Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini - TFF, Jamal Malinzi amewatakia kila la kheri Wawakilishi pekee wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CC) timuYoung Africans katika mchezo wake wa marudiano dhidi ya timu ya Etoile du Sahel utakaochezwa kesho nchini Tunisia.
Katika salamu zake Malinzi amesema ,Young Africans wakiwa ndio timu wawakilishi pekee wa Tanzania na Afrika Mashariki katika michuano ya kimataifa barani Afrika wanapaswa kupambana kuhakikisha wanasonga mbele katia hatua inayofuata.
Katika mchezo wa awali uliofanyika wiki mbili zilizopita jijini Dar es salaam, Young Africans ilitoka sare ya bao 1- 1 na Etoile du Sahel, na mshindi wa jumla kwa mchezo wa huo, atacheza hatua ya mtoano (Play-off) dhidi ya timu zitakazokuwa zimetolewa kwenye Ligi ya Mabingwa (CL) kuwania kufuzu kwa hatua ya makundi.
Mchezo huo wa marudiano utapigwa kesho jumamosi katika dimba la Olympique de Sousse katika mji wa Sousse kuanzia majra ya saa 3 kamili usiku kwa saa za Afrika Mashariki na Kati
VPL KUENDELEA WIKIENDI HII
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara inatarajiwa kuendelea mwishoni mwa wiki hii kwa michezo sita kuchezwa katika viwanja mbalimbali nchini, huku michezo mitatu ikichezwa siku ya jumamosi na michezo mingine mitatu ikichezwa siu ya jumapili.
Jumamosi katika Uwanja wa Sokoine wapinzani wa jiji la Mbeya, Prisons FC watakua wenyeji wa wagonga nyundo Mbeya City mchezo utaochezwa majira ya saa 10 kamili kwa saa za Afrika mashariki na Kati.
Katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona wenyeji timu ya Ndanda SC watawakaribisha wakata miwa wa Kagera Sugar, huku jijini Tanga Mgambo Shooting wakiwa wenyeji wa maafande wa JKT Ruvu mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Jumapili katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaa, Simba SC watawakaribisha Azam FC, mchezo ambao unatabiriwa kuwa na upinzani mkali kusaka nafasi ya pili ili mwakani kuweza kuwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Jijini Tanga wagosi wa kaya Coastal Union watawakaribisha timu ya Stand United kutoka mjini Shinyanga, mchezo utakaochezwa kwenye uwanja wa Mkwakwani, huku kwenye Uwanja wa Manungu mjini Morogoro wenyeji Mtibwa Sugar wakiwakaribisha maafande wa Ruvu Shooting.
AMBROSE, NGASA WACHEZAJI BORA VPL MACHI, APRILI
Mchezaji James Mwasote Ambrose wa timu ya Tanzania Prisons FC amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa mwezi Machi 2015 kufuatia kuwapiku wachezaji wengine waliokua wakiwania nafasi hiyo.
Jopo la maalum la makocha ambao hutafuta wachezaji bora kwa kila mchezo na kisha kujumlisha alama za mchezaji kwa kila mchezo na kumpata mchezji bora wa mwezi, ndio hufanya kazi ya kuchagua mchezaji bora kwa kila mwezi.
Mshambuliaji wa Young Africans Mrisho Ngasa amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom mwezi Aprili kufuatia kuwapiku Amos Edward, Frank Domayo na Emmanuel Okwi baada ya kupata alama nyingi za jumla za mchezaji bora kwa kila mchezo.
Kwa kuibuka wachezaji bora wa mwezi Machi na Aprili, James Ambrose na Mrisho Ngasa watazawadiwa fedha taslimu sh. milioni moja kwa kila mmoja kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodaom.
NB: Kesho jumamosi tarehe 02 Mei 2015, kutakua na mkutano na waaandishi na habari saa 5 kamili asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa TFF - Karume, waandishi wote wa habari mnaombwa kuhudhuria bila kukosa.
No comments:
Post a Comment