WAKAGUZI
WA POLISI 07 PAMOJA NA ASKARI WA VYEO MBALIMBALI 157 JUMLA 164 WA POLISI KANDA
MAALUM DAR ES SALAA WABADILISHWA KITENGO
CHA USALAMA BARABARANI
Jeshi la Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam limewabadilisha kazi wakaguzi 07 na askari wa vyeo
mbalimbali 157 wa kikosi cha Usalama barabarani ambao utendaji wao umekosa
tija. Uamuzi wa kuwabadilisha askari hao kutoka kikosi cha usalama barabarani
kwenda kazi nyingine mbalimbali za kawaida umetokana na ufuatiliaji wa muda
mrefu wa tabia na mwenendo wa askari hao wakati wa utendaji wao wa kazi.
Utendaji wao
umeonekana sio wa kuridhisha ndiyo maana baadhi yao wamekuwa wakilalamikiwa
mara kwa mara na wananchi. Aidha makamanda wa Mikoa yote ya Polisi mkoa wa Dar
es Salaam ya ILALA, KINONDONI na TEMEKE wametakiwa kufuatilia kwa makini tabia
na mienendo ya askari walio chini yao ili kuhakikisha kwamba hazijitokezi kero
dhidi ya wananchi na kinachotakiwa ni huduma nzuri zitakazolifanya Jeshi la
Polisi lionekane kwamba linatekeleza wajibu wake kwa kuzingatia weledi na
ufanisi wa hali ya juu.
Kubadilishwa askari
hao ni hatua ya kwanza kwani bado uchunguzi zaidi unafanyika kwa wale ambao
wataendelea kufanya kazi chini ya kiwango. Aidha askari ambao watabainika
wamejihusisha ma makosa ya moja kwa moja ya jinai kama vile kujihahusisha na
vitendo vya rushwa au ukiukwaji wa maadili ya Jeshi la Polisi watashtakiwa
katika mahakama za kijeshi au za kawaida kwa makosa yatakayothibitishwa.
Uchunguzi zaidi
unaendelea kuhusu vikosi vingine vya Kanda Maalum na Jeshi la Polisi kwa jumla
ili kubaini kama kuna askari, Mkaguzi au Afisa anayefanya kazi chini ya
kiwango, bila tija katika utendaji au anafanya kazi katika kiwango
kisichoridhisha na analalamikiwa, nao watachukuliwa hatua kama hizi au nyingine
za kisheria.
Watendaji wote wa
Jeshi la Polisi wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii na weledi wa hali ya juu ili
kuwahakikishia wananchi kwamba wananufaika kutokana na utendaji wa Jeshi la
Polisi na kulifanya jiji la Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla pawe mahali
salama pa kuishi.
WAHAMIAJI
HARAMU 105 WAKAMATWA KWA KUINGIA NCHINI BILA KIBALI
Jeshi la Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam asubuhi ya leo 26/11/2015 limewakamata wahamiaji haramu
wapatao 105 huko Tabata Segerea Ilala jijini Dar es Salaam. Baada ya kupata
taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwa huko maeneo ya Tabata Segerea kuna
nyumba ina wahamiaji haramu, Polisi walizunguka nyumba hiyo tangu alfajiri ya
leo na hatimaye kwa kutumia utaratibu wa kisheria nyumba hiyo ilipekuliwa ndipo
walipokutwa watu hao 105 wanaume na iligundulika kwamba wanatoka nchini
Ethiopia.
Watuhumiwa wote
walihojiwa kuhusu vibali vya kuingia nchini na kukutwa hawana ndipo
ilipogundulika waliingia kupitia njia za panya au kwa mbinu ambazo bado
zinachunguzwa.
Uchunguzi wa awali
unaonyesha kwamba watu hawa walikuwa chini ya usimamizi wa mtu mmoja aitwaye
ZABIBU D/O UMWIZA, Miaka 25, anayesemekana ni raia wa Burundi anayejihusisha na
biashara ya usafirishaji wa binadamu kutoka nchi za Afrika kwenda Ulaya kwa
malipo yanayosemekana kufikia US Dolla 1000 kwa mtu mmoja. Kutokana na tukio
hili jinsi lilivyo tumewajulisha idara ya uhamiaji na tunashirikiana nao katika
upelelezi ili hatimaye sheria ichukiue mkondo wake.
Tunawaomba wananchi
washirikiane na Jeshi la Polisi katika kuzuia makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja
na hili la wahamiaji haramu ambao wanaweza kuwa tishio kwa usalama wa maisha ya
wananchi na hata kwa uchumi wa taifa.
KUKAMATWA
KWA SILAHA SMG MOJA, BASTOLA NNE, JUMLA YA RISASI 36 PAMOJA NA WATUHUMIWA 13.
Katika hatua nyingine
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea na oparesheni kali ya
kuwasaka kuwakamata wahalifu wa aina zote na kuhakikisha hatua kali za kisheria
zinachukuliwa dhidi yao.
Katika oparesheni hiyo
Jeshi la polisi limefanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa 13 kwa tuhuma za
makosa mbalimbali yakiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha, unyang’anyi wa
kutumia nguvu, wanaojihusisha na mitandao ya kigaidi pamoja na makosa mengine.
Watuhumiwa hao wamekamatwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam
kufuatia ushirikiano toka kwa wananchi.
Pia oparesheni hiyo
imefanikisha kukamatwa kwa bunduki moja CHINESE 56 (SMG) iliyofutwa namba zake,
bastola tatu ambapo mbili ni aina ya BERETA na bastola moja aina ya CHINESE
zote zikiwa zimefutwa namba zake. Aidha zimekamatwa jumla ya risasi 36 katika mchanganuo ufuatao: risasi za SMG zipo 08, risasi za bastola zipo 13, na risasi za shotgun
zipo 15. Aidha wamekamatwa jumla
ya watuhumiwa 30 kuhusiana na matukio haya ambapo upelelezi unaendelea ili
hatua kali dhidi yao ziweze kuchukuliwa.
POLISI KANDA MAALUM DAR ES SALAAM YATOA ONYO KALI
KWA WENYE TABIA YA KUJICHUKULIA SHERIA MIKONONI. WATUHUMIWA 49 WASHIKILIWA NA
KADHAA WAFIKISHWA MAHAKAMANI.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es
salaam linawashikilia watu 31 kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi katika
matukio tofauti yaliyosababisha vifo, majeruhi, na uharibifu wa mali kwa baadhi
ya watu. Hii ni tabia iliyoanza kuota mizizi jijini Dar es Salaam na mikoa
mingine ambayo pia ni kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu.
Katika
tukio la kwanza mnamo tarehe 27/10/2015 huko maeneo ya
SUKITA Buguruni, Ilala jijini Dar es Salaam walikamatwa watu 27 kwa tuhuma a
kujichukulia sheria mikononi baada ya kumshambulia mtu mmoja jina halijafamika
kwa kumpiga mawe sehemu mbalimbali za mwili kisha kumchoma moto lakini
aliokolewa na askari waliokuwa doria.
Katika kuwatafuta
wahusika, alikamatwa mtuhumiwa ELIUD S/O ELIA MWAKISUNGA @ MAJANI na wenzake
27. Aidha, watuhumiwa 08 kati ya waliokamatwa wametambuliwa kuhusika na tukio
hilo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote.
Katika
tukio lingine Jeshi la Polisi kanda Maalum
linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kumshambulia mtu mmoja aliyejulikana
kwa jina maarufu la “Kinjunga”, miaka 27, mkazi wa Somangila, Temeke jijini
dare s Salaam.
Tukio hilo lililotokea
tarehe 21/11/2015 huko Malimbika kata ya Somangila, wilaya ya Kigamboni, Temeke
jijini Dar es Salaam ambapo watu hao wanadaiwa kumshambulia na kumpiga kwa fimbo
na mawe hadi kufa na kisha kumchoma moto baada ya kumtuhumu kutaka kumpora
abiria mmoja aliyekuwa akiteremka kutoka katika daladala ambalo halikusomeka
namba zake mara moja.
Taarifa za awali
zinasema marehemu alikuwa na wenzake
wakitumia pikipiki ambayo pia haikusomeka namba yake na KINJUNGA
alishuka na kujaribu kumpota abiria huyo aliyepiga kelele ndipo watu walimvamia
na kumpiga hadi kumuua. Katika tukio hilo watuhumiwa kadhaa wamekamatwa ambao
ni:
1. RUDOVICK
S/O VINCENT, Miaka 27, Mkazi wa Malimbika Somangila.
2. JOHN
S/O SALUM, Miaka 36, Mkazi wa Malimbika Somangila.
3. MOHAMED
S/O SALUM, Miaka 36, Mkazi wa Malimbika Somangila.
Katika
tukio lingine, tarehe 27/10/2015 majira ya saa07:20
huko mtaa wa Sandali, Temeke walikamatwa
watuhumiwa 08 wanaosadikiwa ni wafuasi wa chama fulani cha siasa kwa
tuhuma za kuchoma moto ofisi ya Afisa Mtendaji Kata ya Sandali na kuteketeza
maboksi yaliyokuwa na matokeo ya kura za udiwani. Watuhumiwa wote wamefikishwa
mahakamani.
Majina ya watuhumiwa
hao ni kama ifuatavyo:
1. SHABANI
S/O ABDALLAH @ POLLOMO, Miaka 40, Mkazi wa Temeke.
2. SALIM
S/O ABDALLAH NGUNDA, Miaka 27, Mfanyabiashara , Mkazi wa Mbagala Charambe.
3. RAJAB
S/O OMARY, Miaka 25, Mwanafunzi, Mkazi wa Temeke Mikoroshini.
4. SEIPA
S/O RAMADHANI KANIKI, Miaka 38, Mkazi wa Temeke Mikoroshini.
5. OMARY
S/O JUMA BOMEZA, Miaka 56,
Mfanyabiashara, Mkazi wa Temeke Sandali.
6. MARIAM
D/O SIFA, Miaka 51, Mkazi wa Temeke Mikoroshini.
7. BONIPHASI
S/O RAYMOND, Miaka 30, Mfanyabiashara, Mkazi wa Temeke Maganga.
8. NORBERT
S/O RAYMOND, Miaka 26, Mfanyabiashara, Mkazi wa Temeke Maganga.
Aidha, Jeshi la Polisi
linatoa onyo kali kwa watu au kundi la watu wenye tabia ya aina hii kuacha mara
moja kwani ni vitendo vya kihuni, kikatili na havikubaliki katika jamii ya
watanzania. Pia, vitendo hivi ni kinyume cha sheria za nchi yetu na kinyume cha
haki za binadamu. Kikundi au mtu yeyote atakayekamatwa kuhusiana na tuhuma za
aina hii atachukuliwa hatua kali za kisheria bila ajizi.
S. H. KOVA
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM
DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment