Afisa mkuu wa uendeshaji wa kampuni ya Acacia Mishel Ash akimvisha medali mshindi wa mbio hizo Martha Antony wakati wa Hafla ya Kutoa zawadi kwa washindi.
Washiriki wa mbio za baiskeli zijulikanazo kama “Acacia
Tufanikiwe Pamoja Lake Zone Cycle Challenge” kutoka mikoa ya Shinyanga
na Mwanza wameendelea kuudhihirisha umma wa wakazi wa kanda ya ziwa na
watanzania kwa ujumla kuwa mpaka sasa hawana mpinzani baada ya washiriki wa
mbio hizo kuibuka kidedea katika fainali za kumtafuta mshindi wa kanda hiyo.
Washiriki wa mikoa hii miwili wamejinyakulia nafasi
zote za juu na hivyo kuwashinda wenzao wa mikoa mingine ya Kanda ya ziwa
ikiwemo Kagera, Mara, Geita na Simiyu.
Katika mbio za wanaume za umbali wa kilometa 156.6
kutoka Kahama mpaka Tinde na kisha Kurejea Kahama, mshindi wa mwaka jana
Masunga Duba (Mwanza) aliibuka tena kidedea huku nafasi ya pili ikichukuliwa na
Lupilya Hamis(Shinyanga) na nafasi ya tatu ikimuendea Kulwa Tuki(Shinyanga),
washindi hawa wamejinyakulia kitita cha pesa taslimu Sh1,500.000/- kwa mshindi
wa kwanza, Sh1,200.000/= mshindi wa pili na Sh800,000/= kwa mshindi wa tatu.
Kwa upande wa mbio za wanawake za umbali wa kilometa
80, kutoka Kahama mpaka Mwakata Kisha kurejea Kahama, timu ya mkoa wa Mwanza
imedhihirisha kuwa wao bado ni mabingwa kwa kuibuka tena washindi wa mbio hizo,
huku mshindi wa mbio za Mwaka jana Martha Antony, akiibuka mshindi wa kwanza
akifuatiwa na Laulensia Luziba na nafasi ya tatu ikienda kwa Veronica Simon.
Washindi hao wamepata zawadi ya pesa taslimu Sh1,200.000/= kwa mshindi wa kwanza,
Sh800,000/= mshindi wa pili na Sh600,000/= mshindi wa tatu.
Mbio hizo ambazo zimeandaliwa na Chama cha Baiskeli
Tanzania (CHABATA) kwa udhamini wa kampuni ya uchimbaji wa Madini ya Acacia,
inayomiliki migodi ya North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi, yote ikiwa mikoa ya
kanda ya ziwa, kupitia mpango wake wa Tufanikiwe Pamoja ikiwa ni mara ya
pili sasa ambapo mashindano ya mwaka huu yameonyesha mafanikio makubwa kutokana
na maandalizi mazuri yaliyofanyika.
Akizungumza na washiriki wa mashindano hayo Mkuu wa
wilaya ya Kahama Benson Mpyesa, ambaye alikua mgeni rasmi wa fainali hizi,
amesema ana imani kuwa mashindano hayo yatasaidia kuibua vipaji ambavyo
vitauletea sifa mkoa wa Shinyanga, Kanda ya ziwa na hata taifa kwa ujumla kwani
baiskeli kwa maeneo hayo ndiyo jadi yao.
Awali akimkaribisha Mkuu wa wilaya kuzungumza na
washiriki hao, Makamu wa Rais wa Acacia Deo Mwanyika amesema kampuni ya Acacia
imekuwa ikifanya shughuli za uchimbaji unaojali na ndio maana iliona vyema
kuweka udhamini wake pia katika mchezo wa baiskeli, “toka tuanze huu sasa ni
mwaka wa pili na tunayaona mafanikio makubwa kwani hata maeneo ambapo mchezo
huu ulikuwa hauchezwi sasa unachezwa, hali ambayo imeongeza hamasa na idadi ya
washiriki.”
Aidha Makamu wa Rais huyo wa Acacia amesema mipango ya
kampuni kwa sasa ni kuona pia inashiriki katika kuendeleza michezo mingine
ikiwemo na soka.
|
No comments:
Post a Comment