Ujumbe
wa wiki ya maji kitaifa ni “maji kwa maendeleo endelevu” na maadhimisho
yanafanyika Musoma ambao Rais anatajiwa kuhutubia. Kwa kuwa maadhimisho haya ni
ya mwisho kwa utawala wake, anapaswa kulieleza taifa ni kwa nini ameonyesha
udhaifu wa kushindwa kutekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati akizindua Bunge
mwaka 2005 ya kwamba anatambua kuwa maji ni kero ‘nambari wani’ na kwamba
Serikali yake ingeandaa mpango kabambe wa kuhakikisha matatizo ya maji yanakuwa
historia.
Ameonyesha
udhaifu 2005-2010 na ameendeleza udhaifu huo mwaka 2010-2015 hivyo aelekeze
Waziri Mkuu atekeleze ahadi iliyotolewa na Waziri Mwandosya kwa niaba yake ya
Serikali kuwasilisha katika kila Mkutano wa Bunge Taarifa ya Mpango wa dharura
kwa kuwasilisha katika Mkutano huu wa 19 wa Bunge taarifa hiyo.
Aidha,
nabashiri kwamba Rais atatumia maadhimisho ya Musoma kwenye uzinduzi wa miradi
kueleza ‘mafanikio’ makubwa yaliyopatikana kutokana na Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (MMS)- Big Results Now BRN.
Hata
hivyo, Rais azingatie kwamba MMS/BRN kwenye Sekta ya Maji haijaweza
kushughulikia kwa ukamilifu matatizo niliyoyaeleza kwenye hoja binafsi
niliyowasilisha Bungeni kuhusu Hatua za Haraka za Kuboresha Upatikanaji wa Maji
Safi na Ushughulikiaji wa Maji Taka Jijini na Nchini (Rejea: http://mnyika.blogspot.com/2013/02/maelezo-na-hoja-binafsi-ya-kupendekeza.html
). Ilani ya CCM ya mwaka 2005 iliahidi ifikapo 2010 maji yangepatikana mijini
ikiwemo Jijini Dar Es Salaam kwa asilimia 90 na vijijini kwa asilimia 75 ahadi
ambayo haijatekelezwa.
Ili
Rais asiendelee kuonekana dhaifu zaidi walau kupitia siku hii ya maji awaagize
watendaji katika ofisi yake watekeleze agizo alilowapa la kuitisha kikao cha
kazi Ikulu kuhusu matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam mwezi Machi
2013 kama alivyoahidi ( rejea: http://gkitalima.blogspot.com/2013/03/jakaya-kikwete-kukutana-na-mnyika.html
na http://www.matukiotz.co.tz/2013/03/mnyika-aitwa-ikulu.html
).
Namshukuru
Rais kwamba kuna hatua katika upatikanaji wa fedha na utekelezaji wa miradi ya
Ruvu Chini na Ruvu Juu na pia miradi mingine ya visima vya dharura ikiwemo
katika Jimbo la Ubungo ikiwemo mradi wa Mpiji Magohe ambao tumeuzindua siku
chache zilizopita kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya maji; hata hivyo kasi,
nguvu na ari ya mpaka sasa hailingani na ahadi za kufanya tatizo la maji kuwa
historia 2010, 2011, 2012, 2013, 2014 na hata 2015.
Zipo
hatua zaidi zinaweza kuchukuliwa katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa
iwapo tukikutana na kujadili udhaifu
uliopo katika utekelezaji wa Mpango Maalum wa maji Dar es Salaam; hivyo kwa
kuwa nimeshamkumbusha yeye mwenyewe na wasaidizi wake mara kadhaa bila kikao
hicho kuitishwa ni wakati sasa wa wananchi wa Dar Es Salaam kushiriki
kumkumbusha kwa njia mtakazoona zinafaa.
Kwa
kuzingatia hali hii kwa wote wenye kutaka kushiriki ujumbe wetu kwake na kwa
wengine kitaifa unapaswa kuwa #Maji Na Mabadiliko Kwa Maendeleo ( #MaMaMa ) ili
tuitumie siku hii na zijazo kuhamasisha mabadiliko yenye kuwezesha kupatikana
kwa maji kwa maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla. ( #WaterIs #MaMaMa ).
Wenu
katika uwakilishi wa wananchi,
John
Mnyika (Mb)
Jimbo
la Ubungo
22
Machi 2015
No comments:
Post a Comment