Tuesday, June 17, 2014

ONYO KUHUSU UTAPELI WA AJIRA KATIKA KAMPUNI YA TIGO TANZANIA



Tumepata taarifa kwamba kuna baadhi ya watu wasiowaaminifu wanaojifanya wafanyakazi wa kampuni ya Tigo na kutumia mwanya huo kuwadanganya wananchi kujaza fomu feki kama njia ya kupata ajira katika kampuni yetu. Inadaiwa kwamba kila fomu inatozwa kiasi cha TZS 20,000 (Shilingi elfu ishirini). 

Tigo inapenda kuwataarifu wale wote wanaotafuta ajira katika kampuni yetu na umma kwa ujumla kwamba hakuna fomu za aina hii zinazotolewa kutoka mawakala, matawi au idara yoyote ya kampuni yetu. Tunapenda kuwatahadharisha wananchi wote kwamba msidanganyike na watu hawa ambao wamekuwa wakizunguka sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam wakifanya utapeli  huu.  

Ifahamike kwamba nafasi yoyote ya ajira katika Tigo hutangazwa kupitia magazeti ya kila siku na pia kuwekwa katika tovuti yetu ya www.tigo.co.tz pamoja na ile ya www.millicom.com

Tunapenda ifahamike kwamba Tigo, matawi yake au idara zake hazitawajibika kwa namna yoyote ile kutokana na vitendo hivi vya kitapeli. 


Imetolewa kwa manufaa ya umma.

No comments: