Saturday, January 30, 2016

MAMA YASSODA AFUNGA KOZI YA MAKOCHA WANAWAKE




Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mama Juliana Yassoda leo amefunga kozi ya ukocha wa wanawake ngazi ya juu (High Level Course) iliyoandaliwa na TFF kwa kushirikiana na FIFA.

Akiongea wakati wa kufunga kozi hiyo, Mama Yassoda amesema anaishukuru TFF/FIFA kwa kuona wanawake wanapata nafasi ya kushiriki kozi mbalimbali, ikiwemo kozi hiyo ya ukocha kwa ngazi ya juu kwa wanawake.
Mama Yassoda amewataka washiriki wa kozi hiyo kuyafanyia kazi mafunzo waliyopatiwa katika kuhamasisha wanawake wengi kuupenda mpira wa miguu na kuzalisha vipaji vya wachezaji wengi wa kike kuanzia ngazi za chini, na sio kuhitimu na kuweka vyeti ndani tu.


Naye Mariam Mchaina akiongea kwa niaba ya washiriki wenzake, ameishukuru TFF kwa kuwakumbuka wanawake na kuwapatia kozi hiyo ya ukocha, na kuahidi watakaporudi sehemu wanazoishi watatumia ujuzi walioupata kufundisha wanawake mpira miguu kwa ngazi zote.
Kozi hiyo ya ukocha kwa wanawake, ilianza Jumatatu na kumalizika leo ambapo jumla ya washiriki 25 wameshiriki kozi hiyo ya awali kutoka katika mikoa ya Dar es salaam, Iringa, Ruvuma, Pwani na Tanga na kupewa vyeti ya ushiriki na mpira kama kifaa cha kuanzia kazi ya ukocha.

No comments: