LEO NIMEKUWEKEA MAKALA HII ALIYOIANDIKA ZZK KATIKA
GAZETI TANZANIA DAIMA DESEMBA 30, 2012 MAKALA AMBAYO ALIIPA JINA LA FUATA MISINGI USIFWATE WATU
'Fuata Misingi sio watu'
MEI mwaka 2003 tukiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
tulitembelewa na mgeni kutoka Chama cha SWAPO cha Namibia. Wakati huo nchini
Namibia (na Afrika kwa ujumla) kulikuwa kuna mjadala kuhusu kubadili katiba ya
nchi hiyo ili kumruhusu Rais Sam Nujoma kugombea kipindi cha tatu.
Mgeni huyu alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa
SWAPO na alialikwa na vijana wa CCM pale Mlimani, kina Wilman Kapenjama na
Martin Shigella. Walimleta kwenye moja ya kumbi za semina ili kufanya mjadala
kuhusu Afrika. Nilimuuliza swali kwamba msimamo wake nini kuhusu mabadiliko ya
Katiba ya Namibia ili kumwezesha Nujoma kugombea kipindi cha tatu cha urais.
Akanijibu kwamba wao vijana wa SWAPO wanaunga mkono
lolote ambalo Sam Nujoma atataka! Mmoja wa washirika wa mkutano ule Kitila
Mkumbo, alisimama na kumwambia kijana yule ‘hupaswi kufuata mtu, fuata
misingi’. Alitoa kauli hii kwa ukali kidogo. Nadhani ndiyo maana bado ni kauli
ambayo imenikaa mpaka hivi sasa.
Hivi sasa hapa nchini kumezuka wimbi la wanasiasa kuwa na
makambi ambayo yanatokana na ufuasi kwa mtu au kiongozi wa kambi husika badala
ya ufuasi kwa misingi ya chama cha siasa au basi angalau misingi ya kambi
husika ya chama hicho. Makambi ni utamaduni ambao umeshamiri zaidi ndani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ingawa hata vyama vya upinzani sasa vimeingia kwenye
mtego huo hatari sana kwa demokrasia.
Huu ni mfululizo wa makala sita, zitakazokuwa zinaelezea
misingi mbalimbali ya chama ambacho mimi ni mwanachama, CHADEMA, na namna
ambavyo viongozi mbalimbali wa chama hicho wamekuwa wakisimamia kwa vitendo
misingi hiyo. Makala hizi zitakuwa zinatoka kila wiki ya mwisho ya mwezi katika
kipindi cha nusu ya kwanza cha mwaka 2013. Chama cha siasa ni jumuiko la watu
wenye nia moja na lengo moja la kisiasa.
Ni mchanganyiko wa watu wenye kuunganishwa na misingi
fulani. Misingi hii inapokosekana au kupondwapondwa basi uwepo wa jumuiko hilo
linaloitwachama cha siasa unakuwa shakani. Kwa kutolea mfano wa chama changu,
CHADEMA, ni chama cha siasa ambacho tangu kuanzishwa kwake kimekuwa wazi kabisa
kuhusu misingi yake inayosimamia. Iwapo wana CHADEMA watashindwa kuheshimu
misingi ya chama basi uhai wa chama hicho utakuwa shakani na hatimaye hata uhai
wa mfumo imara wa vyama vingi nchini Tanzania.
CHADEMA sasa imejijenga kama chama cha siasa kinachopinga
ufisadi, kinachosimamia uwajibikaji na uwazi katika uendeshaji wa serikali,
kinachopigania siasa za ukweli, kinachotetea haki za raia – haki za kuishi na
kushiriki siasa, kinachotetea rasilimali za nchi.
Katika katiba ya chama hicho kuna misingi 12 ambayo chama
kimejengwa juu yake. Iwapo wanachama wake watasimamia kwa dhati misingi hii
badala ya kusimamia watu, kamwe hapawezi kutokea malumbano yasiyo na msingi
yanayopoteza malengo ya ukombozi mpya kwa Mtanzania. Inasikitisha sana hivi
sasa kwenye siasa za Tanzania, kwa vyama vyote vya siasa, kumekuwa na ufuasi wa
watu badala ya ufuasi wa misingi.
Watu si mawe, hugeuka. Misingi inabaki misingi. Ama
unafuata misingi hiyo au unajiunga na chama kinachofuata misingi unayoitaka, au
unaanzisha misingi mingine katika chama kipya. Ufuasi wa mtu kwenye chama cha
siasa unapaswa kuangaliwa kwa ufuasi kwa misingi inayojenga chama hicho. Ufuasi
wa kiongozi wa CHADEMA unapaswa kupimwa kwa kuangalia ni namna gani kiongozi
huyo anatekeleza kwa vitendo misingi ya chama iliyotajwa hapo juu (kupinga
ufisadi, kusimamia uwajibikaji).
Uadilifu wa mwanachama wa chama hicho utapimwa si kwa
uaminifu kwa kiongozi au mwanachama mwingine wa chama au kikundi cha wanachama,
bali kwa uaminifu na utekelezaji wake wa misingi ya chama. Kiongozi au
mwanachama atakuwa ni msaliti iwapo anakwenda kinyume cha misingi ya chama.
CHADEMA imejipambanua wazi wazi katika ‘utetezi wa
rasilimali za taifa’, kwamba utajiri wa nchi uwe ni ardhi, madini, misitu,
maji, gesi asilia vinatumika kwa maendeleo ya Watanzania na si kwa kikundi cha
watu wachache. Hata masuala ya rasilimali fedha pia imekuwa mstari wa mbele
kama chama kisichotaka mchezo kabisa na kutapanywa kwa mali za taifa.
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa kuna malalamiko
makubwa ya wananchi kuhusu uporaji wa ardhi, migogoro ya ardhi kati ya wafugaji
na wakulima na kati ya wanavijiji na wawekezaji. Malalamiko haya yalikuwa
yanaandikwa na vyombo mbalimbali vya habari vya hapa nchini na hata nje ya
nchi. Katika Bonde la Mto Rufiji maelfu ya ekari za ardhi yamegawiwa kwa
wanaoitwa wawekezaji wakubwa kwa ajili ya kulima miti ya mibono kaburi.
Kule Mkoa wa Katavi katika Wilaya ya Mulele kumekuwa na
sintofahamu kuhusiana na ardhi ambayo ilikuwa inakaliwa na wakimbizi kutoka
nchini Burundi na sasa kugawiwa kwa wawekezaji. Kilosa mkoani Morogoro kumekuwa
na vurugu za mara kwa mara zikihusisha wakulima na wafugaji.
Mkoani Manyara na mkoani Mbeya kumekuwa na malalamiko ya
wananchi kuhusu mashamba yaliyokuwa ya NAFCO na sasa yamebinafsishwa kwa
wawekezaji ambao wamehodhi ardhi bila kuifanyia uzalishaji wowote ilhali
wananchi hawana ardhi. Msingi mkubwa hapa ni kulinda maliasili ya nchi kwa
ajili ya matumizi ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. Kuzuia uharibifu wa
rasilimali za nchi unaofanywa na kikundi cha watu wachache dhidi ya wengi ama
unaofanywa na kizazi cha sasa dhidi ya vizazi vijavyo ni kazi ambayo chama
hicho kimeifanya kupitia wabunge wake.
Mwanachama au kiongozi yeyote wa CHADEMA ambaye hasimamii
msingi huu anakwenda kinyume cha chama na anapaswa kutafuta chama kingine
ambacho kitampa uhuru wa kuruhusu rasilimali za nchi kutumika vibaya. Viongozi
wa chama hicho na hasa wabunge wanapaswa kuwa mstari wa mbele kusimamia msingi
huu. Malalamiko ya wananchi yalikuwa ni malalamiko tu yanayoibuka na kuzama
mpaka pale mbunge kijana alipoamua kushughulikia suala hilo, si kwa kupiga
kelele au kuendeleza kulalamika, bali kwa kutumia njia za kidemokrasia kupitia
Bunge.
Katika Mkutano wa Tisa wa Bunge la 10, Mbunge wa Kawe
alifanikiwa kupitisha hoja bungeni kuhusu usimamizi bora wa ardhi ya Tanzania.
Kiongozi huyu aliona kuwa kuna changamoto zilizoanishwa hapo juu lazima
zifanyiwe kazi kwa faida ya wananchi wa kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Bunge bila kujali itikadi za kisiasa lilipitisha azimio
la kutaka kufanyika kwa tathmini ya ardhi nchi nzima ili kuweza kufahamu ni
ardhi kiasi gani imegawanywa mpaka hivi sasa na kwa nani. Lengo ni kuweka
maamuzi ya kisera kuhusiana na ugawaji wa ardhi ili kulinda wananchi maskini
ambao kila kukicha wamekuwa wakinyang’anywa ardhi kwa kisingizio cha uwekezaji.
Haya ni mafanikio ya kazi za waabunge wa CHADEMA
wanaosimamia misingi ya chama kwa kutekeleza kwa vitendo misingi hiyo. Kutokana
na hoja yenyewe ya ardhi inavyo nufaisha watu binafsi au vikundi vya watu ambao
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, anawafahamu au asiowafahamu, mbunge huyu
angeendekeza ufuasi wa watu badala ya misingi ya chama asingefanikiwa kufanya
masuala haya mazito kwa nchi, yenye mafanikio kwa wananchi wote bila kujali
vyama vyao.
Faida kubwa ya ufuasi wa misingi ni kwamba mafanikio
yoyote yanayopatikana katika utekelezaji wa misingi ya chama,kila mwanachama
anajivunia nayo. Hata hivyo, pale ambapo chama kimegawanyika kwa misingi ya ufuasi
wa watu au vikundi vya watu ni nadra mafanikio ya misingi ya chama
inayotekelezwa na mwanachama ambaye wewe si mfuasi wake kuyaona kama ni
mafanikio ya chama.
Mafanikio yote yatakayopatikana kutokana na hoja yenye
kuhusiana na ardhi yanapaswa kuwa mafanikio ya kujivunia kwa wana CHADEMA wote.
Chama hicho kisione aibu kujivunia mafanikio ya viongozi wake wanaotekeleza
misingi kwa vitendo. Mwelekeo wa siasa za zama hizi ni ya ufuasi wa misingi na
si ufuasi wa watu. Mfuasi wa misingi hawezi kuyumbishwa kwani misingi haiyumbi.
Mwezi ujao nitatolea mfano msingi wa kupinga
ufisadi ambapo tutaona kuhusu usimamizi kwa vitendo wa vita dhidi ya rushwa na
ufisadi kupitia kwa viongozi wa chama hicho.
No comments:
Post a Comment