|
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kimetaja ngome saba za Mawaziri wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), zilizosambaratishwa na kuchukuliwa na Chadema katika Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa.
Ngome hizo ni pamoja na Jimbo la
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Jimbo la Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Jimbo la
Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, Jimbo la Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, Jimbo la Waziri wa Chakula, Kilimo na
Ushirika, Stephen Wassira.
Mengine ni Jimbo la Waziri wa Kazi
na Ajira, Gaudensia Kabaka pamoja na Jimbo analotoka Naibu Waziri wa Sayansi,
Teknolojia na Mawasiliano, Januari Makamba na mengine mengi, na kwamba Mawaziri
hao hawana sifa wala uwezo tena wa kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Hayo yalibainishwa juzi na Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalim, alipokuwa akihutubia mkutano
wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Sengerema mjini hapa
mkoani Mwanza.
Katika mkutano huo, Salum
aliyeongozana na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la chama hicho Taifa, Patrobas
Katambi, alieleza kuwa Chadema na washirika wake wa vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (UKAWA), imezima ndoto za vigogo hao wa CCM kugombea urais
2015.
“Naomba leo niwatobolee siri hii.
Ndani ya CCM mtu aliyekuwa wa kwanza kuwa na kiherehere cha kutaka kugombea
urais alikuwa ni Dk. Harrison Mwakyembe, huyu mtu na Mawaziri wenzake niliowatajia
mitaa yao wanayoishi ilichukuliwa na Chadema katika Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa.
“Yaani ni hivi, wakitaka kugombea
urais lazima wathibitishe uraia wao kwa barua itakayoandikwa na Mwenyekiti wa
Chadema katika maeneo yao wanayoishi. Kwa maana hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba mwaka huu njia ya Chadema na UKAWA kwenda Ikulu ni nyeupeee,” alisema
Mwalim na kushangiliwa.
Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo wa
Chadema (Zanzibar), aliwaambia wananchi kwamba UKAWA imejipanga vema kuchukuwa
dola Oktoba mwaka huu, na Serikali yake itazingatia nyayo na misingi iliyoachwa
na Mwalimu Julius kambarage Nyerere.
Mwalim aliitaja misingi hiyo kuwa ni
uzalendo, uadilifu, uaminifu, utu na haki za binadamu, na kusema kwamba:
“Utawala wa Nyerere ulikuwa imara kiuchumi kutokana na kuwepo kwa viwanda vingi
nchini ambavyo kwa sasa vimeuzwa na kubinafsishwa na Serikali ya CCM,”.
Aliwaomba Watanzania kutokwenda
kuipigia kura Katiba Mpya Inayopendekezwa kwa madai kwamba CCM na Serikali yake
imetupa maoni ya wananchi yaliyokuwa kwenye Rasimu ya Jaji Joseph Warioba,
hivyo ni vema CCM ikaangushwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Pamoja na mambo mengine, Mwalim
aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha kwenye daftari la
wapiga kura ili wawe na shahada za kupigia kura Oktoba 2015 zitakazowawezesha
kuiingiza madarakani Serikali ya UKAWA itakayokuwa na neema kwa Watanzania
wote.
No comments:
Post a Comment