Kuanzia jana
Julai 15 hadi 19 mwaka huu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kimefungulia rasmi milango kwa watu wenye nia na sifa kujitokeza kuchukua na
kurejesha fomu za kuwania ubunge kwenye majimbo yenye wabunge wa chama hicho.
Aidha, baada
ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza majimbo mapya 26 ya uchaguzi, CHADEMA
pia kimelazimika kupangua ratiba ya awali na sasa kimeruhusu wanachama wote
wenye sifa kuchukua na kurejesha fomu za kuwania uteuzi wa ndani ya chama katika
nafasi za udiwani na ubunge katika majimbo yote ya uchaguzi nchi nzima.
Kupitia
Waraka wa Katibu Mkuu Namba 5 wa mwaka 2015, uliosainiwa na Katibu Mkuu Dk.
Willibroad Slaa, chama kimesema kuwa wananchi wote wenye nia na sifa za
kuchukua fomu za ubunge kwenye majimbo yote yakiwemo mapya wanaruhusiwa kufanya
hivyo kuanzia tarehe 15/07/2015 hadi saa 10 jioni tarehe 19/07/2015.
Kwa mujibu
wa Katibu Mkuu Dk. Slaa, kwa nafasi za udiwani , zoezi la kuchukua na kurejesha
fomu katika kata zote nchi nzima limeongezwa muda kuanzia Julai 15, 2015 hadi
29/07/2015 saa 10 jioni.
Itakumbukwa
kuwa hapo awali CHADEMA ilitoa ratiba yake ya uteuzi wa ndani ambapo ilionesha
kuwa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania udiwani na ubunge katika kata
na majimbo yenye madiwani au wabunge wa chama hicho ulitakiwa kusubiri hadi
halmashauri zitakapokoma au bunge litakapokuwa limevunjwa.
Katibu Mkuu
pia ameelekeza kuwa baada ya NEC kutangaza majimbo mapya 26 kwa upande wa
Tanganyika, fomu za kuwania uteuzi katika majimbo hayo zitaendelea kutolewa
katika ngazi ya taifa, mkoa, wilaya na jimbo kwa utaratibu ule ule ambapo
makatibu wa majimbo mama (yale ya zamani) wataendelea kutoa fomu kwa ajili ya
majimbo mapya.
“Wagombea
ambao walishachukua na kurejesha fomu wana haki ya kuamua jimbo lipi wanaenda
kugombea na hawalazimiki kuchukua fomu upya…watatakiwa kuujulisha uongozi wa
chama ngazi ya jimbo kwa barua rasmi kuonesha kuwa fomu yake iwe ni ya jimbo
lipi kati ya jimbo mama ama jipya na nakala ya barua hiyo inakiliwe ngazi ya
wilaya, mkoa, kanda na taifa,” ameelekeza Katibu Mkuu Dk. Slaa.
Kuhusu zoezi la kura ya maoni
Kupitia
waraka huo ambao umetumwa kwa Waratibu wa Kanda, Wenyeviti na Makatibu wa
majimbo, Katibu Mkuu Dk. Slaa ameagiza kuwa majimbo yote yanatakiwa kuanza zoezi
la kura ya maoni tarehe 20-25 Julai
mwaka huu kwa kuzingatia Mwongozo wa Taratibu za Kura ya Maoni ambao
umeshatumwa nchi nzima.
“Kwa majimbo ya yaliyogawanywa kila jimbo
litafanya mchakato wake wa kura ya maoni kwa kusimamiwa na mamlaka zilizotajwa
katika mwongozo husika. Hii maana yake ni kwamba zoezi la kura ya maoni
litafanyika kwa siku 6 mfululizo. Kila kanda inapaswa kuweka ratiba yake ya ndani
katika muda huo na kuhakikisha kuwa majimbo yote, ya zamani na mapya, katika
kanda husika yakamilishe kura za maoni ndani ya tarehe hizo.
“Kamati Kuu
iliazimia pia kuwa kura za maoni nafasi ya udiwani zitaanza kufanyika kuanzia
tarehe 30 Julai hadi 5 Agosti, 2015. Hii maana yake ni kuwa zoezi la kura za
maoni kwa nafasi ya udiwani litaanza baada ya kumalizika kwa zoezi la kura za
maoni nafasi ya ubunge,” ameagiza Katibu Mkuu Dk. Slaa kupitia waraka huo.
Aidha Katibu
Mkuu amewaagiza Waratibu wa Kanda za CHADEMA kusimamia utaratibu wa
kuwatangazia wananchi katika majimbo yote kwa njia anuai ikiwemo vyombo vya
habari, mitandao ya kijamii, matangazo kwenye mbao na nafasi mbalimbali za
hadhara ili Watanzania wote wapate fursa ya taarifa hiyo muhimu.
Imetolewa leo Alhamis, Julai 16, 2015
na
Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
No comments:
Post a Comment