Wednesday, August 27, 2014

WAZIRI MKUU PINDA AZIDI KUANDAMWA,JUKATA NAO WAMVAA



Na Karoli Vinsent

       SIKU chache  kupita baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutangaza nia ya kumrithi  Rais Jakaya Kikwete kwenye uchaguzi mkuu mwakani Ndani ya Chama cha Mapinduzi CCM na kupeleka kuwapa kiwewe wasaka Urais wenzanke ndani ya chama hicho,
        
       Nao Jukwaa la Katiba nchini limeibuka na kusema Kitendo alichokifanya Waziri huyo mkuu kimezorotesha utendaji serikalini kutokana na kauli hiyo kuchochea uhasama kwa watumishi wa Umma.
         
       Kauli hiyo Imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mwenyekiti wa jukwaa la Katiba nchini Hebron Mwakagenda wakati wa mkutano na waandishi wa Habari,ambapo alisema Waziri mkuu huyo alikosea kuzungumza nia yake mapema huku akijua bado ni msimamizi wa Shughuli za serikali.
          

          “Waziri mkuu amefanya makosa makubwa sana kutangaza nia mapema hivyo,amesahau kabisa kwamba bado yeye ni msimamizi wa shughuli za Serikali,na sisi Jukwaa tumeshuhudia Jinsi mambo yanavyokwenda hovyo Serikalini kutokana na yeye kutangaza nia mapema na kupelekea ofisi za serikali watu kuacha kufanya kazi na kuendesha malumbano yasio kuwa na lazima kuhusu wasaka Urais”alisema Mwakagenda.
           
          Mwakagenda alizidi kusema Taifa litegemee kusinyaa kwa utendaji serikalini kutokana Nia hiyo aliyotangaza Waziri mkuu kwani sasa wakuu wa Wilaya na Mikoa wameanza kujigawa kimakundi na kila mtu kuanza kipigia chapuo upande wake anaoutaka na kuleta misuguano ndani ya Serikali.
       
           Kauli ya Jukwaa la Katiba imekuja siku chache baada Waziri Mkuu Mizengo panda,kuitaka nafasi hiyo ya Juu ya uongozi nchini,Nia hiyo aliitoa Wiki iliyopita  Ikulu ndogo ya Mwanza jijini Mwanza, mara baada ya kuwaalika wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) toka mikoa sita ya Kanda ya Ziwa.
       
          Habari kutoka vyanzo vyetu vya kuaminika zilieleza kuwa Waziri mkuu aliwaalika wajumbe tisa kutoka katika wilaya zote za mikoa ya Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na Kagera.
       
           Pinda aliyekuwapo jijini Mwanza kwa ajili ya kuendesha harambee ya Mfuko wa Taasisi ya Benjamin Mkapa iliyofanyika wiki iliyopita, alikutana kwa ‘mafungu’ na wajumbe zaidi ya 50 kutoka Mara, baadhi toka Mwanza, Geita na Kagera.
      
        “Wajumbe wengine wa Shinyanga, Simiyu na wale Mwanza na Geita alikutana nao Jumamosi jioni ili kuwashawishi wamuunge mkono  baada ya jina lake kupitishwa na NEC,” kilisema chanzo chetu.

     Chanzo hicho kilisema wajumbe toka wilaya hizo za Kanda ya Ziwa, walianza kuwasili Ijumaa mchana jijini Mwanza kwa lengo la kuitikia wito wa Waziri Mkuu kabla ya hawajatangaziwa nia yake.

SABABU ZA KUTANGAZA NIA
     

            Waziri Pinda aliwaeleza wajumbe hao sababu kubwa zilizomfanya aguswe kutangaza kuwania nafasi ya Rais 2015, ni kutokana na ushawishi mkubwa toka kwa maaskofu, masheikh, baadhi ya wabunge, watu maarufu pamoja na mke wake.

     “Sikuwa na nia hiyo kwa vipindi vyote vitatu vya ubunge wangu, lakini watu hao akiwamo mke wangu, nimeshawishika kutaka nafasi hiyo,” alisema Pinda.

          Alisema ameona hana sababu ya ‘kuzembea’ kutangaza nia ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu ujao.
SIFA
 

         “Ninazo sifa za kunitosheleza kuwania nafasi hii, ikiwamo kutokuwa fisadi, pia nimekuwa ndani ya viongozi wa nchi wa awamu zote nne tangu 1974 enzi za Nyerere (Julius), Ali Hassan Mwinyi, Mkapa (Benjamin) na sasa Kikwete,” alidai.
     
          Aidha, alisema kutokana sifa hizo hataweza kuchangishiwa pesa za kuingia madarakani kama wengine (hakuwataja), bali atawapa kiasi alichonacho ili kuwawezesha kumsaidia.
      
          Pinda maarufu kama “mtoto wa mkulima”, alidai anaamini viongozi wakuu waliopita madarakani na kuongoza nchi, wanamuunga mkono.
        
         Kutangaza huko kwa Waziri mkuu Pinda kumeibua presha kwa Wasaka wengine Urais ndani ya Chama hicho ambao wamejiapiza kutumia kila njia kushika nafasi ya upangaji wa Ikulu ya Tanzania.
       
          Makada hao ambao wamesema watafanya kufa na kupona kushika nafasi ya urasi  ni Waziri mkuu aliyejiuzulu,Edward Lowassa,Waziri wa ushirikiano na Uhusiano wa Afrika Mashariki,Samwel sitta,Naibu waziri mawasiliano,Sayansi na Teknolojia,January Makamba,Waziri Mkuu mstaafu wa awamu ya tatu,Fredrick sumaye, Waziri wa Maliasili na Utalii ,Lazaro Nyalandu,Naibu Waziri wa Fedha Mwiguru Nchemba,Waziri wa Sheria Dk Rose Migilo pamoja Waziri wa mambo ya Nje,Berdard Membe.

      Naye Msomi na mchambuzi wa masuala ya Kisiasa nchini kutoka chuo Kikuu cha Dodoma,Seiph Yahaya.alisema kitendo cha Waziri mkuu mizengo pinda kujitosa katika nafasi hiyo ya kuwania urais,ni ishara tosha chama cha Mapinduzi CCM,kinaweza kugawanyika.
         
        “Sikiliza mwandishi,tunajua kabisa Rais Jakaya Kikwete anamuandaa Mizengo pinda ashike nafasi hiyo ya Urais,na mimi nakwambia kama Rais  leo tupangiwe na Rais Jakaya Kikwete,basi chama hiki akifiki mbali lazima kigawanyike tu utashuhudia tu mwakani”alisema Yahaya   

No comments: