Wednesday, January 13, 2016

HAFLA YA KUMPONGEZA MBWANA SAMATTA


Kufuatia mchezaji Mbwana Samatta kushinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania  (TFF) lilikuwa limeandaa shughuli maalum ya kumpongeza, kumshukuru na kumtakia kheri katika taaluma yake ya uchezaji mpira.


Kama ilivyotangazwa hapo awali shughuli hii ilikuwa ifanyike kesho Alhamisi tarehe 14/01/2016 Makao Makuu ya TFF Uwanja wa Karume kuanzia saa 11 jioni.
Tarehe hii ilipangwa mahsusi ili kupisha shughuli za kitaifa za siku ya Mapinduzi tarehe 12/01/2016 na fainali ya Kombe la Mapinduzi tarehe 13/01/2016.
Kufuatia maandalizi ya Mbwana Samatta ya safari ya kuelekea Ulaya kukamilika hivyo mchezaji huyo siku ya Alhamisi hatoweza kuhudhuria shughuli hii na hivyo shughuli haitakuwepo tena.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaendelea tena kumpongeza Mbwana Samatta kwa mafanikio aliyoyapata na pia kumtaka huko aendako  aendelee kuwa  mfano mwema kwa vijana wote wa Tanzania.
TFF inamshukuru sana Mh Rais John Pombe Magufuli kwa salamu za pongezi alizozitoa kufuatia ushindi wa Mbwana, Wanafamilia wa Mpira wa Miguu tumefarijika sana kwa salam hizi.
Tunamshukuru sana Waziri Mkuu Mh Majaliwa Kassim Majaliwa kwa kumuandalia jana Mbwana Samatta hafla katika hoteli ya Hyatt na kwa kumpatia zawadi zikiwemo fedha taslim na kiwanja eneo la Kigamboni.
Tunamshukuru sana Mh Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni Sanaa na Michezo pamoja na viongozi wote wa Wizara kwa kujitolea kwao kushiriki katika shughuli mbalimbali za kumpokea na kumpongeza Mbwana Samatta.
Shukrani za pekee pia kwa wazazi wake Mbwana Samatta, pia familia na washauri wake.

No comments: