Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Charles Boniface Mkwasa ameendelea na mazoezi ya kukinoa kikosi chake kujiandaa na mchezo dhidi ya Algeria Novemba 14 jijini Dar es salaam kuwania kufuzu kwa kombe la Dunia nchini Urusi mwaka 2018.
Baada ya kufanya mazoezi kutwa mara mbili (asubuhi na jioni) kwa siku tatu, leo Ijumaa kocha Mkwasa amekiongoza kikosi chake kufanya mazoezi mara moja wakati wa jioni katika uwanja wa Edenvale.
Mkwasa amesema baada ya kufanya mazoezi ya kujenga mwili, stamina, na pumzi sasa kazi anayoifanya ni kutengeneza mfumo wa kikosi chake kinachojiandaa na mchezo dhidi ya Mbweha wa Jangwani.“Tulipofika tulianza na mazoezi ya utimamu wa mwili, stamina na pumzi ili kuhakikisha wachezaji wote waliopo kambini wanakuwa katika kiwango kimoja kutokana na kuwa wachezaji wanatoka katika timu tofauti na zenye walimu na mifumo tofauti” Alisema Mkwasa.
“Sasa baada ya wachezaji kufanya mazoezi kwa siku nne kuweka uwiano sawa kiwango cha kimazoezi (fitness level) kwa sasa tunafanya kazi kutengeneza mfumo na jinsi ya uchezaji” aliongeza Mkwasa.
Stars inaendelea na mazoezi leo jioni na kesho Jumamosi itafanya mazoezi asubuhi katika uwanja wa Edenvale
No comments:
Post a Comment