Friday, May 13, 2016

PICHA CHAFU MITANDAONI ZALAANIWA NA WANAHARAKATI LEO

Na Exaud Mtei
Kufwatia kukithiri kwa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii nchini Tanzania hususani mwasala ya ukiukwaji wa haki za binadamu,urushwaji wa picha mbaya, na chafu hatimaye mashirika ya kutetea haki hizo yameibuka na kuitaka serikali kuacha kufumbia macho vitendo hivyo na kuwachukulia hatua kali watu wanaosambaza picha mitandaoni kwa kuwa wanavunja haki za binadamu nchini.
Mkurugenzi Mtendaaji wa kituo cha sheria na haki za Binadamu Nchini Tanzania LHRC Bi HELLEN KIJO BISIMBA akizungumza na wanahabari mapema leo
Leo asubuhi mashirika yanayotetea haki za binadamu hususani zile zinazohusu
 makundi maalum kama watoto na wanawake wamekutana na wanahabari kulaani vikali baadhi ya matukio mabaya yanayoendelea katika mitandao ya kijamii na kuiaka serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti hali hiyo kwani inakwenda kinyume na sheria mbalimbali ikiwemo sheria ya mtandao.

Bi HELLEN KIJO BISIMBA ni Mkurugenzi mtendaji wa kituo cha sheria na haki za binadamu nchini LHRC ambao waliyaongoza mashirika hayo katika kutoa tamko hilo ambapo ameeleza kuwa katika kipindi cha karibuni kumekuwa na wimbi kubwa katika jamii kusambaza na kutumiana picha za watu waliofanyiwa ukatili,au waliopata ajali zikionyesha majeraha,au hata maiti za watu hao na zile ambazo zinaonyesha ukatili dhidi ya wanawake na watoto huku serikali ikiwa haifwatilii swala hilo.
Akitolea mfano baadhi ya matukio ambayo yamesukuma mashirika hayo kutolea tamko ni pamoja na picha zilizokuwa zikimwonyesha mama na mtoto waliochinjwa huko bagamoyo ,picha za mtoto aliyeuawa na mama wa kambo mkoani Kilimanjaro,picha za mwanamke aliyesemekana kuwa ni msukule aliyekutwa kwenye kisima huko kibamba,pamoja na picha nyingi kama hizo ambazo amesema zimekuwa zikikiuka maadili ya mtanzania na utu wa makundi hayo.

Ameeleza kuwa serikali ya Tanzania imekuwa ikiwakamata na kuwafwatilia wale ambao wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuitukana serikali au viongozi wa serikali huku wakisahau kuwa sheria ya mtandao inakataza pia urushwaji wa picha chafu katika mitandao hiyo.

Bi HELLEN ameongeza kwa kuitaka jamii kuacha kuendelea kuwavunjia haki makundi hayo hasa pale ambapo haki yao imeshavunjwa na itambue utu wa makundi hayo kwa kuwa usambazaji wa picha hizo unamuathiri muhusika pamoja na ndugu na marafiki wa mhusika.

Nchi ya Tanzania ni moja kati ya nchi barani afrika ambayo inakuja kwa kasi katika katumizi ya mitandao ya kijamii kwa wananchi wake ambapo wananchi wake wamekuwa wakitumia mitandao hiyo kinyume na matumizi halali,ikiwemo utumwaji wa picha za matukio mabaya,na picha zilizokosa maadili.

Mashirika zaidi ya tisa likiwemo LHRC,TAWLA,TAMWA,TWCWC,WILDAF,CWCA,AFNET,na NAFGEM wameungana kwa pamoja kulaani vitendo hivyo leo Jijini Dar es salaam

No comments: