Wednesday, December 23, 2015

Raia Waamirifu wilayani Kahama Wakerwa na Utoro.


Pichani nikiwa nazungumza na   Raia waamilifu kutoka kijiji cha Kilago  wilayani Kahama ambapo nilipata nafasi ya kujua mambo  mbalimbali ikwemo mchango wa uraghabishi  katika kijiji hicho katika sekta ya elimu 

Na Krantz Mwantepele , Kahama
Utoro ni tabia ya kuondoka au kutokufika mahali mara kwa mara bila ya kutoa taarifa. Tabia hii ipo kwenye maeneo ya makazini pamoja na shuleni. Katika baadhi ya kata za wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.

Tabia hii imekuwa kero kwa wanajamii wa kata za Nyandekwa na Kilago kwa kuwa inawarudisha nyuma kimaendeleo. Wakiwa kama sehemu ya wananchi wa kata hizo, waraghbishi wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto watoro wanahudhuria shuleni.

Ikiwa kama sehemu ya uraghbishi, kutambua changamoto zinazokabili jamii wanayoishi, waraghbishi walitambua kwamba hili ni tatizo na hivyo kuamua kulishughulikia.

“Nikiwa njiani kuelekea kwenye shughuli zangu, nikakuta watoto wamejibanza kwenye kichaka, na wengine walikuwa wakicheza mpira. Nikataka kujua kulikoni mbona hawapo shuleni, wakati ni muda wa masomo?”

Hili ni swali ambalo raia mwamilifu na mraghbishi Paul Izengo toka katika kijiji cha Nyandekwa kilichopo wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, alitaka kulipatia majibu yake. Udadisi huu ndio uliopelekea kwa yeye kuwasogelea watoto ambao kimsingi walitakiwa kuwa shuleni mda huo na kutaka kujua kulikoni.
Na jibu lilikuwa ni moja tu kwamba wametoroka shule na kwanini watoroke. Paul hakuishia tu kujiuliza maswali, alikwenda hatua moja mbele kwa kuwafuata watoto wale na kuwauliza,
“Nyinyi mnafanya nini hapa? Wakati huu ni muda wa kuwa darasani. Haya shuleni haraka, niliwakaripia, hao wakakimbia.”
Kukimbia wakati umeulizwa ni dalili ya kuogopa kutokana na kosa unalojua umefanya. Watoto wale walijua kwamba wamekosa, na kosa lilikuwa ni utoro shuleni. Hili si tatizo tu la kijiji cha Nyandekwa, hata Kilago pia ambapo baadhi ya wazazi wanatajwa kuwa chanzo cha tatizo hilo la utoro.
Akiwa kama raia mwamilifu na mraghbishi toka katika kijiji cha Kilago, wilayani Kahama Mathew Charles anasema:
“Wazazi ndio sababu ya utoro huu mashuleni, wanawapa watoto wao kazi muda ambao ni wa kwenda shule. HIvyo unapomwambia ukweli anachukia anaona kama vile unamwingilia maisha yake,”

Tabia hiyo ya baadhi wa wazazi kuunga mkono utoro wa watoto wao kwa visingizio vya kutaka kuwa huru na maisha, haviwatakatishi tamaa waraghbishi hao. Kwani hili ni jukumu lao katika kuhakikisha watoto wanapata haki zao.
Katika kusadia watoto hao wanarudi shuleni, waraghbishi kupitia mtandao wao wa wilaya ya Kahama, wamekuwa wakitoa elimu na kuwakishirikisha baadhi ya wazazi wa watoto hao kutambua umuhimu wa elimu na inapobidi kukamata watoto watoro na kuwapelekashule.

 Na baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwafuata na kuomba ushauri wanapoona mtoto ameanza kuwa na tabia ya utoro. Na mara nyingi wamekuwa wakiwashauri wazazi hawa kushirikiana na walimu ili kuweza kufuatilia maendeleo ya watoto wao. Akifafanua hilo Michael Mathew anasema:

“Kwa mfano katika kipindi cha mwezi wa 10 wazazi wawili wamekuja kuniomba niongee na watoto wao umuhimu wa kwenda shule. Na nafarijika kuona harakati zangu za uraghbishi zinatambuliwa kwenye kijiji change.


Raia Waamilifu, Mathew Charles (kushoto) wa kijiji cha Kilago na Alphonce Peter toka kijiji cha Ufala wilayani Kahama wakifurahia jambo walipkuwa wakijadili tatizo la utoro mashuleni

Tukiacha hili za wazazi kutowapeleka watoto wao shule kwa sababu mbalimbali, ambapo serikali imekuwa ikiwachulia hatua kali za kisheria wazazi hao, watoto wenyewe nao ni chanzo cha kingine cha utoro mashuleni. Wengine wanaaga wamekwenda shule lakini ukweli ni kwamba hawafiki shule na badala yake wanajificha wanapokujua hadi muda wa kurudi unapofika nao hurejea majumbani kana kwamba wanatoka shule.
Hivyo ni wajibu wa raia mwamilifu na aliye mraghbishi anapaswa kuhakikisha watoto wanapata haki yao hii ya msingi ya elimu. Na hivyo ikibidi hata kutumia nguvu, kama anavyosimulia Mathew Charles:
“Muda mwingine nawabeba kwa nguvu watoto hadi shuleni na kuwakabidhi kwa mwalimu. Nimeshafanya hivyo kwa watoto watano sasa. Tunajua kwamba wasiposoma sasa watakuwa mizigo kwenye jamii. Kuna siku watatukumbuka kwamba tulikuwa tunawasaidia,”
Ni dhahiri kwamba tatizo hili ni kubwa na si jukumu la walimu peke yao?
Nikiwa katika picha ya pamoja na waragahbishi na raia waamilifu wa kijiji cha Kilago wilayani Kahama siku za hivi karibuni 
Kila mwananchi pale alipo ana jukumu la kuhahakisha huduma bora za jamii zinapatikana kwa mustakabali wa maendeleo yao. Katika kufanikisha hili raia waamirifu ama waraghbishi toka katika vijiji vya kata ya Nyandekwa na Kilago wameonesha njia katika kuhakikisha wanafunzi watoro wanahudhuria shuleni.

Waraghbishi na Raia Waamilifu toka katika kijiji cha Nyandekwa wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano wao hapo kijijini
                                                              
Akielezea jinsi alivyoamua kushughulikia tatizo hilo kijijini pao, Paul ambaye pia ni kiongozi wa waraghbishi wapya kutoka kijiji cha Nyandekwa anasema:

“Nililazimika kumpigia simu mwalimu mkuu na kuomba kuonana naye kwa lengo la kujadiliana naye kuhusu hili tatizo. Na pale ndipo nilipoweza kuelewa ukubwa wa tatizo la utoro. Hivyo nikakubaliana na mwalimu kuwa tutasaidiana katika kuhakikisha kwamba watoto watoro wanahudhuria shuleni.”
Kwa mujibu wa orodha aliyokabidhiwa mraghbishi Paul Izengo na mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nyandekwa, kuna wanafunzi 21 ambao wameripotiwa utoro kati ya 449 wa shule hiyo.
Kitendo hiki cha mraghbishi kuamua pasipo kulazimishwa na mtu kufuatilia suala la utoro wa wanafunzi katika shule yao ya msingi pale kijijini, ndicho ambacho raia mwamilifu anatakiwa kukifanya.
Raia mwamilifu ni yule ambaye anachukua hatua kwa kushirikiana na wanajamii wengine wa maeneo yake. Huyu ni yule anayetambua majukumu na haki zake kwa mujibu wa ibara ya 12 hadi 24 ya Katiba ya Muungano wa Tanzania. Huyu ni raia anayependa kuona mabadiliko chanya kwenye jamii yake. Huyu ni yule anayetenda pasipo kulazimishwa, bali kwa utashi na uelewa wake kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa. 
Katika kuhakikisha anaelewa vizuri chanzo cha tatizo hilo, ilimlazimu Paul kwenda kumtembelea mzazi ambaye mtoto wake yumo kwenye orodha wa watoro. Na huko alitaka kujua, nini hasa kinachosababisha tatizo hilo.
“Nilikwenda kwa mama mzazi wa mmoja wa wale watoto walioripotiwa kuwa watoro. Lengo langu nilitaka kujua nini hasa tatizo mpaka mtoto haendi shuleni. Ndipo nilipogundua kuna changamoto kubwa zaidi. Inahitajika elimu ya ziada kutolewa,” 
Mama mzazi huyo, alimweleza mraghbishi huyo kwamba michango kwa ajili ya kulipia mitihani ya watoto wake waliopo darasa la 4 na la 6 ni changamoto kubwa inayomkabili. Kushindwa huko kuwalipia watoto wake gharama hizo kumepelekea kwa watoto hao kurudihswa nyumbani.
Sababu nyingine anayoitaja mama huyo ni upungufu wa chakula hasa watoto wanapokwenda asubuhi na kurudi shule mchana. Hali hii inasababisha watoto wasiende shule na kujikita katika shughuli za kuzalisha kwa ajili ya familia.
Pamoja na changamoto hizo, bado raia huyu mwamilifu alimshauri mama huyo kwenda kuonana na mwalimu mkuu ili aangalie ni kwa jinsi gani anaweza kusaidiwa ili watoto wake wahudhurie shuleni.
Ushauri huu unatokana na ukweli kwamba mwalimu mkuu wa shule hiyo Ramadhani Masatu naye pia ni raia mwamilifu kwa nafasi yake. Uwamilifu huo unaelezewa na mraghbishi Elizabeth Ngayalina, toka kijiji cha Nyandekwa:
“Mwalimu mkuu ni muelewa na ndio maana amekubali kushirikiana nasi. Ametupatia kwanza idadi ya wanafunzi ambao ni watoro kwa kuwa anajua ni jukumu letu sote si la kwake na walimu wenzake”  
Nikiwa katika picha ya  pamoja na Waraghbishi na Raia Waamilifu toka katika kijiji cha Nyandekwa wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano wao hapo kijijini

Kwa hakika raia hawa waamilifu toka katika vijiji vya Nyandekwa na Kilago wanahitaji kuungwa mkono na wadau wote wa maendeleo. Elimu ni haki ya msingi ya kila mtoto na ndio maana sera ya serikali ni kutoa bure elimu ya msingi na ile ya sekondari. Njia pekee ya kumkomboa mtoto ni kumpatia elimu ambayo ndio dira ya maendeleo ya kila nchi, kuwa na wasomi wengi kadri iwezekanavyo. 

No comments: