Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanznaia (TFF), Jamal Malinzi amempongeza Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete kwa kukubali uteuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) na GAVI utakaomfanya kuwa bingwa wa chanjo na balozi wa mradi wa Africa United Duniani.
“Familia ya mpira wa miguu inajua umuhimu wa chanjo na hasa katika maendeleo ya vipaji na wanamichezo kwa ujumla na jinisi chanjo inavyoweza kuwapa watoto siyo tu fursa ya maendeleo bali pia haki ya kuishi” ilisema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
Katika barua hiyo, Malinzi ameelezea furaha ya TFF kuona kiongozi wa Tanzania akiongoza mapambano ya kuokoa afya na uhai wa kizazi cha sasa na kijacho katika Afrika na dunia kwa ujumla.
“TFF itaunga mkono juhudi zako ili kufanikisha malengo yaliyowekwa na ushirika wa chanjo” ilimalizia barua hiyo ambayo nakala yake imetumwa kwa Rais wa Caf, Issa Hayatou.
No comments:
Post a Comment