Charles Kuyeko, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala (Ukawa) (Wakwanza), Edward Lowassa, aliyekuwa Mgombea Urais kwa tiketi ya Ukawa na Boniface Jacob, Meya wa Halmashauri ya Kinondoni (Ukawa) |
KISIRANI cha viongozi wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushindwa kwenye uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam kinaendelea, anaandika Happyness Lidwino.Sasa hivi CCM na viongozi wake wanatajwa kuwa na mkakati wa kupoka vyanzo vyote vikuu vya mapato katika Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam na kuvibinafsisha kwa taasisi za serikali.
Hata hivyo, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimeeleza kutorudi nyuma katika harakati za kuwasaidia wananchi licha ya vitimbi vya CCM.
Charles Kuyeko, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala amesema hayo leo jijini humo wakatika akizungumza na Umoja wa Madereva Tax Ilala (UMATAWI).
Kuyeko amesema, CCM ina mpango wa kupoka vyanzo vya mapato na kwamba, jambo hili linafanywa chini kwa chini na mpaka sasa bado halijawekwa wazi.
“Hizo ndizo taarifa zilizopo japo bado hazijaletwa rasmi. Kwa hatua hiyo waliyofikia ni kiashiria cha chuki baina ya chama cha upinzani ambacho kinashikilia jiji hili, kitu ambacho hawakukitarajia,” amesema Kuyeko na kuongeza;
“Zipo taarifa kwamba serikali itachukua vyonzo vikubwa vya mapato kama ushuru wa mabango na kodi za majengo katika manispaa zote ambazo zitakuwa zikikusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na taasisi nyingine zilizochini yake.”
Amesema, mpango huo ni wa kukomoa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) Dar es Salaam kwa kuwa ndio wanaosimamia jiji hilo.
“CCM ina lengo la kutugombanisha na wananchi wetu ambao tumewaahidi kuwatumikia vema ili watuone hatuwezi majukumu yetu. Niwaambie wananchi kwamba, hata kama wakichukua vyanzo vya mapato na kukusanya kodi wao, hatutarudi nyuma.
“Katika jiji hili hakutakuwa na maendeleo kama hatutashirikiana pasipo kujali itikadi za vyama. Na shanganzwa na viongozi wakubwa wa nchi wanafanya kazi kwa ubaguzi wakati lengo ni moja la kuwatumikia wananchi. Nyumba ni moja ya nini kugombea boliti?” amehoji Kuyeko.
Hata hivyo, katika mkutano huo ambao UMATAWI walipeleka changamoto zao zilizodumu kwa muda mrefu, ikiwemo ya utaratibu wa ulipaji kodi na kuwaondoa madereva ya taxi zisizosajiliwa, Kuyeko amewaahidi kutatua kero zao huku akiwahimiza kulipa kodi kwa hiari.
Hamisi Kivugo, Katibu Mkuu wa UMATAWI baada ya kuwasilisha changamoto za umoja huo amesema, “tangu wilaya hii (Ilala) ianzishwe hatujawahi kupata fursa ya kuongea na meya moja kwa moja na kutoa changamoto zetu.”
Amesema, wamefurahishwa na utendaji wa Meya Kuyeko na kwamba watampa ushirikiano katika ukusanyaji wa mapoto kwa hiyari.
No comments:
Post a Comment