Meneja Mawasiliano wa TPA, Bibi Janeth Ruzangi (kulia) akikabidhi vitanda 20, magorodo 20 na mashuka 100, vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 13 kwa hospitali ya Wilaya ya Kisarawe mwishoni mwa wiki. Anayekabidhiwa vifaa hivyo ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Bwana Hamis Likupotile (kushoto) na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dkt Elizabeth Oming'o. Makabidhiano hayo yaliyafanyika hospitali hapo.
Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Usimamizi wa
Bandari Tanzania (TPA) imetoa msaada wa Vitanda 20, Magodoro 20 na Shuka 100
kwa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani.
Vitanda hivyo vya kisasa aina
ya ‘Cardiac’, mashuka pamoja na magodoro yake vilivyokabidhiwa katika hospitali
hiyo ya wilaya vina thamani ya shilingi za kitanzania milioni 13.
Akizungumza wakati wa kukabidhi
vifaa hivyo, Meneja Mawasiliano wa TPA, Bibi Janeth Ruzangi alisema msaada huo
ni sehemu ya wajibu wa Mamlaka kuisaidia jamii ya Watanzania.
“Pamoja na shughuli zake za
kupakua na kupakia mizigo, Mamlaka pia ina wajibu wa kurudisha kile
inachokipata kutokana na huduma zake kwa kuisaidia jamii na ndio maana leo hii
tumekuja kutekeleza wajibu huo,” alisema Ruzangi.
Bibi Ruzangi alisema pamoja
na kwamba msaada huo ni mdogo lakini wana imani utasaidia kupunguza changamoto
za uhaba wa vitanda katika hospitali hiyo ya wilaya.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu
wa Hospitali hiyo, Dkt Elizabeth Oming’o hospitali hiyo ina uhaba wa vitanda 94
na mashuka 1,200.
“Hiki kilicholetwa na
Mamlaka ya Bandari ni zaidi ya msaada kwani vitanda hivi ni vya kisasa na ni
vya gharama sana,” alisema Dkt Oming’o.
Dkt Oming’o alisema kwamba
wanashukuru sababu msaada huo utaenda kupunguza pengo la uhaba wa vitanda na
mashuka walilonalo hospitalini hapo.
Alisema kwamba mbali ya
vitanda na mashuka hayo, pia wana changamoto ya vitanda vya upasuaji. Vilivyopo
sasa katika hospitali hiyo vimechakaa na hivyo havikidhi mahitaji yao.
Akizungumzia vitanda
walivyokabidhiwa na TPA, Dkt Oming’o alisema ‘Cardiac bed’ ni vitanda vya
kisasa kabisa ambavyo hospitali hiyo ilikuwa haina.
“Vitanda hivi ni gharama
sana kiasi kwamba kama tungeamua kwenda kuvinunua kwa pesa yetu, hakika
tusingeweza,” alisema.
Alisema wamefarijika na ujio
wa vitanda hivyo kwani vitarahisisha kazi zao kwa kiasi kikubwa.
Naye Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya hiyo Bw. Hamis Likupotile alisema wanaishukuru Mamlaka
kwa msaada huo kwani hospitali yao ina upungufu mkubwa wa vitanda.
Vitanda hivi 20 na magodoro
yake pamoja na mashuka ni msaada mkubwa kwetu kwani umesaidia kutatua tatizo
sugu la uhaba wa vitanda katika hospitali hiyo.
Alisema kwamba changamoto
walizo nazo ni nyingi na walishapeleka maombi sehemu mbalimbali ili wasaidiwe
lakini kote bado hawajibiwa.
“Kwa kweli tunawashukuru
sana TPA kwani katika mashirika yote tuliyoomba, bandari ndio wamekuwa wa
kwanza kutujibu na kutusaidia kwa wakati,” alisema.
Hospital hiyo kwa sasa
imekuwa chombo muhimu si kwa Kisarawe tu bali hata kwa wananchi wa mikoa jirani
kwani kwasasa wanahudumia watu wengi sana kutoka Gongo la Mboto, Pugu na
Mbagala.
Kwahiyo alisema msaada huo
umesaidia jamii kubwa ya watanzania na si Kisarawe pekee, hivyo kuiomba Mamlaka
iendelee kuwasaidia vifaa tiba vingine, kwani ujio wa wagonjwa wengi pia huleta
changamoto nyingi.
|
No comments:
Post a Comment