Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa
taarifa za msiba wa Mufti Mkuu wa Tanzania Tanzania, Sheikh Issa Shaaban bin
Simba, Kiongozi Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kilichotokea
asubuhi ya leo kwa maradhi ya sukari na shinikizo la moyo.
Akitoa
salaam za pole na rambirambi kwa waumini wa madhehebu ya Kiislamu na Watanzania
wote kwa ujumla baada ya kupata taarifa za msiba huo, Mwenyekiti wa CHADEMA
(T), Freeman Mbowe amesema kuwa Mufti Mkuu Simba atakumbukwa kwa namna
aliyosimama kama kiongozi wa dini kupitia kauli zake mara kwa mara akisisitiza
ushirikiano ndani ya jamii ya Watanzania bila kujali tofauti zao katika itikadi
za dini.
“Mara kwa
mara Mufti Mkuu Simba amesikika akiwaambia Watanzania, si Waislam pekee
aliokuwa akiwaongoza kiroho, hata wale wanaoamini katika madhehebu tofauti,
umuhimu wa kudumisha ushirikiano miongoni mwa dini mbalimbali na makundi
mengine katika jamii ikiwa ni mojawapo ya misingi ya kuimarisha umoja wa taifa
letu.”
“Naungana na
Waislam wote nchini katika wakati huu wa kuomboleza kifo cha kiongozi huyu wa
kiroho. Kwa niaba ya niaba ya uongozi wa CHADEMA, wanachama, wapenzi na
wafuasi, natoa salaam za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, BAKWATA,
viongozi wa kiroho nchini na Watanzania wote ndani na nje ya nchi walioguswa na
msiba huu mzito.”
“Mwenyezi
Mungu awatie nguvu wote na kuwafanyia wepesi katika wakati huu mgumu wa majonzi
ya msiba wa Mufti Mkuu Simba,” amesema Mbowe
Inna Lillahi
wa inna ilaihi raji’un.
Imetolewa leo Jumatatu, Juni 16, 2015
na;
Idara ya Habari na Mawasiliano-
CHADEMA
No comments:
Post a Comment