Wednesday, January 28, 2015

MICHEZO24--HIVI NDIVYO SIMBA ALIVYONYONYOLEWA TAIFA JIONI HII

CHOLLO AKOSA PENALTI DAKIKA YA MWISHO, SIMBA SC YALALA 2-1 KWA MBEYA CITY

BEKI Nassor Masoud ‘Chollo’ amekosa penalti dakika ya mwisho, Simba SC ikilala 2-1 mbele ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Chollo alipiga penalti hiyo ikagonga mwamba wa juu dakika ya 90+3 baada ya beki Yussuf Abdallah kumchezea rafu kiungo Jonas Mkude kwenye boksi.

Chollo alifanya kosa hilo, Simba SC ikitoka kufungwa bao la pili kwa penalti pia na Yussuf Abdallah baada ya kipa Peter Manyika kumshika miguu Raphael Daudi dakika ya pili 90+2.  

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Abdallah Kambua wa Shinyanga aliyesaidiwa na Anold Bugado wa Singida na Yahya Ali wa Mara, hadi mapumziko tayari Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.

Hamad Kibopile wa Mbeya City kushoto akishangilia baada ya kufunga bao la kusawazisha

Mfungaji wa bao la Simba SC, Ibrahim Hajibu (kushoto) akitafuta maarifa ya kumtoka beki wa Mbeya City, Juma Nyosso

Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji chipukizi, Ibrahim Salum Hajib dakika ya 45+2 kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 20, baada ya kiungo Awadh Juma kuchezewa rafu.

Mbeya City ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Hamad Kibopile dakika ya 77 akitumia vizuri makosa ya mabeki wa Simba SC kuchanganyana na kipa wao, Peter Manyika.

Simba SC walicheza vizuri kipindi cha kwanza na hata hata kipindi cha pili walikianza vizuri, lakini baadaye wakawapa nafasi ya Mbeya City kuuteka mchezo.

Hiki ni kipigo cha kwanza kwa Simba SC katika Ligi Kuu chini ya kocha mpya, Mserbia Goran Kopunovic aliyeshinda mechi moja 2-0 dhidi ya Ndanda na baadaye sare ya 1-1 Azam FC.    

Matokeo hayo, yanaiacha Simba SC na pointi zake 13 za mechi 11, wakati Mbeya City inafikisha pointi 15 za mechi 11.

Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Peter Manyika, Nassor Masoud ‘Chollo’, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murushid, Jonas Mkude, Simon Sserunkuma/Ibrahim Twaha ‘Messi’ dk62, Awadh Juma, Dan Sserunkuma/Elias Maguri dk46, Ibrahim Hajib/Abdi Banda dk74 na Ramadhani Singano ‘Messi’.

Mbeya City; David Burhan, Richard Peter, Hamad Kibopile, Juma Nyosso, Yussuf Abdallah, Steven Mazanda, Themi Felix/Hamidu Mohammed dk70, Raphael Alpha, Paul Nonga, Cossmas Freddy/Peter Mapunda dk67 na Deus Kaseke/Idrisa Rashid dk78

 STORY KWA MSAADA WA BIN ZUBEIRY BLOG

No comments: