitia kauli ya serikali hapa bungeni, mtindo huu wa udikteta unaofanywa na serikali hii inayojiita sikivu inayoshughulikia vyombo vya habari, utaendelea hadi lini?
Mheshimiwa Spika, kwa sasa zipo fikra miongoni mwa wadau wa vyombo vya habari kwamba uhuru wa habari nchini unazidi ‘kuwambwa msalabani’ kwa sababu ya utatu wa hatari ambao umetengenezwa na Serikali ya CCM, kwenye Wizara ya Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni. Utatu huu hatari unaundwa na waziri mwenyewe Dk. Fenela Mkangara ambaye mbali ya kwamba si mwanahabari, si mwanasanaa, si mwanamziki wala si mwanamichezo, taarifa zinaonesha kuwa amekuwa na dhamira ya kupambana na vyombo vya habari, ambao ni wadau wake, tangu alipoteuliwa.
Mheshimiwa Spika,
Akiandika kwenye safu yake, mmoja wa waandishi waandamizi nchini, alikuwa na
haya ya kusema juu ya Dk. Mukangara;
“Waziri
mwenye dhamana Dk. Fenella Mukangara kwa muda mrefu amekuwa na nia ovu dhidi ya
vyombo vya habari. Julai mwaka jana (akimaanisha 2012) tukiwa Hotelki ya Dodoma
mjini Dodoma, wakati tunafanya mazungumzo rasmi na Waziri Mukangara, walikuwepo
Theophil Makunga, Pili Mutambalike, Neville Meena na marehemu Alfred Mbogola na
wengine, Dk. Mukangara alitoa kauli iliyotushtua wengi na sasa ndipo tunaona
inatekelezeka kwa vitendo.”
Mwandishi huyo aliongeza kwa kunukuu
maneno ya Waziri Mukangara ambaye amenukuliwa akisema;
“Nikipata fursa
Mwananchi nitalifuta, mimi linanikera sana. Tena na Nipashe nao naona wanakuja,
ikibidi nitawafungia tu, mimi siogopi kitu.” Hayo ni maneno ya Waziri
anayetakiwa kuwa mlezi wa vyombo vya habari!
Mwandishi huyo katika makala yake akaendelea kuandika hivi;
“Baada ya kauli hii
tuliendelea na mazungumzo mengine, lakini Meena akatwambia kuwa Dk. Mukangara
aliwahi kutoa kauli kama hii ofisini kwake walipokwenda akina Jesse Kwayu,
Meena na Absalom Kibanda kuomba Gazeti la Mwanahalisi lifunguliwe. Mwanahalisi
alilifungia kwa muda usiojulikana…”.
Mheshimiwa Spika, si Waziri Mukangara mwenyewe wala mtu mwingine yeyote kwa niaba yake,
amewahi kukanusha maneno hayo aliyonukuliwa akiyasema hadharani mbele ya wadau
ambao yeye anapaswa kuwa kiongozi na mlezi wao. Kutokana na mwenendo wa Waziri Mukangara wa
kupamabana na vyombo vya habari, unaofumbiwa macho na mamlaka iliyomteua, labda
kwa bahati mbaya au sehemu ya mkakati wa serikali hii ya CCM. Uhusiano wa
waziri na vyombo vya habari ulifikia hatua mbaya zaidi, baada ya wadau wa
habari waliokutana Oktoba 9 mwaka jana, kufikia maazimio kadhaa, ikiwemo lile
linalosema;
“Kusitisha kuandika, kutangaza na kupiga picha shughuli zozote zitakazowahusisha au kuratibiwa na Mheshimiwa Fenella Mukangara na Assah Mwambene hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo. Adhabu hiyo inaanza mara moja kuanzia leo.”
Mheshimiwa Spika, hapo juu kwenye moja ya maazimio ya wadau wa habari, ametajwa Assah Mwambene, huyu ni Mkurugenzi wa Habari Maelezo. Mkurugenzi huyu ambaye amewahi kufanya kazi kwenye vyombo vya habari kama mwandishi, pamoja na kwamba kwa majukumu yake hayo alipaswa kuwa mtu wa karibu kama mwelekezi na kiongozi kwa wadau wake, kwa kushirikiana na Waziri Fenella Mukangara, amekuwa ni mwiba kwa utendaji wa vyombo hivi, akihusika kuuweka uhuru wa habari na uhariri katika sintofahamu kubwa.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha Mkurugenzi wa Habari Maelezo kufanya maamuzi makubwa ya kuyatisha magazeti ya Mwananchi na Rai, kutimiza wajibu wa kuendelea kuhabarisha, kwanza bila kuwa na msingi wowote wa kisheria na pili bila kuwasiliana na wakubwa wake wala wasaidizi wake, kama ilivyotamkwa na aliyekuwa Naibu Waziri Amos Makala, ni jambo ambalo linathibitisha jinsi alivyo sehemu ya utatu huu tunaozungumza hapa.
2.3 Kauli za Dharau Dhidi ya
Wanahabari
Mheshimiwa Spika, wakati katibu mkuu kiongozi anataja mabadiliko ya baraza la mawaziri Ikulu tarehe 19 Januari Mwaka huu, akiwa amezungukwa na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, wakati akitaja jina la Naibu waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Juma Nkamia, wanahabari hao waliguna na kucheka ikiwa ni ishara ya kutoridhishwa na uteuzi huo. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inaungana na wana habari wote kwa kuguna na kuchekeshwa na uteuzi wa Mhe. Juma Nkamia ambaye ni dhahiri hana maslahi na wana habari bali ameitumia tasnia ya habari kama daraja lake la kufanikisha maslahi yake binafsi ya kisiasa.
Mheshimiwa Spika, tarehe 17 Novemba mwaka 2013, Baraza la Habari la Tanzania lilioneshwa kusikitishwa na kauli za Mhe. Nkamia ambaye alitoa kauli ya kulikashifu baraza hilo wakati akiwa katika vikao vya Bunge wakati yeye akiwa ni mmoja watu walionufaika na Baraza hilo. Akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Nkamia alitamka kuwa , MCT(Baraza la Habari Tanzania) na TEF (Jukwaa la wahariri Tanzania) ni sawa na asasi zisizo za Kiserikali (NGOs) lakini zimekuwa zikijipa kazi ya kusimamia waandishi wa habari nchini.
Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa kauli ya Mhe. Nkamia ilikua ni ya dharau dhidi ya wana habari, dharau dhidi ya tasnia ya habari na dharau dhidi ya vyombo hivyo ambavyo kwa nyakati tofauti, kabla na hata baada ya kupata ubunge, Naibu Waziri alikua akizitambua na kushirikiana nazo. Na kwa kumbukumbu rasmi, ni kuwa MCT na TEF ndizo taasisi zinazoendelea kupigania maslahi ya wana habari dhidi ya uonevu unaofanywa na Serikali hasa kwa wale ambao wana misimamo na misingi ya uadilifu kwani vyombo hivyo ndivyo vilivyounda timu maalum ya uchunguzi kuchunguza mazingira yaliyopelekea kuuawa kwa mwandishi wa habari Daudi Mwangosi Septemba 2, 2012 katika kijiji cha Nyololo, wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa ambapo ripoti yake ilifichua kuwepo kwa mahusiano mabaya baina ya waandishi wa habari na aliyekua kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa ambaye aliulizwa maswali magumu na Marehemu Mwangosi ikiwemo ni kwanini chama tawala cha CCM kiko huru kufanya mikutano ya kisiasa wakati chama cha upinzani kama Chadema kinawekewa vikwazo na polisi kila wakati.
Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri amesahau kuwa anazoziita asasi zisizo za kiserikali, ndizo zilizochangia kwa mapinduzi katika sekta ya habari nchini kwa kufanikisha mambo muhimu ikiwemo kusimamia maadili ya waandishi wa habari, kuandaa mitaala ya kufundishia waandishi wa habari ambayo imepitishwa na Baraza la Elimu la Taifa (NACTE) na pia kutumiwa na viongozi wakuu wa Serikali na wanasiasa kama aliyekua Makamu wa Rais, Dkt. Omar Ali Juma, mawaziri wakuu waliopita Edward Lowassa na Fredrick Sumaye katika kusululuhisha migogoro inayohusiana na tasnia ya habari, inakuaje yeye binafsi avipuuze vyombo hivyo muhimu? Na ndio maana kuteuliwa kwake kuwa Naibu Waziri kuliwashangaza wanahabari na wadau wa habari.
Mheshimiwa Spika, aidha kwa nyakati tofauti Naibu waziri amekua akiwaita waandishi wa habari kuwa ni waandishi makanjanja na yeye kujinasibu kuwa ni mwandishi mwenye weledi na taaluma. Kambi rasmi ya Upinzani, ina ushahidi kuwa Mhe. Nkamia amelidanganya bunge na taifa kwa ujumla kwa kutuaminisha kuwa yeye alikua ni mfanyakazi mwajiriwa wa Shirika la Habari La Uingereza BBC, kitengo cha Propaganga wakati Bwana Tido Mhando ambaye amefanya kazi na Shirika hilo kwa takribani miaka 20, alikana kujua uwepo wa kitengo hicho katika Shirika hilo na zaidi kueleza kuwa Mhe. Nkamia hakua muajiriwa wa Shirika hilo bali aliitwa ili kwenda kusoma taarifa za habari tu kama kibarua jaambo ambalo hajawahi kusema hadharani. Hivyo mbwembwe zote za Naibu waziri zilikua ni kumuhadaa Rais Kikwete ili apate uongozi kwa sifa asizostahili. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inauliza, je wakiitwa waandishi makanjanja, Kiranja wao ama mwalimu wao mkuu ni nani?
3.0 MAENDELEO YA VIJANA
3.1 Baraza la Vijana la Taifa,
Benki ya Vijana na Mustakabali wa Maendeleo ya Vijana Nchini
Mheshimiwa Spika; Kifungu 6002 Idara ya Maendeleo ya Vijana ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo katika mwaka wa fedha 2014/2015 inaombewa jumla ya Sh. 995, 234,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Fedha hizo kwa kiwango kikubwa ni za matumizi yasiyo ya lazima yanayohusiana na Mbio za Mwenge yasiyokuwa na uhusiano moja kwa moja na maendeleo ya vijana nchini. Ikumbukwe kwamba siku chache zilizopita tarehe 27 Mei 2014 katika kikao cha kumi na tisa kwenye Mkutano huu wa Bunge, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ilijibu kwa mfano mwaka 2012 Jumla ya Tsh 650,000,000 zilitengwa kwa ajili ya kuadhimisha Uzinduzi na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Hali hii inajidhihirisha katika uchambuzi wa kasma za idara hii ya maendeleo ya vijana ambapo kwenye matumizi ya kawaida kasma 210314 kumetengwa posho za vikao Sh 20,100,000 katika mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili ya “vikao vya uanzishwaji wa Baraza la Vijana, Benki ya Vijana pamoja na tathmini ya Mbio za Mwenge wa Uhuru”.
Mheshimiwa Spika;
Hali hii inadhihirisha Wizara haiweki kipaumbele katika kazi muhimu zinazohusu
uanzishaji uanzishwaji wa vyombo viwili muhimu kwa ajili ya vijana: Baraza la
Vijana la Taifa na Benki ya Vijana ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani imehoji kwa
nyakati mbalimbali kutaka utekelezaji uharakishwe. Kitendo cha kutenga
rasilimali kidogo kwa ajili ya kazi hizo, huku rasilimali hizo zikielekezwa
katika posho za vikao na vikao hivyo
vikiwa na ajenda nyingi nyingine zikiwa tofauti na masuala ya msingi ya
maendeleo ya vijana kinaashiria udhaifu mkubwa wa Serikali inayoongozwa na CCM
katika masuala yanayohusu vijana.
Mheshimiwa Spika, kwa vyovyote vile, chini ya makada wa CCM posho hizo zitatumika kujadili kuhusu mbio za Mwenge kuliko masuala ya msingi ya uanzishwaji wa Baraza la Vijana la Taifa na Benki ya Vijana kwa kuzingatia namna Serikali ya CCM ilivyojibu bungeni kubariki Mwenge huo kutumika kwa ajili ya propaganda potofu za Serikali mbili kuelekea kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba. Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa mwito kwa uongozi wa Bunge na Wabunge katika mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hii kuhakikisha mamlaka na madaraka ya wabunge kwa mujibu wa Ibara ya 63 ya Katiba ya Nchi yanatumika vizuri zaidi kuwezesha kuharakishwa kuundwa kwa Baraza la Vijana la Taifa na Benki ya Vijana kwa ajili ya Maendeleo ya Vijana nchini.
Mheshimiwa Spika; Katika Mkutano wa 14 Kikao cha 15 tarehe 21 Disemba 2013 ulisomwa Bungeni Muswada Binafsi wa Mbunge wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013. Baada ya muswada huo, Bunge lilielezwa pia na Mheshimiwa Spika,
“ Waheshimiwa
wabunge, muswada binafsi wa Mheshimiwa Zitto Kabwe sasa utaanza kuwepo kwenye
website ya Bunge na utakuwa public mpaka utakapopangiwa tarehe ya kujadiliwa na
utapelekwa kwenye kamati zitakazohusika wakati muafaka”.
Kambi
Rasmi ya Upinzani inatoa mwito kwa Spika: Mosi, kuweka kumbukumbu sawa kwa
kulieleza Bunge kwamba muswada binafsi wa mbunge uliwasilishwa na Mheshimiwa
John Mnyika; Pili, kulieleza Bunge sababu ya maelekezo yake ya muswada huo
kuwepo kwenye tovuti ya bunge kwa ajili ya kuwa wazi kwa umma mpaka sasa
kutokutekelezwa, Tatu, ni lini muswada huo utapangiwa tarehe ya kujadiliwa;
Nne, ni kwanini mpaka sasa muswada huo haujapelekwa kwenye kamati
zinazohusika; Tano, ni upi wakati
muafaka alioutaja kwenye maelezo yake.
Mheshimiwa Spika;
Kambi Rasmi ya Upinzani inawahimiza wabunge kuzingatia kwamba kutokuwepo kwa
chombo kinachowaunganisha vijana wote bila kujadili itikadi kufuatilia masuala
ya maendeleo ya vijana kunafanya Wizara mbalimbali za kisekta kutokuzingatia
masuala yaliyokipaumbele kwa maendeleo ya vijana. Mathalani, katika Mkutano huu
wa Bunge katika Fungu la 65 la Wizara ya Kazi na Ajira Kitabu cha Nne Cha
Miradi ya Maendeleo Kifungu cha 2002, pamoja na wabunge na vijana kupewa
matumaini kwamba zimepitishwa bilioni tatu kwa ajili ya mikopo na mitaji kwa
vijana ukweli ni kwamba fedha hizo zimepangiwa matumizi ambayo kusipokuwa na
chombo cha kuyafuatilia kutakuwa na udhaifu, ufisadi na ubadhirifu kama
ilivyojitokeza katika fedha za mifuko ya maendeleo ya vijana kati ya mwaka 1993/1994 mpaka 2013/2014.
Mheshimiwa Spika;
Kwa mujibu wa Kasma za Kifungu hicho cha 2002 cha Bajeti iliyopitishwa ya Fungu
65 Wizara ya Kazi na Ajira, fedha hizo zinazopaswa kuwa za mikopo na mitaji kwa
vijana zitatumika milioni 700 kwa ajili ya kulipia utaalamu elekezi
(consultancy fees) kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vijana 200 tu; milioni 150
zitatumika kununulia magari Wizarani, milioni 60 zitatumika kwenye matangazo na
orodha ndefu nyingine ya matumizi yasiyo
ya lazima ambayo kutokana na ufinyu wa muda sitaendelea kuyataja. Aidha, katika mjadala wa bajeti hiyo wabunge
waliweka bayana kwamba kiwango kinachotengwa katika Mifuko ya Maendeleo ya
Vijana iwe ni kwa Serikali Kuu na hata Halmashauri ni kidogo ukilinganisha na
uwezo wa nchi, mahitaji ya vijana na mafungu mengine yasiyo na matumizi muhimu
yanavyotengewa fedha nyingi katika baadhi ya Wizara.
Mheshimiwa Spika;
Hivyo, ili Baraza la Vijana la Taifa na Benki ya Vijana ambavyo ni vyombo
muhimu kwa maendeleo ya vijana viweze kuanzishwa kwa wakati, Kambi Rasmi ya
Upinzani inatoa mwito kwa Spika wa Bunge kuelekeza muswada binafsi uliokwisha
wasilishwa kwa Bunge kwa kamati zinazohusika kwa ajili ya kuanza kuujadili. Aidha, Spika arejea ratiba ya
Bunge ambapo imetajwa bayana kwamba kati ya tarehe 5 Juni 2014 na 11 Juni 2014
ratiba ya Bunge haitahusu uwasilishaji wa Bajeti za Serikali. Ratiba imetaja
bayana kwamba “Shughuli nyingine yoyote kama itavyokuwa imeelekezwa na Spika”
inaweza kuingizwa kwenye ratiba; hivyo, fursa hiyo itumike kuleta muswada huu
Bunge kusomwa kwa mara ya pili.
Mheshimiwa Spika;
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Bunge kuingilia kati suala hili na kuisimamia
Serikali kwa kuzingatia kwamba katika majumuisho ya Bajeti ya Wizara hii kwa
mwaka 2013/2014 tarehe 21 Mei 2013 mkutano wa 11 kikao cha 30; Serikali
ilitumia kisingizio kwamba ‘ni bunge la bajeti’ kukwepa kuwasilishwa kwa muswda
Bunge. Hata hivyo, ahadi ya Serikali ya kuwasilisha muswada haikutekelezwa
kwenye mikutano mitatu uliyofuatia ya 12, 13 na 14; hivyo mkutano huu wa 15 ni
muafaka kuwezesha maamuzi kufanyika kwa ajili ya maendeleo ya vijana nchini.
Mheshimiwa Spika;
Kambi Rasmi ya Upinzani inaikumbusha Serikali na wabunge kwamba Sera ya zamani
ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 ilitamka kwamba kutaanzishwa Baraza la Vijana na suala hilo kurudiwa
katika Sera mpya ya mwaka 2007; hata hivyo Serikali imekuwa ikikwepa
kuhakikisha kwamba matakwa hayo ya sera tajwa yanatekelezwa pamoja na kuwa
suala hilo linahusu mustakabali wa maendeleo ya vijana nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani inakumbusha pia kwamba katika ilani za uchaguzi Mkuu wa mwaka
2010 vyama mbalimbali viliahidi kuhakikisha kwamba Baraza la Vijana la Taifa
linaundwa. Ili kuwahadaa na kujipatia
kura za vijana CCM kwa kupitia ilani yake katika kipengele 80 (k) inasema
“Kuhamasisha
ushiriki wa vijana katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwa ni pamoja na
kukamilisha uanzishaji wa Baraza la Vijana”.
Mheshimiwa Spika;
Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inatarajia kwamba wabunge wa pande zote katika
suala hili la kuanzishwa kwa Baraza la Vijana la Taifa kuungana kuwa kitu kimoja
kuisimamia Serikali na kutumia madaraka ya
Bunge kutunga sheria wakati wa Mkutano huu wa Bunge unaoendelea.
Serikali na wabunge mzingatie kwamba
zaidi ya miaka 18 ahadi za kukamilisha mchakato wa kuanzishwa kwa
baraza la Vijana la Taifa; bila utekelezaji
kamili na wa haraka. Baraza la Vijana litawezesha vijana kuanzia kwenye
vijiji/mitaa mpaka taifa kuweza kuwa na vyombo vya kuwaunganisha vijana kwa
kike na wa kiume kwa ajili ya maendeleo yao na ya taifa.
Mheshimiwa Spika;
Aidha, Baraza hilo litafuatilia pia kwa karibu utekelezaji wa mipango ya
maendeleo ya vijana kwenye Halmashauri, Serikali kuu, katika vyombo mbalimbali
vya maendeleo na wadau wa maendeleo. Pia, Baraza la Vijana litafuatilia kwa
karibu utendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kuhakikisha kwamba fedha
zinatengwa za kutosha na kufika kwa walengwa kuwawezesha vijana kujiajiri,
kukuza vipaji vyao na kushughulikia maendeleo yao kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, aidha Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji ni kwa
nini kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 Jumla ya fedha zilizopelekwa kwenye
vikundi mbalimbali kwa kupitia mfuko wa vijana ni shilingi milioni 172.6 tu sawa na asilimia 2.8 tu, kati ya Shilingi Bilioni 6.1 ambazo Serikali mwaka jana iliwadanganya vijana kuwa
itatenga, huku taarifa ya wizara ikionesha kuwa kiasi cha shilingi Bilioni 2 sawa na asilimia 32.7 pekee ndizo zilizokua zimepokelewa hadi kufikia April
2014. Je, kiasi cha shilingi milioni 827.4,
zimetumikaje tumikaje? Je, Serikali itaacha lini kuwahadaa vijana kuwa
wanatenga mabilioni ili kuwanyamazisha katika kudai haki zao huku ikijua kuwa
haiwezi kuwasaidia hata kwa kile wanachostahili?
4.0
UTAMADUNI
4.1
UTAMADUNI: KIELELEZO
CHA HISTORIA YA TAIFA
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, imekua ikishauri Serikali juu ya umuhimu wa kutunza
maeneo na majengo ya kale ili kuweza kuonesha urithi wa utamaduni wa taifa
letu. Ni dhahiri kuwa maeneo mengi ya kihistoria yameachwa na kuwa magofu na
mengine yanaendelea kubomolewa kwa ujenzi mpya hali inayofanya historia ipotee,
jambo ambalo pia linalikosesha taifa mapato yanayotokana na utalii. Kambi Rasmi
ya Upinzani, inataka kujua mikakati ya wizara kuhakikisha kuwa maeneo na
majengo ya kale yanahifadhiwa na kuachwa katika hali yake kwa mwaka huu wa
fedha wa 2014/2015.
4.2
BARAZA LA SANAA TANZANIA (BASATA)
Mheshimiwa
Spika, Baraza la Sanaa
nchini lina dhamana kubwa kuhakikisha kuwa sanaa ya mtanzania haipoki wala
kudhalilisha maadili pamoja na kuiendeleza sanaa hapa nchini. Ni jambo la
kushangaza kuona kuwa Baraza hili hufanya kazi kwa kuzinduka tu usingizini huku
athari za uporomokaji wa maadili kwa kupitia sanaa katika jamii zinakua kubwa.
Mheshimiwa
Spika, ngoma ya Kigodoro
haikua maarufu katika sehemu kubwa za nchi kutokana na ngoma hiyo kuchezwa
katika sehemu chache. Lakini, baada ya kutolewa kwa filamu ya Kidogoro ambayo
kwa kiasi kikubwa ilihamasisha jamii kutaka kujua maana ya kidogoro na hivyo
ngoma hiyo kuzidi kupata umaarufu katika sehemu kubwa ya jamii ya watanzania
hata kwa watanzania wanaoishi nje ya nchi. Mara baada ya Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, kuelezea athari za ngoma hii katika maadili ya watanzania
BASATA ghafla ikazinduka usingizini na kupiga marufuku ngoma hiyo, huku filamu
ya Kigodoro ikiwemo katika soko la filamu na ikiendelea kuuzwa huku ikiambatana
na ujumbe ambao si tu unahamasisha uvunjifu wa maadili ya kitanzania bali
unatoa taswira ya jamii isiyostaarabika. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
inaitaka wizara hii kuisimamia BASATA ipasavyo pamoja na kuipa uwezo wa kifedha
ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kuutunza na kuutangaza utamaduni wa
mtanzania kwa kupitia kazi za sanaa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka BASATA kuacha uvivu na kutekeleza majukumu yake kwa ubunifu ili
kulinda na kuutangaza utamaduni wa Mtanzania ili hatimaye navyo vitoe mchango
katika taifa kutokana na mapato yanayotokana na mauzo ya kazi za sanaa na
utamaduni.
4.3
WASANII NA HARAKATI MBALIMBALI
Mheshimiwa
Spika, katika mapambano ya
kudai haki za wasanii duniani popote, wasanii huongozwa na dhamira ya kutumia
sanaa zao ili kuleta mabadiliko ya kweli na si kukubali kutumika kuwa faraja
kwa watu wengine kufanikisha malengo yao na mwishowe haki wanazozipigania
kuonekana kama kelele za chura.
Mheshimiwa
Spika, kila mtu ana uhuru
wa kufanya maamuzi yake hasa maamuzi ya msimamo wa kisiasa. Ila kwa muda mrefu
sasa, wasanii wa Kitanzania tumeshindwa kuwa mabalozi wa kweli wa haki katika
kuhakikisha kuwa tunatumia kazi zetu za sanaa tunapigania haki na usawa ili
kulikomboa taifa. Matokeo yake, baadhi ya wasanii wamekua wakitumika kama
chambo na baadhi ya wanasiasa ili kuweza kutimiza maslahi ya wanasiasa, ambayo
kwa kifupi baada ya kutumika, hata maslahi ya wasanii ambayo wanapigania huwa
hayapewi kipaumbele. Mfano mzuri kwetu wasanii ni jinsi ambavyo tumetumika sana
katika harakati za kisiasa lakini katika mchakato wa katiba, tumesahulika. This
is a wake up call kwa wasanii wote ambao wamekubali kutumika kwa maslahi ya
muda mfupi bila kuangalia mustakabali wa sekta ya sanaa katika taifa letu.
Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, inawataka wasanii kuacha kutumika na kujenga
umoja imara utakaotetea maslahi yao kwa ujumla bila ya kufuata mashinikizo ya
kisiasa ili kuleta mapinduzi ya kweli katika sanaa.
4.3.1SANAA NA WASANII KUTUMIKA KWENYE
UFISADI NA UFICHAJI WA MGONGANO WA MASLAHI
Mheshimiwa Spika, Katika Maoni yetu kwa
hoja hii ya mwaka jana, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu
ilizungumzia kwa kirefu jinsi ambavyo Serikali hii ya CCM imeshindwa kulinda
haki za wasanii licha ya kuwepo kwa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki tangu
mwaka 1999. Tulielezea jnsi ambavyo, licha ya masharti ya Sheria hiyo na licha
ya kuwepo kwa Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) tangu mwaka 2007, nyimbo
za wasanii nchini zimeendelea kutumiwa kwenye matangazo ya vyombo vya habari,
hasa vya Serikali kama vile Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1 na TBC2) bila
wasanii waliozitunga au kuziimba nyimbo hizo kupata malipo yoyote.
Mheshimiwa Spika,
Ni haki na wajibu kwa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu kupiga
kelele dhidi ya unyonyaji huu wa wasanii wetu, hasa wanamuziki vijana wa kizazi
kipya ambao wanajihangaikia kutafuta maisha na kuendeleza vipaji vyao. Kwa
sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inawaahidi wasanii
wetu kwamba itaendelea kutimiza wajibu wake kwa kutetea haki na maslahi yao
hadi watakapotendewa haki.
Hata
hivyo, Mheshimiwa Spika, ni haki na wajibu kwa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge
lako tukufu kuwakemea na kuwakosoa vijana pale wanapojiingiza katika vitendo
vinavyochafua sanaa na sifa zao kama wasanii na wa-Tanzania. Kama
inavyofahamika na wananchi na hata kwa Bunge lako tukufu, wasanii kadhaa wa
ki-Tanzania wamekamatwa katika nchi za nje wakiwa na madawa ya kulevya. Wasanii
wa aina hii, wanaokubali kutumiwa kama punda wa mizigo ya madawa ya kulevya na
mitandao haramu ya biashara hiyo, hawastahili chochote kutoka kwa wa-Tanzania
zaidi ya dharau na adhabu kali zilizowekwa na sheria za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Kutumia
umaarufu wao ili kuficha ushiriki wao katika biashara haramu ya madawa ya
kulevya sio tatizo pekee la baadhi ya wasanii wetu. Sasa limejitokeza tatizo la
baadhi ya wasanii wetu, hasa wanamuziki maarufu wa Bongo Fleva, kujiingiza –
kwa kujua au kwa kutumiwa na wajanja bila ya wao kujua – kwenye ‘dili’ za
kifisadi za kuiba fedha za umma. Wajanja hao hujificha katika kivuli cha
makampuni yanayotajwa kuwa na malengo ya kuendeleza wasanii na sanaa kumbe ni
vichaka vya kuficha ufisadi, mgongano wa kimaslahi na matumizi mabaya ya
madaraka ya baadhi ya viongozi wa umma dhidi ya fedha za umma wanazopaswa
kuzisimamia.
Utaratibu
unaotumika kutekeleza dili hizi za kifisadi unafanana kwa kiasi kikubwa na
utaratibu uliotumika kuiba mamia ya mabilioni ya fedha za umma kutoka kwenye
akaunti ya madeni ya nje ya Benki Kuu ya Tanzania (EPA) mwaka 2005.
Mheshimiwa Spika, Tarehe
13 Agosti, 2012, Msajili Msaidizi wa Makampuni katika Wakala wa Usajili wa
Makampuni na Leseni (BRELA) alitoa Hati ya Usajili (Certificate iof Incorporation) kwa kampuni inayoitwa Leka Dutigite
Limited. Kwa mujibu wa nyaraka za BRELA, Leka Dutigite Ltd. ina ofisi zake
katika ghorofa ya kwanza ya jengo la City House lililoko katika Mtaa wa Mkwepu,
Dar es SalaaM. Mheshimiwa Spika,
Katiba,
yaani Memorandum and Articles of
Association, ya kampuni ya Leka Dutigite Ltd. iliyosajiliwa BRELA tarehe 13
Agosti, 2012 inaonyesha kwamba mwenye hisa nyingi katika kampuni hiyo ni
kampuni nyingine inayoitwa Gombe
Advisors Ltd. ya Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa taarifa za kibenki ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako
tukufu imezipata, mnamo tarehe 10 Desemba, 2012, Hifadhi ya Taifa ya Saadani
ilihamisha jumla ya shilingi 12,200,000 kwenda kwenye akaunti na. 0150357447800
iliyoko CRDB Bank tawi la Pugu Road, Dar es Salaam, inayomilikiwa na Leka
Dutigite Ltd. Hifadhi ya Taifa ya Saadani inamilikiwa na Mamlaka ya Hifadhi za
Taifa (TANAPA), ambayo ni shirika la umma. Siku moja baadae, fedha hizo
zilitolewa kwa pesa taslimu kutoka kwenye akaunti hiyo.
Baada
ya hapo, kati ya tarehe 14 Januari na 7 Februari, 2013, akaunti ya Leka
Dutigite Ltd. iliingiziwa jumla ya shilingi 28,600,000. Fedha hizi zote
ziliingizwa kama fedha taslimu na mtu aitwaye Mchange (shilingi 3,600,000
tarehe 14 Januari, 2013) na Leka Dutigite (shilingi 25,000,000 tarehe 23
Januari na 7 Februari, 2013). Kufikia tarehe 7 Februari, 2013, fedha hizo zote zilikwishatolewa
benki.
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 28 Februari, 2013, akaunti ya Leka Dutigite Ltd. iliingiziwa shilingi
32,367,000 na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Kwa mujibu wa taarifa
za kibenki, siku hiyo hiyo, fedha hizo zilitolewa kwenye akaunti hiyo. Siku nne
baadae, yaani tarehe 4 Machi, 2013, NSSF ilifanya malipo mengine kwenye akaunti
ya Leka Dutigite Ltd., kwa mikupuo miwili, ya jumla ya shilingi 46,663,000.
Siku hiyo hiyo, fedha hizo nazo zilitolewa kutoka kwenye akaunti hiyo kwa mikupuo
miwili. Kwa hiyo, katika kipindi cha miezi mitatu katika ya tarehe 10 Desemba,
2012 na 4 Machi, 2013, Leka Dutigite Ltd. ililipwa shilingi 119,930,000 kwa
utaratibu huo huo wa ingiza na toa fasta. Kati ya fedha hizo, shilingi
12,200,000 zililipwa na TANAPA na shilingi 79,027,000 zililipwa na NSSF.
Mheshimiwa Spika, Katika
mazingira ya kawaida, sio kitu cha ajabu kwa mashirika ya umma kama NSSF na
TANAPA kufanya biashara na watu au taasisi mbali mbali kama makampuni binafsi.
Ukweli ni kwamba, kwa upande wa malipo yaliyofanywa na TANAPA, Kambi Rasmi ya
Upinzani ya Bunge lako tukufu imeweza kupata nakala ya mkataba unaohusu Maandalizi ya Filamu (Documentary) kwa Ajili
ya Kuhamasisha Shughuli za Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani kwa
Kutumia Wasanii Kutoka Kigoma. Mkataba huo umesainiwa tarehe 5 Desemba,
2012, kati ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Leka Dutigite Ltd. na una thamani
ya shilingi 12,200,000, kiasi kile kile kilicholipwa na Hifadhi hiyo.
Hata
hivyo, Mheshimiwa Spika, mazingira ya malipo haya sio ya kawaida. Hii ni kwa
sababu ya uwepo wa kampuni ya Gombe Advisors Ltd. Kwa mujibu wa nyaraka za
BRELA, kampuni hii ilisajiliwa tarehe 24 Novemba, 2011. Kwa mujibu wa nyaraka
hizo, ofisi za Gombe Advisors Ltd. ziko kwenye jengo la City House, Mtaa wa
Mkwepu, Dar es Salaam, ziliko ofisi za Leka Dutigite Ltd. Kwa mujibu wa nyaraka
hizo, wakurugenzi wa Gombe Advisors Ltd. ni Zitto Zuberi Kabwe ambaye kazi yake
inatajwa kuwa ‘mchumi’, na Raphael Ongangi ambaye anatajwa kuwa ‘mchambuzi wa
fedha na vitega uchumi’ (Financial and Investment Analyst). Bwana Ongangi
aliwahi kutajwa na gazeti la kila wiki la Mawio la tarehe 26 Desemba 2013 kuwa
ni mmoja wa washauri wa Zitto Zuberi Kabwe na anasemekana kuwa msaidizi
wake.
Mheshimiwa Spika,
Zitto Zuberi Kabwe sio ‘mchumi’ anayetajwa katika nyaraka za BRELA zinazoihusu
kampuni ya Gombe Advisors Ltd. pekee, bali pia ni Mbunge, tangu mwaka 2005, wa
Bunge lako tukufu. Kama Mbunge, Mheshimiwa Zitto Kabwe ni ‘kiongozi wa umma’
kwa mujibu Sheria ya Maadili ya Viongozi
wa Umma, 1995. Sheria hii inawalazimu viongozi wa umma, wanapokuwa
madarakani, kuwa “waadilifu, wenye
huruma, utulivu, umakini na watakaoendeleza viwango vya juu vya maadili ili
kujenga na kuendeleza imani ya umma kwa uadilifu wa Serikali.”
Aidha,
viongozi wa umma “... watawajibika
kutekeleza wajibu wao kwa umma na kuendesha shughuli zao binafsi kwa namna
ambayo itaonekana na kuthibitika kuwa ni wazi kwa umma na haitatosheleza kwao
kutekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria tu.” Vile vile, kuhusiana na maslahi
binafsi, Sheria hii inaelekeza kwamba “...
viongozi wa umma hawatakuwa na maslahi binafsi ambayo yanaweza kuathiriwa na
maamuzi ya serikali wanayoshiriki katika kuyafanya.”
Mwisho,
kuhusiana na maslahi ya umma, viongozi wa umma wanatakiwa, pale wanapochaguliwa
au kuteuliwa, kupanga masuala yao “kwa
namna itakayozuia migongano ya maslahi ya wazi, iliyojificha au inayoonekana
kuwepo na pale ambapo migongano hiyo inatokea kati ya maslahi binafsi na
maslahi ya umma basi itatatuliwa kwa kuangalia zaidi maslahi ya umma.” Kwa
kadri ya ufahamu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, Mheshimiwa
Zitto Kabwe hajawahi kutangaza maslahi aliyonayo kwenye mikataba ya Gombe
Advisors Ltd. na Leka Dutigite Ltd. na NSSF na TANAPA.
Mheshimiwa Spika,
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe sio tu ni Mbunge anayebanwa na masharti ya Sheria
ya Maadili ya Viongozi wa Umma, bali pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Fedha za Serikali (PAC). Kwa mujibu wa kipengele cha 12 cha Nyongeza
ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge lako tukufu, mojawapo ya majukumu ya PAC
ni kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma
katika Wizara na Mashirika ya Umma yaliyoainishwa katika taarifa ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. NSSF na TANAPA ni baadhi tu ya Mashirika ya
Umma yaliyo chini ya usimamizi wa kibunge wa PAC.
Kwa
maana hiyo, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zitto Kabwe, kwa kutumia makampuni
yake ya Leka Dutigite Ltd. na Gombe Advisors Ltd., amefanya biashara na TANAPA,
shirika la umma analolisimamia kama Mbunge na Mwenyekiti wa PAC. Mheshimiwa
Zitto Kabwe na wanamuziki washirika wake, kwa kutumia makampuni ya Gombe
Advisors Ltd. na Leka Dutigite Ltd., wamelipwa fedha za umma za TANAPA na NSSF.
Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo juu ya madai ya ukiukwaji wa
Sheria uliofanywa na viongozi wa umma na mashirika ya umma katika kashfa hii.
Pamoja na maelezo yatayotolewa , Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum juu ya matumizi ya fedha
zilizotolewa na TANAPA na NSSF; msukumo uliofanya fedha hizo zitolewe na
matumizi ya fedha hizo kwa kuzingatia
masharti yanayosimamia fedha za umma na utawala bora katika usimamizi wa
fedha za umma. Aidha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
ifanye uchunguzi juu ya malipo na matumizi husika kwa kurejea masharti ya
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Sheria nyingine zinazohusika. Kwa upande mwingine, kwa kuwa suala hili
linahusu mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayohusika na usimamizi wa
fedha za umma, Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge nayo ifanye uchunguzi
wake juu ya madai ya masharti ya Katiba ya Nchi, Sheria ya Haki, Kinga na
Madaraka ya Bunge na Kanuni za Bunge juu ya maadili ya kiongozi wa umma ikiwemo
yahusuyo utangazaji wa maslahi.
Mheshimiwa Spika;
Mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inatoa rai kwa wanamuziki
na wasanii wengine wote nchini kuwa waangalifu na watu wanaotaka kutumia
umaarufu wao kama wanamuziki na wasanii kwa lengo la kufanikisha dili za
kifisadi. Bila kuchukua tahadhari ya kutosha, wasanii hao wanaweza kujikuta
wakipoteza sifa na umaarufu wao ambao wameujenga kwa jitihada zao wenyewe.
4.4
MCHAKATO BUTU WA VAZI LA TAIFA
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni,
Vijana na Michezo, wakati huo chini ya Waziri Dk. Emmanuel Nchimbi, ilifanya
uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Kubuni Vazi la Taifa mwezi Desemba 15,
2011.Kamati hiyo iliyokuwa na watu wanane, Mwenyekiti ni Joseph Kusaga na
Katibu ni Angela Ngowi, pamoja na wajumbe wa kamati hiyo ni Habib Gunze, Joyce
Mhaville, Mustafa Hassanali, Makwaia Kuhenga, Ndesambuka Merinyo na Absalom
Kibanda, ambaye baadaye alitangaza kujiweka kando. Desemba 22, 2011, kamati hiyo ikazinduliwa rasmi na aliyekuwa Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Emmanuel Nchimbi, tayari kuanza
kazi ya kubuni Vazi la Taifa, mchakato ambao ulipaswa kukamilika ndani ya siku
75 tangu siku ya kuzinduliwa kwake. Mhe.Nchimbi
aliahidi kuwa mara baada ya kamati hiyo kukamilisha kazi hiyo ikiwamo kuainisha
mapendekezo mbalimbali ya vitambaa vinavyoweza kufaa, Watanzania watakuwa
wamepata Vazi la Taifa. Siku hiyo
Waziri Nchimbi alisema kazi ya kamati hiyo si kuanza mchakato mpya wa Vazi la
Taifa, bali ni kumalizia mchakato wa kupata vazi la mwanamume na mwanamke
ulioanza mwaka 2004. Hata hivyo, baada ya mabadiliko ya baraza la mawaziri,
tarehe Septemba 10, 2012, Kamati ya Vazi la Taifa chini ya Ndugu
Kusaga ilikabidhi ripoti kwa Waziri Mukangara aliyekuwa na naibu wake, Amos Makalla. Uwasilishaji wa ripoti hiyo ulifanywa na Katibu wa
Kamati ya Vazi la Taifa Angela Ngowi, akiwa na wajumbe wa kamati hiyo, Joyce
Mhaville, Mustafa Hassanali na Ndesambuka Merinyo. Angela akasema katika mchakato wa kupata vazi hilo,
walipokea zaidi ya michoro 200 kutoka kwa wasanii 88 na kupitisha michoro sita
iliyokuwa imekidhi vigezo na kuikabidhi kwa wataalamu wa vitambaa kwa ajili ya
kutoa uamuzi wao. Waziri Mukangara alionesha
shauku yake ya kuona vazi hilo linapatikana haraka na kwamba lingevaliwa katika
maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanganyika ya Desemba 9, mwaka 2012.
Mheshimiwa
Spika, ikiwa
inakaribia kuwa miaka takribani miwili sasa tangu Waziri Mukangara apokee
ripoti hiyo, hakuna vazi lililopatikana wala maelezo mapya juu ya hatima ya
vazi hilo. Kwa vile vazi la taifa limekuwa likisubiriwa kwa shauku kubwa na
Watanzania tangu mchakato huo ulipoanzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2004,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka maelezo ya kina kutoka kwa Waziri ni
nini kimeukwamisha mchakato huo?
4.5 SANAA NA USANII KUTAMBULIWA KAMA
SEKTA YA KIUCHUMI NA ULINZI WA MILIKI BUNIFU KUBORESHWA KUINUA VIPATO VYA
WASANII NA MAPATO KWA NCHI
Mheshimiwa Spika;
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina taarifa juu ya maoni ambayo Wasanii
waliyawasilisha mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na baadaye kwa baadhi ya
wabunge ikiwemo wa upinzani kutaka wasanii watambuliwe kama kundi maalum katika
katiba mpya kama ilivyo kwa wafugaji, wakulima na fani au tasnia nyingine.
Aidha, wasanii wamependekeza kwamba rasimu ya katiba mpya itaje miliki bunifu
(intellectual property).
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na umuhimu wa mapendekezo ya wasanii hao waliyoyatoa kupitia
mashirikisho yao manne Shirikisho la Filamu, Shirikisho la Muziki, Shirikisho
la Sanaa za maonyesho na Shirikisho la Sanaa za ufundi, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inatoa maoni kwa Serikali kwamba haipaswi kusubiri mpaka mchakato wa
mabadiliko ya katiba bali marekebisho ya
msingi ya kisheria yapaswa kuharakishwa kuwezesha sanaa na usanii kuchangia
katika kuongeza ajira, kuboresha maisha ya wasanii na kuchangia kwa kiwango
kikubwa katika mapato ya Serikali na Uchumi wa Nchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika;
Serikali imekuwa ikitazama sanaa kama suala la burudani zaidi badala ya
kuitazama kama ni sekta muhimu ya kiuchumi. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kuzingatia kwamba Wasanii sio wanamuziki tu, wasanii wapo karibu
katika kila kaya Tanzania. Wafinyanzi, wasusi, wapambaji, wanamuziki waigizaji,
mafundi mbalimbali wa ushonaji ujenzi na kadhalika, wako wengi wala hata wao
hawajitambui kama ni wasanii kutokana na mazingira waliyomo.
Mheshimiwa Spika;
Katika ripoti mojawapo ya BASATA ya mwaka 2006, idadi ya wasanii nchini wakati
huo ilikuwa ni milioni 6, ni wazi kuwa idadi hiyo kwa sasa itakuwa
imepanda. Katika miaka ya karibuni
vijana wengi wamekuwa wanaongezeka kujiunga na kundi hili kwani katika sanaa
kumekuwa na uwezekano wa kujipatia ajira, tena isiyokuwa na ukomo. Na hivyo
sanaa kwa sasa si utamaduni peke yake bali ni sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika;
Wasanii ni sehemu muhimu katika sekta ya Hakimiliki, takwimu za ripoti ya
WIPO(World Intellectual Property Organisation) ya mwaka 2010, kuhusu mchango wa
sekta ya hakimiliki katika uchumi wa Tanzania, inaonaonyesha kuwa sekta hii, kati ya 2007-2010 ilichangia
kati ya asilimia 3-4.6% ya gross domestic product(GDP). Na kiasi cha kati ya
TSH 38.930 bilioni na 86.686 billion kilipatikana kama kipato cha walioajiriwa
katika sekta hiyo.
Mheshimiwa Spika;
Kati ya watu 28, 202 na 44, 331 waliajiriwa rasmi, na hiyo ilikuwa kati ya
asilimia 4.5 na 5.2% ya kundi zima la waajiriwa wa Taifa hili. Kwa kipimo cha
GDP, sekta hii ilikuwa zaidi ya sekta ya madini, ambayo wote ni mashahidi
imekuwa katika mazungumzo kila kona ya nchi. Na katika ajira sekta hii ilikuwa
juu zaidi ya sekta nyingi zikiwemo madini, usafirishaji, mawasiliano, afya na
ustawi wa jamii, maji, gesi, na hata ujenzi. Kwa mchango wa sekta hii wa 3.2%
katika GDP kwa mwaka 2009 , umeweka sekta hii kuwa bora kuliko sekta za aina
yake katika nchi kama Croatia 3%,
Singapore 2.9%, Latvia 2.9%, Lebanon 2.5%, Kenya 2.3%. Na katika mchango wa
ajira sekta hii ilikuwa juu ya Romania, Bulgaria, Lebanon, Jamaica, Colombia,
Kenya na Ukraine.
Mheshimiwa Spika; kwa
upande wa Tanzania, Takwimu hizi hazijionyeshi katika takwimu za Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kuwa sanaa bado inaonekana ni burudani
tu, na thamani yake katika uchumi haitiliwi uzito. Kutambuliwa kwa kundi hili
kutawezesha kutungwa sheria na taratibu za kuwezesha Wasanii kuongeza ajira na
mapato, na Taifa kufaidika na uchumi wa
raslimali hii.
Mheshimiwa Spika;
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka marekebisho makubwa kwenye sheria za nchi yetu
kuwezesha kutajwa kwa miliki bunifu katika sanaa, usanii na sekta zote nyingine
muhimu za kiuchumi. Ni muhimu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na
Serikali kwa ujumla ikazingatia kwamba mali ziko za aina tatu. Kuna mali
zinazohamishika, mali zisizohamishika na mali zitokanazo na ubunifu. Aina mbili
za kwanza zimetajwa katika katiba na ulinzi wake hujulikana na ni wa jadi.
Lakini hii aina ya tatu ya mali huwa ni ngumu kuilinda kutokana na mfumo wake
kuwa haushikiki hivyo sheria maalumu hutungwa kulinda aina hii ya mali (IP
Laws).
Mheshimiwa Spika;
Mali zitokanazo na ubunifu kwa sasa ndio mali zenye kipa umbele duniani.
Uvumbuzi wa teknolojia mbalimbali, ugunduzi wa njia mbalimbali za kuboresha
maisha, sanaa na mengi yanayolindwa na milikibunifu, vimeweza kutoa ajira kubwa
na kutoa mchango mkubwa wa kipato kwa wagunduzi na nchi ambazo wagunduzi hao
wamekuwa wakiishi au kuzisajili kazi zao. Kama wasanii, haki zetu katika
milikibunifu zinajulikana kama Hakimiliki, lakini kama Watanzania tunaona ni
muhimu kulinda haki zote za Milikibunifu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika;
Nchi zote ambazo zimeweka taratibu imara za kulinda Milikibunifu duniani,
zimewezesha wabunifu wake kubuni mambo ambayo yameweza kubadilisha maisha ya
binadamu wengine duniani kote. Marekani iliweka kipengele cha Ulinzi wa hakimiliki
katika katiba yake tangu mwaka Agosti 1787, na kazi za wagunduzi wa Marekani
tunaziona kila wakati katika kazi za sanaa na teknolojia. Korea kusini
ilinakiri sehemu ya katiba ya Marekani kuhusu ulinzi wa Milikibunifu kuanzia
mwaka 1948, kwa wakati huu wote ni mashahidi wa bidhaa kama Samsung, Ld Daewoo,
Hyundai na kadhalika.
Mheshimiwa Spika;
Milikibunifu pamoja na kulinda haki katika kazi za sanaa ambazo picha ndogo ya
mapato yake zimetajwa hapo juu, Milikibunifu italinda haki za wabunifu wetu, tafiti
za wasomi wetu, ugunduzi mbalimbali, taratibu mbalimbali za mambo yetu ya
kiasili, dawa za asili za miti yetu, na taratibu za matumizi ya dawa hizo, na
mali asili zetu nyingine nyingi tunazozifahamu na ambazo bado hatujazifahamu .
Mheshimiwa Spika;
Kuna hasara nyingi ambazo hupatikana kama nchi haina ulinzi wa Milikibunifu,
mifano michache hapa Tanzania, ni kupoteza kwa Milikibunifu ya jina Tanzanite,
ambayo licha ya kuwa inachimbwa Tanzania tu lakini jina linamilikiwa na kampuni
ya Afrika ya Kusini. Vazi la kikoi, pamoja kuwa ni la asili ya Tanzania,
milikibunifu imesajiliwa Kenya, staili ya michoro maarufu ya Tingatinga
milikibunifu yake iko Japan. Na haya ni machache ambayo yameshtukiwa
Milikibunifu ikifuatiwa vizuri ndipo haswa ukubwa wa tatizo utakapojulikana.
Kuna ulazima mkubwa wa kutaja Milikibunifu katika sheria zote muhimu na
kuanisha ulazima wa kulinda kuendeleza na kwezesha wabunifu wan chi kwa manufaa
ya kizazi hiki na vizazi vijavyo.
6.0
SEKTA YA MICHEZO NCHINI
6.1
UENDELEZAJI WA VIWANJA VYA MICHEZO NCHINI
Mheshimiwa
Spika, kwa muda mrefu Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeendelea kuona umuhimu wa taifa kuwekeza katika
viwanja vya michezo ili kuweza kupanua wigo wa taifa kujitangaza na kukusanya
mapato yanayotokana na viwanja vya michezo nchini. Labda, wizara mpaka sasa
haijaweza kujua hasara ambazo kama taifa tunapata kutokana na kutotumia nafasi
zinazotokea na kutowekeza vya kutosha katika kuboresha michezo nchini.
Mheshimiwa
Spika, enzi za chama kimoja,
majengo na maeneo yote ya umma yalikuwa chini ya Serikali. Ujenzi na
uendelezaji wa maeneo hayo ulifanya na Serikali kupitia kodi za wananchi,
michango, fedha za wafadhili na wahisani mbalimbali. Hata baada ya uwepo wa
vyama vingi, uendelezaji wa miradi yote iliyokuwa chini ya Chama kimoja
ilifanywa kuwa ni jambo la kitaifa. Kwa namna isiyoeleweka baadhi ya maeneo ambayo
CCM imeshindwa kuyarudisha kwa wananchi na kuwa mali ya umma na kuyafanya ni mali ya chama ni pamoja na Uwanja wa CCM
Kirumba (Mwanza), Samora (Iringa), Sokoine (Mbeya), Sheikh Amri Abeid (Arusha),
Majimaji (Songea), Kaitaba (Kagera) n.k.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na CCM
kuendelea kuhodhi viwanja hivi imeshindwa kuviendeleza na matokeo yake
kuwanyima fursa wananchi wa maeneo husika kushuhudia michezo mbalimbali kwa
kuwa viwanja hivyo huwa havikidhi viwango vya ubora vya michezo hali inayofanya
michezo mingi mikubwa ikiwemo ya kimataifa kufanyika Dar Es Salaam pekee. Kambi rasmi ya upinzani inarudia tena kuitaka
Serikali kuvirudisha viwanja vyote vilivyohodhiwa na CCM kwa wananchi ili
viendelezwe kwa kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Michezo nchini kama
tulivyopendekeza mwaka jana.
Mheshimiwa
Spika, kitendo cha Mechi ya
Taifa Stars na Zimbabwe kuhamishwa kutoka uwanja wa Sokoine Mbeya tarehe 18 Mei
na kuhamishiwa uwanja wa Taifa Dar Es Salaam, kwanza kimewavunja moyo mashabiki
wa mpira na wakazi wa Mbeya ambao walijiandaa kuonesha uzalendo kwa taifa lao.
Kutokana na kitendo cha mechi hii kuhamishwa, Wanambeya walikoseshwa fursa za
kujitangaza kiutalii na hatimaye kuchangia katika uchumi kulikosababishwa na
Serikali ya CCM kuendelea kuhodhi viwanja vya michezo nchini. Rudisheni viwanja
vya wananchi ili viendelezwe na kuwanufaisha wananchi.
6.2 KASUMBA
YA MPIRA WA MIGUU KUWA MCHEZO PEKEE WA KIPAUMBELE.
Mheshimiwa
Spika, kama Waziri kivuli
mwenye dhamana ya kuisimamia Serikali katika masuala ya habari, vijana,
utamaduni na michezo. Lakini ni dhahiri kuwa Wizara hii imeshindwa kusimamiwa
ipasavyo katika sekta ya michezo,huku soka peke yake ikifanywa kuwa ni mchezo
unaopewa kila aina ya msaada na kuidharau michezo mengine. Kwa kifupi ni kuwa,
Tanzania ina hazina kubwa ya wanamichezo ambao hawajatumika ipasavyo na wala
Serikali haijawekeza vya kutosha katika kuhakikisha kuwa aina nyengine za
michezo zinapewa kipaumbele. Kwa mfano, Filbert Bayi ni mwanariadha wa Tanzania
ambaye alililetea taifa sifa kubwa kwa kushinda medali ya dhahabu mwaka 1974,
tunaye mchezaji wa mpira wa kikapu nchini Marekani Hasheem Thabit anayechezea
NBA.
Mheshimiwa
Spika, kama taifa kushindwa
kuwa na orodha ya wana michezo ambao wamefanya vizuri katika medani ya michezo
duniani na kuweza kuwahesabu kwa uchache wao, kunazua maswali mengi sana si
kwetu tu bali hata kwa wadau wa michezo nchini ikiwa Serikali ina nia ya dhati
ya kuendeleza michezo kwa ujumla.
6.3 MAKOCHA WA KIGENI NA
MUSTAKABALI WA MICHEZO NCHINI
Mheshimiwa Spika, kwa
muda mrefu tumekua tukionesha wasiwasi kwa uamuzi wa Serikali kuendelea
kuwaabudu makocha wa kigeni katika
michezo. Hali hii si tu kuwa inadumaza soka, bali pia inavunja nguvu makocha
wazawa pamoja na kuwakatisha tamaa vijana ambao wamekua na ndoto za kuwa
makocha hapa nchini. Hii imekua ni Kasumba ambayo ina athari katika maendeleo
ya michezo hapa nchini. Pamoja na makocha wa kigeni kuabudiwa na baadhi ya
viongozi wa michezo na wa kitaifa , makocha hawa wamekuwa na dharau kwa makocha wa nyumbani hali ambayo
inadumaza maendeleo haya ya michezo. Imekuwa ni kawaida hata kwa baadhi ya
viongozi wa soka wa klabu zetu na hata timu ya taifa kuwathamini na
kuwatetemekea makocha kutoka nje pamoja na kwamba tuna zaidi ya miaka 15 sasa
na mlolongo mrefu wa makocha wa kigeni, lakini hawajaweza kuleta mafanikio
makubwa yanayostahili majina makubwa ya klabu zetu na timu zetu za taifa.
Mheshimiwa Spika,
umeshuhudia mara nyingi makocha kutoka nje wakiletwa nchini na kupokelewa na
maandamano na shangwe na wanachama na wapenzi wa klabu husika kukifuatwa na
kupewa mishahara minono, usafiri wa uhakika na nyumba za kisasa za kuishi. Kuna
kocha wa timu mojawapo kubwa ya Tanzania alitaka nyumba atakayopewa kuishi
lazima iwe na bwawa la kuogelea, na akapewa. Hii ni sawa na kuwa mtumwa ndani
ya nyumba yako mwenyewe. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji ni nini
ambacho makocha wa kigeni wanancho ambacho makocha wazawa hawana kinachofanya
Serikali itenge kiasi cha shilingi Bilioni
1.6 kwa ajili ya malipo ya makocha wa kigeni kwa timu za taifa na matumizi
ya kawaida ya BMT bila mchanganuo? Je, kwanini Serikali inaendelea kuajiri
makocha wa kigeni wakati nchi kuna makocha wenye uwezo wa kufundisha timu za taifa?
Je, ni kwanini serikali na wizara hii inasita kuwafadhili kimasomo makocha
wazawa nje ya nchi ili waweze kutumikia taifa lao pindi wakimaliza masomo na
mafunzo yao?
6.4 MWENENDO WA MCHEZO WA RIADHA
Mheshimiwa Spika; Tanzania imewahi kupata heshima
kubwa kimataifa kutokana na mchezo wa riadha.Hata hivyo, katika mchezo huu pia
nchi yetu iko katika ‘chumba cha wagonjwa mahututi’. Hali hiyo, inachangiwa na udhaifu wa
kiuongozi, kisera, kimikakati na kioganizesheni kwenye mchezo wa riadha nchini
kuanzia ngazi za chini mpaka taifa.
Kambi
Rasmi ya Upinzani inaamini kwamba taifa letu linaweza kutolewa ‘kimasomaso’ na
mchezo huu iwapo katika mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2013/2014 na
makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2014/2015 riadha itapewa kipaumbele
katika mjadala.
Mheshimiwa Spika; Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo imekuwa ikitoa maelezo bungeni kwamba riadha nchini inaendelezwa
kupitia wadau mbalimbali ikiwemo Chama Cha Riadha Tanzania (RT). Hata hivyo,
Wizara haijawahi kutoa majibu kamili bungeni namna inavyoshughulikia migogoro
na matatizo ya kiuongozi na kiutendaji katika chama tajwa hali ambayo inaathiri
mustakabali mwema wa mchezo wa riadha nchini.
Kambi
Rasmi ya Upinzani inataarifa kwamba kabla na hata baada ya uchaguzi wa Chama
Cha Riadha Tanzania (RT) uliofanyika Morogoro tarehe 20 Mei 2012 kwa nyakati
mbalimbali kumekuwepo malalamiko ya wadau wa mchezo huo juu ya uhalali wa
uchaguzi huo pamoja na hali tete ya maendeleo ya mchezo huu. Hivyo, Kambi Rasmi
ya Upinzani inaitaka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ujibu
bungeni maswali muhimu yafuatayo kuhusu mustakabali mwema wa riadha nchini:
Mheshimiwa Spika; Mosi, Baada ya kufanya vibaya
katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika London 2012 zilitolewa kauli na
ahadi mbalimbali na Wizara na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ya kufanya
maandalizi bora kuelekea 2016 Rio De Janeiro Olympics; Wizara na Baraza la
Michezo Tanzania (BMT) wanalihakikishia vipi bunge kwamba maandalizi
yamekamilika kuondoa ‘ukame’ wa medali na ‘aibu’ kwa taifa?
Mheshimiwa Spika; Pili, Kambi Rasmi ya Upinzani
inafahamu kwamba kama sehemu ya diplomasia ya michezo Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa alilieleza bunge kwamba kwa kushirikiana na Wizara ya
Habari, Vijana na Michezo ilipeleka vijana 50 pamoja na walimu wao kwenye
makambi ya mafunzo katika nchi mbalimbali ikiwemo New Zeland. Baadhi ya vyombo
vya habari viliripoti kwamba mwanariadha Atson Mbugi na Kocha Samwel Tupa nao
wapo nchini New Zeland kwenye mazoezi. Hata hivyo, taarifa zilizoifikia Kambi
Rasmi ya Upinzani ni kwamba wapo Tanga na Arusha. Je, ni kwanini wameachwa,
wakina nani wamepelekwa badala yao na ni kwanini taarifa za uongo zilitolewa
kwenye vyombo vya habari? Ni muhimu kwa Bunge kupewa taarifa kwa kuzingatia
kuwa kwa nyakati mbalimbali zimekuwepo kashfa za wanamichezo wasio na viwango kupewa nafasi za
wenye vipaji na hatimaye kwenda kulisababishia aibu taifa. Aidha zimekuwepo pia
kashfa za wengine kupenyezwa kwenye misafara ya wanamichezo kwa ajili ya kubeba
biashara haramu yakiwemo madawa ya kulevya.
Tatu;
Wizara na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) walichukua hatua gani baada kupokea
tahadhari ya wanariadha na wataalamu wa
riadha juu ya madai ya uchaguzi wa chama hicho kuelekea kufanyika kinyume na
Sheria na. 12 ya Baraza la Michezo ya mwaka 1967 kabla ya Mwenyekiti wa BMT
Dionis Malinzi na Mkurugenzi wa Michezo Leonard Thedeo kwenda kusimamia
Uchaguzi huo?
Mheshimiwa Spika; Nne; mara baada ya uchaguzi huo
yapo malalamiko ambayo yaliwasilishwa kwa Waziri yenye kuwasilisha maelezo na
vielelezo kuhusu namna uchaguzi huo ulivyokiuka sheria; je, ni sababu zipi
zilizoifanya Wizara kutokutoa majibu yoyote juu ya madai hayo?
Tano;
Inadaiwa kwamba viongozi wa Chama cha Riadha Tanzania (RT) walisaini
Makubaliano ya Maelewano (MOU) mbele ya Viongozi wa Wizara na BMT kwamba
marekebisho bora ya katiba ya chama hicho yangefanyika ndani ya siku tisini
ambazo zilimalizika tarehe 20 Agosti 2012. Hata hivyo, taarifa ambazo Kambi
Rasmi ya Upinzani imeelezwa ni kwamba marekebisho hayo yaliyopaswa kuwezesha
mustakabali mwema wa riadha nchini hayajafanyika. Je, Wizara imechukua hatua
gani kwa chama hicho na viongozi wake kwa kwenda kinyume na makubaliano hayo?
Mheshimiwa Spika; Sita; Chama Cha Riadha Tanzania
(RT) kimekuwa kikipokea fedha za maendeleo ya mchezo wa riadha kutoka
Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kwa ajili ya mashindano ya kitaifa na
kimataifa. Aidha, Kamati ya Olimpiki (TOC) nayo imekuwa ikipokea fedha kutoka
vyanzo mbalimbali kwa ajili ya pamoja na mambo mengine maandalizi ya wanariadha
kwa ajili ya mashindano hayo. Kwa ujumla riadha imekuwa pia ikichangiwa kwa
ajili ya maandalizi ya All African Games. Hata hivyo, pamoja na vyanzo hivyo,
RT imeburuzwa katika mahakama ya Temeke kwa deni la milioni ishirini ambalo
maelezo yake yana utata. Hali hii inaacha maswali kuhusu mapato na matumizi
katika RT na TOC. Je, Wizara na BMT wako tayari kuwasilisha nakala ya taarifa
zote za mapato na matumizi
yaliyokaguliwa ya RT na TOC ya miaka ya fedha 2012/2013 na 2013/2014?
Mheshimiwa Spika; Kwa hali hiyo tete na tata ya
kifedha ambayo inasababisha hata wakati mwingine wanariadha wa Tanzania kukosa
vifaa vinavyostahili, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka maelezo kutoka kwa Wizara
na BMT, ni nini kilisababisha udhamini wa kampuni ya Lining ya China kwa RT na
wanariadha wetu wa toka mwaka 2007 kusitishwa? Je, uamuzi wa TOC kuingia
mkataba mwingine na PUMA bila kujadili masharti ya mkataba mwingine uliokuwepo
uliathiri vipi mkataba wa awali kwa kuzingatia kwamba yapo madai ya baadhi ya
wadau wa riadha kwamba ilikuwa mikataba ya ‘mtaka yote mkosa yote’?
Mheshimiwa Spika; Kwa kuzingatia uzito wa maswali
hayo, pamoja na majibu yatakayotolewa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo katika majumuisho; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ifanye uchunguzi wa masuala haya na
mengine yanayohusu RT na TOC ili kuwezesha mustakabali mwema wa mchezo wa
riadha nchini. Hata hii italiwezesha bunge kupokea taarifa na kupitisha
maazimio yatakayorudisha heshima ya taifa letu kimataifa katika mchezo wa
riadha.
7.0 MBIO
ZA MWENGE
Mheshimiwa
Spika, kwa mufa mrefu Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni imekua ikipingana na utumiaji wa fedha za walipa kodi
na kitendo cha Serikali kuendelea kuwatoza wananchi kwa mashinikizo bila ridhaa
zao kuchangia shughuli za mbio za Mwenge wa Uhuru. Ni kweli kuwa Mwenge wa
uhuru ni hazina kwa taifa letu jambo ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inakubaliana nalo na kwa muda mrefu tumependekeza Mwenge wa uhuru uwekwe katika
makumbusho ya taifa ili kuweza kuwapatia fursa wananchi kuweza kujifunza hapo.
Mheshimiwa
Spika, Suala la kuenzi
utamaduni wa Taifa ni la lazima lakini kuendelea kutumia gharama kubwa kwa
jambo hili wakati Watanzania wengi hawana huduma muhimu ni dharau kubwa. Aidha,
katika kipindi hiki ambacho mwenge wa uhuru unapitishwa katika sehemu
mbalimbali za nchi, chama tawala nacho kinapita katika maeneo mbalimbali ya
nchi kuangalia utekelezaji wa ilani yake pamoja na kuzindua miradi ya maendeleo
ya wananchi. Huu ni usanii mkubwa unaofanywa na Serikali ya CCM kwa dhumuni la
kuwanyonya watanzania masikini kwa kigezo cha kuwa wanachangia shughuli za
maendeleo wakati ukweli ni kuwa watanzania wanachangishwa mpaka fedha kwa ajili
ya malazi na chakula kwa wakimbiza mwenge kama alivyojibu Waziri Mkuu. Na kwa
kuwa kumekua na malalamiko kutoka wa wafanyabiashara, wafanyakazi wa Serikali
na hasa walimu sehemu mbalimbali nchini kuwa wanalazimishwa kuchangia mwenge
bila ridhaa yao. Na kama CCM inataka bado mambo ya mbio za mwenge basi wagharamie wenyewe
kwa asilimia 100 na si kuwalazimisha wananchi kuchangia hasa ukizingatia kuwa
Waziri Mkuu alitoa kauli wiki hii kuwa kuchangia mbio za mwenge wa uhuru ni
hiyari. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kusisitiza kuwa sasa
ni wakati muafaka mwenge wa uhuru kupelekwa jumba la Makumbusho ya Taifa.
8.0
HITIMISHO
Mheshimiwa
Spika, napenda kuhitimisha
hoja za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na michezo kwa kulitaka Bunge lako tukufu kuishinikiza Wizara
kutekeleza maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo Wizara imekua
ikiyakubali kwa muda wa miaka mitatu mfululizo.
Aluta
Continua.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha
…………………………………………..
Joseph Osmund Mbilinyi (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya
Upinzani-Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo.
29.05.2013
No comments:
Post a Comment