Thursday, January 29, 2015

MICHEZO24--TFF YAHADHARISHA MGOGORO WA ZFA KORTINI


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)l imepokea kwa masikitiko taarifa za kuwepo tena kortini kwa kesi dhidi ya uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), jambo ambalo linaweza kuathiri ushiriki wa timu za Zanzibar kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, na Kombe la Shirikisho.

Mwishoni mwa mwaka jana, TFF ilihadharisha juu ya masuala ya mpira wa miguu kupelekwa mahakamani, kwani kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kitendo hicho ni kinyume cha taratibu za uendeshaji mpira wa miguu ambazo zinakataza masuala ya mchezo huo kupelekwa katika mahakama za kawaida.

Kutokana na hali hiyo, TFF iliiandikia barua ZFA kutaka mgogoro huo uondolewe kortini na yenyewe kuridhia kuwa tayari kupeleka ujumbe Zanzibar ili ukutane na pande zinazohusika.

Pia TFF ilisema timu za Tanzania Bara zisingeruhusiwa kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2015 iwapo kesi hiyo ingeendelea kuwepo kortini na kutaka iondolewe bila masharti yoyote.

ZFA iliithibitishia TFF kuwa kesi hiyo imeondolewa kortini bila masharti, hivyo timu za Tanzania Bara kuruhusiwa kushiriki katika michuano ya Kombe la Mapinduzi. Ni muhimu suala hilo likashughulikiwa haraka ili kutohatarisha ushiriki wa timu za KMKM na Polisi kwenye michuano hiyo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

 WAANGALIZI WA SIRI KUSIMAMIA MECHI ZA MWISHO FDL
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litatuma waangalizi wa siri kwenye mechi za raundi ya 21 na 22 ambazo ni za mwisho kwa makundi yote ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zitakazoanza kuchezwa  Februari 10 mwaka huu.

Mwangalizi huyo (match assessor) atatumwa na Katibu Mkuu ambapo baada ya mechi atatuma ripoti kwake kwa hatua zaidi.

Mechi za raundi ya 21 kundi A zitachezwa Februari 10 mwaka huu kati ya KMC na African Lyon (Uwanja wa Mkwakwani), Kurugenzi FC na African Sports (Uwanja wa Mufindi), Majimaji na JKT Mlale (Uwanja wa Majimaji), Kimondo FC na Friends Rangers (CCM Vwawa, Mbozi), Ashanti United na Villa Squad (Uwanja wa Karume) na Polisi Dar na Lipuli FC (Uwanja wa Azam Complex).

Raundi ya 22 itachezwa Februari 16 mwaka huu kwa kuzikutanisha African Lyon na Polisi Dar (Uwanja wa Karume), Kurugenzi na Lipuli FC (Uwanja wa Mufindi), Kimondo FC na Majimaji (CCM Vwawa, Mbozi), JKT Mlale na Ashanti United (Uwanja wa Majimaji), Friends Rangers na African Sports (Uwanja wa Taifa), na Villa Squad na KMC (Uwanja wa Azam Complex).

Kundi B raundi ya 21 ni Februari 17 mwaka huu kati ya Burkina Faso na JKT Kanembwa (Uwanja wa Jamhuri), Mwadui na Polisi Tabora (Uwanja wa Mwadui), Polisi Dodoma na Green Warriors (Uwanja wa Jamhuri), Rhino Rangers na JKT Oljoro (Ali Hassan Mwinyi), Panone na Polisi Mara (Uwanja wa Ushirika), Geita Gold na Toto Africans FC (Geita).

Februari 22 mwaka huu ni JKT Kanembwa na Green Warriors (Lake Tanganyika), Mwadui na Burkina Faso (Mwadui), Polisi Tabora na JKT Oljoro (Ali Hassan Mwinyi), Polisi Dodoma na Panone (Uwanja wa Jamhuri), Toto Africans na Rhino Rangers (CCM Kirumba) na Geita Gold na Polisi Mara (Geita).

Mechi za viporo za Polisi Mara zitachezwa Februri Mosi dhidi ya JKT Kanembwa, na Februari 5 mwaka huu dhidi ya Polisi Tabora. Mechi zote zitachezwa kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma.

FIFA YACHUNGUZA TUHUMA ZA UPANGAJI MATOKEO
Ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) upo nchini kuchunguza tuhuma za upangaji matokeo.

Waamuzi waliosimamishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na watu wengine watahojiwa na ujumbe huo. Matokeo ya uchunguzi huo yatatangazwa na FIFA baada ya shughuli hiyo kukamilika.

Tunaendelea kuwahimiza wanafamilia wa mpira wa miguu wazidi kuzingatia kanuni za maadili za TFF, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na FIFA katika utendaji wao. FIFA itahakikisha kuwa haki inatendeka katika uchunguzi ambao inaufanya.



IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)


No comments: