Katika nchi yenye mfumo
wa demokrasia ya kweli ambapo viongozi wa Serikali wanachaguliwa katika Chaguzi
zilizo huru na za haki, sera ya maendeleo ya Taifa ni mkataba kati ya Serikali
na wananchi. Serikali ikishindwa kutimiza mkataba huu, wananchi wanaiwajibisha
Serikali katika uchaguzi kwa kuiondoa madarakani.
Bajeti ni nyenzo muhimu
ya sera ya Serikali yeyote. Bajeti ni kielelezo cha maeneo ambayo Serikali
inayapa kipaumbele. Bajeti ni kioo cha mapato na matumizi kinachoonesha maeneo
ambayo Serikali inayapa kipaumbele.
Serikali yapaswa
kukusanya mapato toka kwa walipa kodi kwa uadiifu na kupanga na kutumia mapato
hayo kwa uangalifu katika maeneo yatakayotoa huduma bora kwa wananchi na
kuchochea maendeleo.
Malengo ya uchumi mpana
ni kukuza uchumi, matunda ya kukua kwa uchumi yawafikie wananchi wote, na
uchumi usiyumbishwe kwa mfumko wa bei, ukosefu wa fedha za kigeni na thamani ya
sarafu kuporomoka au kupanda sana. Uchumi unapoyumbishwa na mfumko mkubwa wa
bei au thamani ya sarafu kubadilika badilika kwa kiasi kikubwa unapunguza
motisha kwa sekta binafsi ikiwa ni pamoja na biashara ndogo na za kati kuwekeza
na kwa hiyo kukuza uchumi wa kuongeza ajira.
Ili uchumi usiyumbe ni
muhimu kuwa na nidhamu katika sera za mapato na matumizi ya sekta ya fedha za
umma.
Madhumuni ya sera bora ya matumizi ya fedha
za umma ni kuwa na nidhamu katika matumizi (fiscal discipline), kupanga na
kutumia fedha kufuatana na vipaumbele vya sera na kuwa na usimamizi mzuri wa
matumizi haya siku hadi siku.
Usimamizi mzuri wa siku
hadi siku unasisitiza kuwepo kwa tija katika matumizi ya Serikali. Gharama za
kununua bidhaa na huduma ziwe za chini huku ukizingatia ubora wa bidhaa na
huduma zenyewe. Matumizi ya Serikali yafanikishe malengo ya sera kwa mfano
fedha zilizotengwa katika sekta ya elimu zifanikishe watoto wapate elimu iliyo
bora.
Nidhamu katika mapato na
matuizi kunategemea makadirio mazuri ya mapato na matumizi.
Bajeti isiyotabirika
inahujumu vipaumbele vya sera na matokeo ya matumizi ya Serikali. Ikiwa fedha
za kununulia madawa hazipatikani kwa wakati malengo ya kuendeleza na
kuboresha afya za wananchi hayawezi kufikiwa.
Uwajibikaji wa kweli
unasehemu mbili. Sehemu ya kwanza ya uwajibikaji na wajibu wa kutoa maelezo ya
utekelezaji wa mambo muhimu uliyopewa kwa wadhifa ulionao. Viongozi wa Wizara,
Idara za Serikali na Mashirika ya Umma wanawajibika kutoa maelezo ya matumizi
ya fedha ya Serikali katika maeneo yao na malengo gani yamefikiwa katika
matumizi hayo. Sehemu ya pili ya uwajibikaji ni kuwepo na motisha wa
kutambuliwa kwa utekelezaji na matumizi mazuri ya fedha za Umma na kufikia
malengo na kibano kwa utekelezaji mbovu na kutofikia malengo.
Hapawezi kuwa na
uwajibikaji wa kweli bila kuwepo na motisha na kibano kufuatilia tathmini na
uhakiki wa matumizi ya fedha na malengo yaliyofikiwa.
Uwajibikaji unahitaji
kupata maoni ya wananchi wanaotumia huduma za Serikali kuhusu ubora wa huduma
hizo ikiwa ni pamoja na huduma ya miundo mbinu kama vile barabara, maji,
umeme na kadhalika na huduma za jamii kama vile elimu na huduma za afya.
Katika shuguli za bajeti
utekelezaji wa majukumu utakuwa umefanikiwa ikiwa malengo yaliyowekwa
yamefanikiwa kwa mafungu ya fedha zilizotengwa bila kuathiri ubora wa malengo
yenyewe na kuheshimu taratibu na sheria zilizowekwa.
Usimamizi wa matumizi ya
fedha za Umma ulenge katika kupanga na kuyapima matokeo ya matumizi ya fedha
hizo.
Ufisadi ni tatizo katika
matumizi ya fedha za Umma. Lengo moja la kuboresha matumizi ya fedha za
umma ni kupunguza mianya ya rushwa na inapotokea kuhakikisha wanaohusika
wanachukuliwa hatua kali. Pamoja na kuporomosha maadili ya nchi, ufisadi
unadhoofisha nidhamu katika matumizi ya fedha za Umma, unaharibu mgao wa fedha
za umma katika sekta na maeneo mbali mbali ya matumizi na unapunguza tija na
ufikiwaji wa malengo ya matumizi ya fedha za umma. Ufisadi ni matumizi mabaya
ya wadhifa uliopewa kwa manufaa binafsi.
MISINGI MIZURI YA BAJETI
Bajeti ya Serikali
ijumlishe mapato na matumizi yote ya Serikali bila kujali taratibu maalum za
kuendesha baadhi ya miradi na programmu, taratibu za kuidhinisha matumizi na
vyanzo vya mapato.
Kwa ujumla mapato yote
yakusanywe na matumizi kupangwa bila kujali chanzo cha mapato. ikiwa kuna
mahusiano ya karibu kati ya mapato na wanaonufaika na matumizi ya mapato hayo,
hoja ya mapato husika kulipia matumizi ya huduma inakubalika.
Maamuzi ya Serikali na
viongozi ambayo yanahitaji matumizi ya fedha za Serikali katika mwaka wa bajeti
au miaka ijayo yawekwe wazi na kuchambuliwa.
Utayarishaji wa bajeti
uzingatie:-
i) Kufikia
malengo ya uchumi mpana. Ukuaji wa pato la taifa, mfumko wa bei, akiba ya fedha
za kigeni, thamani ya sarafu.
ii) Matumizi
yagawiwe kulingana na malengo ya sera ya taifa.
iii) Kujenga
mazingira ya utekelezaji mzuri wa bajeti.
Jambo linaloathiri sera,
utayarishaji na utekelezaji wa bajeti bora ni uanzishaji wa sera na utamkaji wa
ahadi katika majukwaa ya siasa ambao hayaendani na vipaumbele vilivyotumiwa
kuandaa bajeti.
Bajeti ni kioo cha sera
za Serikali. Ni muhimu kwa bajeti kuwa na mahusiano na sera. Ili kuwa na bajeti
nzuri ya nchi ni muhimu:-
i. Kuratibu
vizuri uanzishaji wa sera
ii. Kushirikisha
umma katika kuanzisha sera
iii. Kuwa
na utaratibu mzuri wa kupitia na kutathmini sera na bajeti za Serikali katika
bunge.
iv. Uchambuzi
wa kina wa mahitaji ya fedha na rasilimali nyingine ya mapendekezo ya bajeti na
kuhakikisha kuwa bajeti ndiyo inayoshika hatamu katika mapato na matumizi ya
Serikali.
Maandalizi ya bajeti
yazingatie hali halisi ya uchumi. Ni muhimu kuwa na makadirio sahihi ya mapato
na kuyatambua matumizi yote ya lazima.
Uandaaji wa bajeti uanze
kwa kutambua mapato yatakayopatikana katika kipindi cha bajeti. Wizara na idara
zijulishwe mapema viwango vya juu vya matumizi katika maeneo yao. Wizara na
Idara zikadirie gharama za matumizi yao kufikia malengo yaliyowekwa huku
wakizingatia ukomo wa matumizi yaliyowekwa.
Mfumo wetu wa Bunge
tumeurithi toka Uingereza. Mamlaka na madaraka ya Bunge katika masuala ya
bajeti ni mdogo sana. Madaraka ya Bunge ni kutathmini utekelezaji kama ulifuata
bajeti iliyopita. Bunge halina mamlaka ya kuandaa Bajeti. bunge halina madaraka
ya kuanzisha muswada wowote utakaohitaji matumizi ya fedha za Serikali.
Hali halisi ya Tanzania ni kwamba
utayarishaji wa bajeti unategemea kikundi kidogo cha wataalamu wa Tanzania
katika Wizara ya Fedha na Benki Kuu, na Wataalamu wa Mashirika ya misaada hasa
Benki ya Dunia, Shirika la Fedha na kimataifa, na mashirika toka nchi za
Jumuiya ya Ulaya. Bunge na Kamati zake hazina mamlaka ya kubadilisha bajeti ya
Serikali.
TATHMINI YA MALENGO MAKUU YA SERA ZA
SERIKALI
Kila bajeti, Serikali inaeleza katika
hotuba ya bajeti kuwa Misingi na shabaha ya Bajeti imezingatia Dira ya Taifa ya
Maendeleo ya 2025 ambayo inalenga kuwa Tanzania iwe ni nchi yenye kiwango cha
kati cha mapato (middle income country) na hali bora ya maisha kwa wananchi;
Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010; MKUKUTA, Mpango wa
Maendeleo ya miaka 5 na Malengo ya Maendeleo ya Milenia. Hata hivyo Waziri
hafanyi uchambuzi wa kina kuonyesha jinsi sera za bajeti na matumizi ya
serikali yanatekeleza mikakati hiyo, mafanikio yaliyofikiwa, vikwazo vilivyopo
na vinavyokabiliwa na serikali.
Kwa mfano Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM
iliahidi kujenga kituo cha kufua umeme wa MW 300 Mnazi Bay Mtwara. Kwa
kuzingatia Ilani ya CCM, Rais Kikwete ambaye ndiye Mwenyekiti wa Tume ya
Mipango aliwaeleza Watanzania katika hotuba yake yakuukaribisha mwaka mpya
tarehe 31 Desemba 2010 aliwaeleza Watanzania kuwa na ninanukuu “Kwa
kushirikiana na sekta binafsi pia, ndani ya miezi 36 ijayo TANESCO wanatarajia
kukamilisha ujenzi wa vituo vya umeme huko Kinyerezi (MW 240) Somanga Fungu (MW
230) na Mtwara (MW 300). Inatarajiwa pia kwamba katika kipindi hicho mradi wa
kuzalisha MW 200 pale Kiwira utakamilika.”
Sasa ni miezi 42 toka Rais Kikwete
atamke maneno hayo Bajeti inayotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeifikisha
wapi miradi hii? Wananchi wa Mtwara walipouliza mradi wa kufua umeme Mtwara
umefikia wapi? Majibu ya CCM ilikuwa kuwapiga na kuwawekea utawala wa kijeshi.
Ni vyema Mawaziri wakawa waungwana kama alivyokuwa Rais Mkapa mwaka 1996
alipoeleza kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM haitekelezeki.
MKUKUTA uliweka lengo la kufikia ukuaji wa
uchumi wa asilimia 10 kwa mwaka. Hotuba za bajeti zinaeleza kuwa Bajeti
inazingatia malengo ya MKUKUTA lakina hakuna uchambuzi unaoeleza kwa nini lengo
la kukuza uchumi kwa asilimia 10 halijafikiwa.
Waziri ameeleza kuwa Bajeti hii imelenga
kupunguza gharama za maisha ya wanachi kwa kuendelea na jitihada za kudhibiti
na kupunguza mfumuko wa bei. Wananchi wengi wanaona kuwa gharama za maisha
zinapanda kwa kasi ya juu kuliko takwimu zinazotolewa na serikali.
Takwimu za
fahirisi ya bei zinaonyesha kuwa kati ya 2007 na 2012 bei zimeongezeka
kwa asilimia 70.5 lakini Hosehold Budget Survey ya mwaka 2012
ukilinganisha na ya 2007 zinaonyesha kuwa bei zimeongezeka zaidi ya mara 2.
Gharama za maisha zinaongezeka kwa kasi kubwa na Watanzania wengi wanahisi kuwa
serikali inawakejeli inapojigamba kuwa inadhibiti gharama za maisha.
Misamaha ya kodi
Mwaka 2011/12 serikali ilipoteza mapato ya
shilingi bilioni 1800 kwa sababu ya misamaha ya kodi. Mwaka 2013/14 mapato ya
zaidi ya shilingi bilioni 2100 hayakuingia katika mfuko wa serikali kwa sababu
ya misamaha ya kodi. Ninaunga mkono uamuzi wa Serikali kuwa na utaratibu wa
kutoa tarifa ya misamaha ya kodi kila robo mwaka kwa kuwatangaza walionufaika
na misamaha kwenye Tovuti ya Wizara ya Fedha.
Utaratibu huu ulianzishwa katika
uongozi wa Rais Mkapa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete – wakati huo akiwa Waziri wa
Mambo ya Nje, alikuwa miongoni mwa watu walioorodheshwa kunufaika na misamaha
ya kodi baada ya kuingiza nchini magari ya kifahari. Serikali ya wawmu ya nne
iliposhika hatamu za uongozi mwaka 2005 ilifuta utaratibu wa kuorodhesha,
wananchi, kampuni na taasisi zilizosamehewa kodi. Kuweka wazi misamaha ya kodi
kunaweza kusaidia kudhibiti misamaha ya kodi na kutawawezesha wananchi kuwa na
taarifa za misamaha na kuweza kudai kwa sauti kubwa kufutwa kwa misamaha ya
kodi
Ili kujenga utamaduni wa kulipa kodi kuwa
ni ishara ya uzalendo ni muhimu misamaha ya kodi ya viongozi wa serikali
wakiwemo Wabunge, Mawaziri na Rais iondolewe. Ni vigumu kwa viongozi ambao
hawalipi kodi kuwahamasisha wananchi kuwa Wazalendo na kulipa kodi.
Hatua ya Waziri kuondoa mamlaka yake ya
kutoa misamaha ya kodi ni jambo jema.
Serikali inaandaa Muswada wa Sheria ya
Bajeti na utakamilika kabla ya mwisho wa mwaka 2014/15. Sheria hii
inalenga kuongeza nidhamu ya matumizi na uwajibikaji kwa wadau wote
wanaotekeleza Bajeti ya Serikali. Sheria hii ilipaswa kuandaliwa mapema katika
uongozi wa Rais Kikwete. Ni vigumu kuwa na sheria nzuri ya bajeti katika mwaka
wa mwisho wa uongozi wa Rais aliyeko madarakani ambayo kimsingi sheria hiyo
itabidi itekelezwe na serikali inayokuja. Ili sheria nzuri ya bajeti itekelezwe
ni muhimu kuacha utaratibu wa cash budget.
Utekelezaji wa miradi chini ya viwango.
Serikali imetambua tatizo la utekelezaji wa
miradi chini ya viwango. Waziri ameeleza kuwa “Katika kuhakikihsa kuwa thamani
ya fedha inawiana na uwekezaji katika miradi husika, Serikali imenunua vifaa
vya kuhakiki ubora wa miradi ya maendeleo.”
Hata hivyo haikuelezwa utaratibu
gani uliotumiwa kuamua kununua vifaa hivyo na taasisi gani itakayotumiwa
kuhakiki ubora wa miundombinu. Miundombinu ni ya aina nyingi. Kuna barabara,
bandari, majengo, mabomba ya maji, mabomba la gesi, mabwawa, mashine za aina
mbalimbali. Vifaa gani vinavyoweza kuhakiki aina mbalimbali za miundombinu.
Kuna tatizo la baadhi ya watendaji serikalini kuchangamkia ununuzi wa vifaa kwa
mategemeo ya kupata commission kuliko malengo ya kuongeza ufanisi.
Waziri kaeleza kuwa “Serikali imeamua
kuzingatia ununuzi wa pamoja (bulk procurement) kutoka kwa wazalishaji badala
ya wakala kama ilivyo sasa na hatua imeanza kuchukuliwa ili ununuzi wa mgari na
vyombo vya TEHEMA ufuate utaratibu huo” Siku za nyuma serikali iliamua kununua
mafuta ya petroli na dizeli kwa pamoja - bulk procurement, lakini Waziri
hajaeleza utaratibu huu umefikia wapi na tumejifunza nini?
Waziri amependekeza hatua nyingine ya
kudhibiti matumizi ya umma kwa kuunganisha matumizi yote ya wizara, idara za
Serikali zinazojitegemea, sekretarieti za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa
na wakala na taasisi za Serikali chini ya mfumo mmoja wa udhibiti wa fedha za
Serikali unaosimamiwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali. Utaratibu wa Single Treasury
Account kusimamia matumizi ya serikali ni jambo zuri lakini linahitaji
maandalizi ikiwa ni pamoja na kufunga akaunti nyingi zinazotumiwa na wizara,
idara na asasi nyingine za serikali. Wizara na Idara nyingi zimeendelea
kufungua akaunti mpya. Kuna wizara zinazopinga Hazina kusimamia ulipaji wa
makandarasi wanaotekeleza miradi ya maendeleo.
Utekelezaji wa Treasury Single
Account unahitaji kuungwa mkono kikamilifu na Rais. Hata ofisi ya Rais itumie
utaratibu unaosimamiwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali. Waziri ana uhakika wa
kuwepo na utashi wa kisiasa wa kutekeleza utaratibu unaopendekezwa?
Bajeti ya 2013/14
Tatizo la msingi la bajeti ya 2013/14 ni
kuwa makadirio ya mapato ya ndani na misaada na mikopo ya nje yalikuwa makubwa
kuliko hali halisi ilivyojitokeza. Matumizi yote yalikadiriwa kuwa shilingi
bilioni 1824.9. Lakini kwa sababu ya upungufu wa mapato matumizi yote
yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 17097.7. Matumizi halisi ni kidogo kuliko
bajeti kwa shilingi bilioni 1152.2 sawa na asilimia 6.3 ya bajeti
iliyoidhinishwa na Bunge.
Bunge liliidhinisha ukusanyaji wa mapato ya
ndani ufikie shilingi bilioni 11154.1. Mpaka ifikapo Juni 30 2014 serikali
inatarajia kukusanya shilingi bilioni 10098.7 ambazo ni shilingi bilioni 1055.4
sawa na asilimia 9.5 chini ya makadirio ya bajeti. Misaada na mikopo ya bajeti
ilikadiriwa kuwa shilingi bilioni 11631.3 lakini serikali inatarajia kupata
shilingi bilioni 988.7 ambazo ni shilingi bilioni 174.5 sawa na asilimia 15 chini
ya bajeti. Serikali ilikadiria kupata shilingi bilioni 1796.9 kama misaada na
mikopo ya miradi. Fedha ya misaada na mikopo ya miradi iliyopatikana kwa mwaka
wa bajeti wa 2013/14 ni shilingi bilioni 922.3 ambazo ni shilingi bilioni
874.6 sawa na asilimia 48.7chini ya bajeti.
Bajeti ya 2013/14 ilipanga kutumia shilingi
bilioni 12574.9 kama matumizi ya kawaida. Matumizi halisi ya kawaida
yanatarajiwa kuwa shilingi bilioni 12085.2 ambayo ni chini ya makadirio ya
bajeti kwa shilingi bilioni 489.7 sawa na asilimia 3.9.
Takwimu za jumla za bajeti ya kawaida
hazioneshi picha halisi ya matatizo ya bajeti. Mfuko wa CFS ambao hutengewa
fedha za kulipia madeni na matumizi ya pensheni na hifadhi ya jamii ulikadiriwa
shilingi bilioni 3319.2 lakini matumizi halisi ya mfuko huu yalikuwa shilingi
bilioni 4251.5 ambalo ni ongezeko la shilingi bilioni 932.4 sawa na asilimia
28.1 ya makadirio ya bajeti. Katika mfuko huu wa CFS fedha iliyotengwa kulipia
madeni ilikuwa shilingi bilioni 2535.7 lakini fedha iliyotumiwa kulipia madeni
ilikuwa shilingi bilioni 3223.1 ongezeko la shilingi bilioni 687.4 sawa na
ongezeko la asilimia 27.1 ukilinganisha na bajeti. Madeni ya serikali
yanayostahiki kulipwa hujulikani vizuri wakati bajeti inaandaliwa.
Hakuna
ulipaji wa dharura wa madeni. Inakuwaje wakati matumizi mengine yanapunguzwa,
ulipaji wa madeni unaongezeka kwa kiwango kikubwa kuliko makadirio ya bajeti.
Mwaka wa fedha wa 2012/13 CFS ilitengewa shilingi bilioni 2735.9 lakini
matumizi halisi yalikuwa shilingi bilioni 3341.7 sawa na asilimia 22.1 zaidi ya
makadirio.
Malipo mengine ya CFS yalikadiriwa kuwa
shilingi bilioni 783.5 lakini serikali imetumia shiling bilioni 1028.5 ambalo
ni ongezeko la shilingi bilioni 245 sawa na asilimia 31.3 ya makadirio ya
bajeti. Sehemu kubwa ya matumizi mengine ya CFS ni malipo ya pensheni na
mchango wa serikali katika mfuko wa hifadhi ya jamii ya wafanyakazi wa serikali
ambayo makadirio ya bajeti yake yanapaswa kuwa ya uhakika. Ni vyema Mdhibitina
mkaguzi wa serikali afanye ukaguzi maalum (special audit) wa mfuko wa CFS.
Ulipaji wa mishahara ulikuwa mkubwa kuliko
makadirio ya bajeti kwa shilingi bilioni 120 sawa na asilimia 2.5.
Matumizi mengine – Other Charges – ndiyo
yaliyopunguzwa kwa kiasi kikubwa. Matumizi mengine ndiyo yanayogharamia
vitendea kazi vya siku hadi siku katika wizara na idara za serikali. Ikiwa
vitendea kazi hivyo havipo wafanyakazi wa serikali hawawezi kutimiza wajibu
wao. Bajeti ya matumizi mengine ilikadiriwa kuwa shilingi bilioni 4109.1 lakini
matumizi halisi yanatarajiwa kuwa shilingi bilioni 2682.1, upungufu wa shilingi
bilioni 1427.1 sawa na asilimia 34.7 ya bajeti.
Wizara na idara zisizokuwa na
nguvu za kisiasa zilitengewa fedha kidogo sana za Matumizi Mengine. Wafanyakazi
wa serikali wanaenda kazini lakini hakuna kazi wanayoifanya kwa kukosa vitendea
kazi, zahanati na hospitali hazina dawa, shule hazina vitabu na vifaa vingine
vya kufundishia. Wanachi hawapati huduma za serikali.
Serikali ilikadiria shilingi 5674.0 kama
bajeti ya maendeleo lakini fedha iliyotelewa ni shilingi bilioni 5011.6.
Upungufu wa shilingi bilioni 662.5 sawa na asilimia 11.7 ya makadirio ya
bajeti.
Bajeti ya Mandeleo inayoidhinishwa ni
tofauti na bajeti halisi inayotekelezwa. Serikali bado haijatoa takwimu za
bajeti halisi kwa kila wizara, idara na taasisi za serikali kwa 2013/14.
Takwimu zilizopo ni za mwaka 2012/13. Mwaka wa bajeti wa 2012/13 Wizara ya
Kilimo ilitengewa bajeti ya Maendeleo ya shilingi bilioni121.1 lakini fedha
iliyopewa ilikuwa shilingi bilioni 67.1 sawa na asilimia 55.4 ya makadirio ya bajeti.
Wizara ya elimu ilitengewa shilingi bilioni 92.6 kama bajeti ya maendeleo
lakini ikapewa shilingi bilioni 59.5 sawa na asilimia 64.3 ya bajeti
iliyoidhinishwa na Bunge.
Bajeti ya Maendeleo ya Wizara ya Maji
ilikuwa shilingi bilioni 465.8 lakini ikapewa shilingi bilioni 229.3 sawa na
asilimia 49.2. Wizara ya Afya ilitengewa shilingi bilioni 283.5 lakini ikapewa
shillingi bilioni 220.2 sawa na asilimia 77.7. Wizara ya ardhi na Makazi
ilitengewa shilingi bilioni 71 lakini ikapewa shilingi bilioni4 sawa na
asilimia 5.6
Katika hali hii bajeti siyo mwongozo wa
utekelezaji wa sera za serikali.
Bajeti ya 2014/15
Bajeti ya 2014/15 imekadiria kukusanya
mapato na kutumia shilingi bilioni 19853.3 ukilinganisha na bajeti ya 2013/14
ya shilingi 18249.0 Matumizi halisi ya mwaka 2013/14 yanatarajiwa kuwa shilingi
17096.8 Ongezeko halisi la bajeti ya 2014/15 ni asilimia 16.1.
Mapato ya ndani yanakadiriwa kuwa shilingi
bilioni 12178.0. Mwaka 2013/14 serikali ilikadiria kukusanya shilingi 11154.1
lakini inatarajia kukusanya shilingi 10098.7. Je serikali hii itaweza mwaka huu
kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa asilimia 20.6 ukilinganisha na
ukusanyaji wa mwaka jana?
Halmashauri zilikadiriwa kukusanya shilingi
bilioni 383.5 mwaka 2013/14. Hata hivyo matarajio ni kuwa zitakusanya shilingi
bilioni 268.4. Bajeti ya 2014/15 inakadiria Halmashauri zikusanye shilingi
bilioni 458.5, ongezeko la asilimia 70.8 la mapato halisi ya 2013/14
Misaada na mikopo ya miradi ilikadiriwa
kuchangia shilingi bilioni 1796.9 lakini zilizopatikana ni shilingi bilioni
922.3 tu. Hata hivyo serikali inakadiria kuwa mwaka 2014/15 misaada na mikopo
ya miradi itakawa shilingi bilioni 1745.3 ongezeko la asilimia 89.2 ya fedha
iliyopatikana mwaka 2013/14.
Kwa uchambuzi wa takwimu hizi bajeti ya
2014/15 haitekelezeki kama ilivyokuwa kwa bajeti ya 20143/14. Huduma za
serikali zilidorora sana kwa kukosa kupangiwa matumizi ya vitendea kazi
zitaendelea kudorora kwani matumizi mengine yanakadiriwa kutengewa shilingi
bilioni 2650.3 tu mwaka 2014/15 ukilinganisha na makadirio ya shilingi bilioni
4109.1 na matumizi halisi ya shilingi bilioni 2682.1.
Bajeti ya serikali bado haitoi kipaumbele
kwenye miradi ya maendeleo. Makadirio ya matumizi ya kawaida ni shilingi
bilioni 13408.2 ambayo ni makubwa kuliko makadirio ya mapato ya ndani ambayo ni
shilingi bilioni 12178.0. Kimsingi serikali haichangii bajeti ya maendeleo. Bajeti
inayojikita kuchochea maendeleo mapato ya ndani yanakuwa makubwa kuliko
matumizi ya kawaida na ziada inahamishiwa kwenye bajeti ya maendeleo. Bajeti ya
maendeleo ya Tanzania inategemea misaada toka nje na mikopo ya ndani na nje.
Bajeti Mbadala ijikite katika ukusanyaji wa
mapato makini na matumizi mazuri ya fedha za umma. Kwa kuondoa misamaha holela
ya kodi tunaweza kukusanya asilimia 22-25 ya pato la taifa kama mapato ya
serikali. Matumizi ya serikali yagawiwe kisekta kama ifuatavyo asilimia 25 elimu,
asilimia 10 kilimo, asilimia 15 afya, asilimia 25 miundombinu, asilimia 25
ulinzi, usalama, utawala na mengine.
Watanzania tunahitaji
tutafakari hali halisi tuliyonayo na tubuni sera na mikakati ya pamoja ya
kujikwamua toka dimbwi la umaskini. Misingi muhimu ya sera na mikakati hiyo
iwe:-
· Kuitumia
vizuri mali ya asili ya Tanzania kwa manufaa ya wananchi wote huku tukilinda
mazingira yetu
· Kuwekeza
kwenye afya ya watoto wa Tanzania toka wakiwa katika mimba za mama zao kwa
kuhakikisha kina mama waja wazito na watoto wachanga wanapata lishe bora
· Kuwekeza
katika elimu ya watoto wa Tanzania toka shule za chekechea na kuendelea. Kuweka
msisitizo maalum katika elimu ya hesabu, sayansi na teknolojia
· Kuwekeza
katika kilimo hasa cha chakula kama vile mahindi, mpunga, maharage, jamii ya
kunde na mbegu za mafuta kukidhi mahitaji ya ndani na kuuza masoko ya nje hasa
nchi za jirani na hususan Congo
· Kuwekeza
katika miundombinu ya barabara, umeme, maji na mawasiliano
Kuweka mkakati madhubuti wa kuanzisha na
kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi ya ndani na kuajiri watu wengi kama
vile viwanda vya nguo na mavazi, viatu na bidhaa za ngozi, vifaa vya matumizi
ya nyumbani na vifaa vya umeme na electroniki.
Serikali ya CCM haina utashi wa kisiasa ya
kuandaa bajeti inayotekelezeka yenye maslahi ya mwananchi wa kawaida. Katika
kipindi hiki kuelekea 2015 tuna wajibu wa kuandaa na kukamilisha mpango na
bajeti inayotekelezeka itakayojenga misingi ya maendeleo ya kweli kwa wananchi
wote.
Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti wa CUF (Taifa)
15 JUNI, 2014
No comments:
Post a Comment