Ofisa
Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Azam Media Rhys Torrington (kulia) akimkabidhi Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania
Silas Mwakibinga nakala ya uthibitisho wa malipo ya fedha kwa ajili ya Ligi Kuu
ya Vodacom.
|
KAMPUNI ya Azam Media imetangaza kuwa tayari imeshatuma fedha kwa Bodi ya Ligi kwa ajili ya msimu wa ligi wa Vodacom kwa mwaka 2014/ 2015.
Fedha hizo zimetolewa mapema zaidi kwa ajili ya kusaidia maandalizi mapema kwa timu kama ilivyokubaliwa kwenye mkataba wa miaka mitatu ya udhamini wao katika ligi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Azam zilizopo Tazara, Dar es salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Rhys Torrington, alisema kuwa kampuni hiyo inavutiwa na aina nzuri ya ushirikiano kati yake na bodi ya Ligi.
Alisema kuwa kupitia bodi hiyo Azam imepiga hatua kubwa katika kufanikisha adhma yake ya kuifanya Ligi hiyo ya Vodacom kuwa ya kuvutia zaidi.
“Ligi hii tunataka kuifanya kuwa ni moja kati ya ligi zinazovutia na kuonesha ushindani barani Afrika, ingawaje ninajua kuwa kuna mengi ambayo yanatakiwa kuendelea kufanywa ili kuipa nguvu zaidi ligi hii”alisema Torrington.
Alisema kuwa kwa kutambua hilo ndio maana Azam Media imehakikisha kuwa klabu zote zinapata fedha mapema ili kusaidia suala zima la maandalizi.
Wakizungumza na wanahabari |
Akizungumzia mikakati ya baadae ya Azam Media alisema kuwa inatarajia kuanza kuonesha soka la mitaani (street soccer) mbalimbali moja kwa moja (live) itakayokuwa ikiendelea kwenye nchi za Kenya na Uganda.
Alisema kuwa kwa sasa Azam Media imeanza kujikita katika nchi za Kenya, Uganda na Malawi ambapo itakuwa ikiuza ving’amuzi vyake katika nchi hizo.
Aliongeza kuwa pia katika kuhakikisha kuwa inatoa mwanya zaidi wa vipindi vizuri na vya kuvutia inaendelea na vipindi vya michezo vya Morning Trumpet, sport@8 pamoja na Kwetu House.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya ligi, Mr Silas Mwakibinga alisema kuwa kwa hatua hiyo ya Azam ya kuhakikisha upatikanaji wa fedha hizo kwa wakati ni nzuri na itasaidia kuzipatia timu muda mzuri wa kujiandaa.
Alisema kuwa bodi yake inavutiwa sio tu na utangazaji wa vipindi unaofanywa na Azam bali pia hata nia yao ya kuendeleza soka la Tanzania.
Azam Media ilisaini mkataba wa miaka mitatu na wenye thamani ya TSHS 5,560,800,000 kuonesha mechi za live na za kurekodi mechi za Ligi Kuu na fedha hizo zinalipwa kwa awamu tatu.
No comments:
Post a Comment