Saturday, July 4, 2015

ZITTO AWAPONGEZA UKAWA KWA KUZOMEA BUNGENI

Wakati bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania likigubikwa na sintofahamu baada ya wabunge wanaounda kambi ua upinzani maarufu kama ukawa kugomea na kufanya vurugu wakati wa uwasilishwaji wa miswada mitatu ya dharura ya gesi na mafuta, naye Kiongozi mkuu wa chama kipya cha ACT mh ZITTO KABWE ameibuka na kusema kuwa kitendo cha kugomea miswada hiyo isiwasilishwe ni kitendo cha kishujaa na kinapaswa kupongezwa na kila mtanzania mwenye mapenzi mema ya nchi yake.Shughuda wako Exaud mtei msaka habari anasimulia-------
Pongezi hiyo ameitoa leo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wa kwanza wa hadhara wa chama hicho katika jiji la Dar es salaam ambapo amesema kuwa umefika wakati sasa wa kuwaambia serikali ya CCM kuwa imetosha kuburuzwa na kufanya jambo la kishujaa kama lililofanywa na viongozi wa upinzani bungeni.
“Huwezi kujadili maswala makubwa kama ya gesi na mafuta ambayo moja kwa moja yanawagusa watanzania ukayafanya mambo ya dharura na kutaka kuyapitisha haraka haraka bila kuwashirikisha watanzania ambao ndio wenye mafuta yao,ni jambo ambalo haliwezekani na watanzania hawatakubali kuona mafuta na gesi yao inamilikiwa na watu wachache”amesema mh ZITTO.
Ameongeza kuwa swala la mikataba ya gesi nchini na mafuta hayapaswi kufanywa kwa siri wala kukimbizwa na badala yake bunge la sasa liachane na miswada hiyo hadi bunge lijalo chini ya serikali mpya waanze kujadili upya miswada hiyo.
Katika mkutano huo uliokusanya maelfu ya wanachama na wakazi wa Dar es salaam mwembe yanga chama hicho kimeutumia kujitambulisha rasmi kwa wananchi wa Dar es salaam na kueleza malengo yao kwa siasa za Tanzania na kwanini wamekuja na chama kipya.
Mh ZITTO anasema kuwa chama cha ACT sio chama ambacho kimepandikizwa kwa ajili ya kuzigawa kura za watanzania kama ambapo imekuwa ikielezwa kila kona bali ni chama ambacho kimekuja kubadilisha mwelekeo wa siasa za Tanzania na kufanya siasa za maswala ya wananchi zaidi zaidi ya kufanya siasa za kuwajadili watu na matusi.
Moja kati ya mambo ambayo anasema kuwa chama hicho kimeshamiria kuyafanya ni kurudusha misingi na miiko ambayo iliwekwa na baba wa taifa mwalimu nyerere kwa kulifufua azimio la arusha ambapo kwa sasa wamelipa jina la azimio la tabora.
Naye mwenyekiti wa chama hicho Taifa mama Anna Mghwira

amewaeleza wana Dar es salaam kuwa moja kati ya mipango ya chama hicho ni kuifanya Dar es salaam iwe salama kwa wakazi wake tofauti na sasa ambapo amesema kuwa Jiji hilo limekuwa sio salama kutokana na kutokuwa na mpangilio unaoliweka kuwa jiji salama.
Chama cha ACT kimeendelea na ziara zake katika mikoa mbali mbali kujitambulisha kwa wananchi kwa lengo la kupata wanachama zaidi kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu

No comments: