Thursday, September 24, 2015

KOVA-Ulinzi SIMBA na YANGA upo asilimia Mia msiogope


JESHI LA POLISI KANDA MAALUM  DAR ES SALAAM KUIMARISHA ULINZI WAKATI WA MECHI YA SIMBA NA YANGA ITAKAYOFANYIKA TAREHE 27/09/2015

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam limejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa pambano la mpira wa miguu kati timu za SIMBA na YANGA (ambazo ni watani wa jadi) lenye kuvuta hisia kwa mashabiki wengi wa hapa Tanzania, na nchi jirani hapa Afrika Mashariki linafanyika katika hali ya amani na usalama. Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Taifa tarehe 27/09/2015.

Wananchi wanashauriwa wasiwe na shaka yoyote ya kiusalama na pia watupe ushirikiano kwa kutoa taarifa  za jambo lolote watakaloliona kuwa linaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani kwa kipindi chote watakapokuwa nje au ndani ya uwanja.

Wananchi wanatakiwa kuwa watulivu wakati wa kushangilia mechi hiyo huku kila mmoja akiwa amekaa kwenye kiti kulingana na tiketi aliyokata ili kuondoa usumbufu usiokuwa wa lazima.


Kutakuwa na askari wa kutosha kuzunguka maeneo yote muhimu ya uwanja huo. Ulinzi utaimarishwa na askari waliovalia nadhifu na wenye weledi wa hali ya juu ambao watakuwa katika milango mikuu ya kuingilia na ndani ya uwanja kuzunguka majukwaa ya washabiki wa timu zote mbili.

Pia kutakuwa na ulinzi kwa kutumia camera za ulinzi (CCTV Camera) zilizofungwa kuzunguka uwanja huo ili kusaidia kuimarisha ulinzi katika mechi hiyo muhimu. Kwa mantiki hii matukio yote yatakayokuwa yanatokea yatarekodiwa.

Aidha, kutakuwa na doria ya Mbwa wa Polisi na Farasi waliopata mafunzo ya kisasa ambao watazunguka nje ya uwanja kuimarisha ulinzi ili kuhakikisha mechi hiyo ya mpira inamalizika kwa amani na utulivu.

Wananchi wanashauriwa kukata tiketi zao mapema kwenye vituo vilivyoainishwa na vyombo husika ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima. Wale ambao watalazimika kukata tiketi zao uwanjani, wanashauriwa kufuata utaratibu uliopangwa.
Kutakuwa na ukaguzi mkali katika milango yote mikubwa ili kuhakikisha wanaoingia uwanjani wote hawana vitu vyenye uwezekano wa kuleta madhara kwa watazamaji wengine.

Ili kuhakikisha hali ya usalama uwanjani imeimarishwa, wananchi wanashauriwa kutoa ushirikiano na vyombo vya usalama kwa kuzingatia mambo yafuatayo:

·        Ni marufuku kuingia na chupa za maji uwanjani,
·        Ni marufuku kuingia na silaha ya aina yoyote  uwanjani.
·        Hairuhusiwi kupaki magari ndani ya uwanja isipokuwa maeneo maalum yaliyoruhusiwa tu.
·        Ni marufuku kukaa sehemu ambazo tiketi haziruhusu.

·        Aidha, kwa urahisi wa mawasiliano wananchi wasisite kutoa taarifa za uhalifu kwa namba muhimu za simu zifuatazo:

1.    RPC ILALA:  LUCAS MKONDYA – SACP                   0715 009 980
2.   RPC TEMEKE: ANDREW SATTA – ACP                     0715 009 979
3.   RPC K’NDONI: CAMILLIUS WAMBURA – ACP   0715 009 976
4.   PETER SIMA: - ACP 0712 891 999 (Mkuu wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum Dar es Salaam).


S. H. KOVA,
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM,
DAR ES SALAAM.


No comments: