Wednesday, April 15, 2015

KOVA AWATIA MIKONONI WATUHUMIWA 901,WAMO VIBAKA WAZOEFU DAR ES SALAAM--SOMA HII


 

WATUHUMIWA 901 WAKAMATWA IKIWA NI PAMOJA NA VIBAKA. OPARESHENI KALI YA POLISI INAENDELEA WANANCHI WASIWE NA HOFU JIJI LA DAR ES SALAAM NI SHWARI

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Slaam limekuwa likifanya oparesheni za mara kwa mara katika jiji la Dar es Salaam ili kukabiliana na uhalifu ambao kwa sasa umekuwa changamoto kubwa. Oparesheni na juhudi hizo kubwa zinalenga kuwafanya wananchi na wageni wa jiji hili maarufu waweze kuishi na kufanya shughuli zao katika hali ya usalama.

Oparesheni hii inajumuisha makosa mbalimbali ya kihalifu yakiwemo ujambazi wa kutumia silaha, unyang’anyi wa kutumia nguvu, kuvunja nyumba usiku na kuiba, kuishi nchini bila kibali, kuharibu miundombinu, uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya, kubughudhi abiria, kucheza kamari, uuzaji na unywaji wa pombe haramu ya moshi (Gongo),  wahalifu sugu, makosa ya ukahaba (kujiuza), makosa ya usalama barabarani, pamoja na uhalifu mwingine.

Katika juhudi/oparesheni  hizo Jeshi la Polisi Kanda maalum limepata mafanikio makubwa kwa kipindi cha kuanzia tarehe 01/03/2015 hadi sasa kama ifuatavyo:

1.      Wamekamatwa jumla ya watuhumiwa 901 kwa makosa mbalimbali kama ilivyoainishwa hapo juu.

2.      Zimekamatwa silaha nne; moja ni BASTOLA 1 Revolver yenye namba TZCAR 96093 ikiwa na risasi 11 ndani ya magazine, nyingine ni bunduki Shotgun moja ikiwa na risasi tatu. Silaha ya tatu ni bastola NORINCO yenye namba TZCAR101653 ikiwa na risasi moja na ya nne ni Bastola  Browning yenye namba A558651 ikiwa na risasi 10.
Zilipatikana risasi kadhaa huko maeneo ya Kitunda zikiwa ndani ya kopo zikiwa zimefukiwa ardhini.

Pia zilikamatwa noti bandia za dolla za kimarekani zipatazo (USD 17750) na watuhumiwa watatu.

3.      Zimekamatwa jumla ya lita 1022 za pombe haramu ya moshi (Gongo).

4.      Zimekamatwa jumla ya Kilo 47 za bhangi, Puri 131, Misokoto 1748, na Kete 2210 za Bhangi pamoja na Bunda 20 za Mirungi.

5.      Kwa makosa ya usalama barabarani yaliyokamatwa kwa kipindi hichi ni ya 34641.
Jumla ya tozo kwa makosa hayo ni TSHS: 1,039,242,000/= (Shilingi Billioni Moja Millioni Thelathini na Tisa Mia Mbili Arobaini na Mbili elfu tu).
Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa kipindi cha mwezi Machi oparesheni hizi ni endelevu ili kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam wanaishi kwa amani na utulivu pamoja na kufanya shughuli zao katika mazingira salama.
Aidha, kazi hii ni ngumu na yenye changamoto mbalimbali hivyo nawaomba wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam waendelee kulisaidia Jeshi la Polisi ili kazi hii iwe na tija zaidi kwani inafanyika kwa maslahi na ustawi wa wananchi wote waishio katika jiji hili na mikoa ya jirani.


S.H. KOVA

KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM

No comments: