Saturday, April 18, 2015

SOMA ALICHOKISEMA MTATIRO KUHUSU KUJIUNGA ACT-WAZALENDO


Mwandishi wa gazeti la jamhuri amenipigia anasema ati gazeti lao lina taarifa kuwa mimi nina mpango wa kuhamia chama cha ACT, nikasikitishwa sana na taarifa alizonipa. Nadhani sasa mwaka wa uchaguzi umefika na magazeti yanalazimisha kutaka kuuza stori hata kama hazipo.

Nimemuonya mwandishi huyu asinichukulie poa sana, mimi siyo mtu mwepesi kiasi cha kuhangaika na vyama vipya kila kukicha. Wakati najiunga CUF kulikuwepo na CHADEMA na CCM na vyama vingine vyenye nguvu kuliko CUF, lakini nilijiunga CUF.

Nimekuwa mwanachama wa CUF na kisha kiongozi wa CUF katika nyadhifa za Ukurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria kwa miaka miwili kisha nimekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara kwa miaka mitatu.

Nimepumzika uongozi ndani ya chamachangu mwaka jana mwezi Juni tulipokwenda kwenye uchaguzi wa ndani ya chama. Sikugombea nafasi yoyote ile kuanzia tawi, kata, wilaya na hata taifa na tayari nilikwishawaaga viongozi wakuu kwamba nahitaji kuwekeza muda wangu katika kumalizia shahada yangu ya Sheria.(Naikamilisha mwezi Juni mwaka huu).

Tangu mwaka jana mwezi Juni nimekuwa nikiwekeza nguvu katika shule yangu, katika tafiti mbalimbali na katika jimbo la Segerea. Na najipanga hasa kuhakikisha kuwa malengo ambayo nimejipangia yanatimia. Nakipenda chama changu na mimi ni mwanachama thabiti kabisa.

Na nataka niwahakikishie kuwa ikiwa UKAWA haitaniruhusu kugombea ubunge katika jimbo langu na ikampa fursa hiyo mwanachama mwingine kutoka CUF au CHADEMA au NCCR au NLD, mimi nitaomba kuwa meneja kampeni wake.

Kuna watu wanadhani kuwa siasa ni mambo ya majaribio na kugawana vyeo. Siasa ni mapambano ya muda mrefu sana, yanahitaji uvumilivu, utulivu, subira, busara na weledi katika kila jambo.

Hao ACT mimi nawatakia kila la heri katika safari yao, siwachukii kwa sababu ni chama cha siasa kama vyama vingine, ni watanzania kama mimi lakini ndiyo maana wao ni ACT na mie ni CUF. Tena wengine ni walimu wangu, kina Prof. Kitila, na wengine ni rafiki zangu kama kina Zitto n.k.

Pamoja na yote haya, sitaacha kusimama mahali na kuijadili CCM, CUF, CHADEMA, NCCR, ACT n.k Mijadala ya namna hiyo itaendelea hapa jukwaani na kwingineko na sitaogopa kuiendesha ati kwa sababu ntahusishwa na chama fulani.

Kama kijana nina uhuru wangu wa kujadili jambo nalolitaka ilimradi sijavunja sheria za nchi na nawaomba vijana wengine waendeleze mijadala juu ya chama chochote kile na muda wowote ule bila kufungwa na vifungo vya vyama walivyomo. Mijadala ni jambo moja na itikadi ya mtu ni jambo lingine.

Nataka mhariri wa gazeti hilo la Jamhuri atambue kuwa sitatetereshwa wala kuyumbishwa na UPEPO, dawa ya upepo ni kuwa wakati unapita wewe INAMA.

No comments: