Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi
ameipongeza timu ya soka ya Young Africans kwa kutwaa ubingwa wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufanya
hivyo msimu uliopita wa mwaka 2014/2015.
Hii ni mara ya 26 kwa Young Africans ambayo kwa sasa inacheza
mashindano ya kuwania kutwaa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kutwaa
taji hilo tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1965. Simba
inafuatia katika rekodi hiyo baada ya kulitwaa taji hilo kwa mara 18.
“Nichukue nafasi hii kuipongeza Young Africans kwa ubingwa. Pia
nizipongeze timu zote za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kushiriki na kufanya
msimu wa Ligi Kuu Bara ya Vodacom 2015/16 kuwa wenye mafanikio,”
amesema Rais Malinzi baada ya Young Africans kufikisha pointi 71 ambaz
o haziwezi kufikiwa na timu nyingine 15 zilizoshiriki ligi hiyo.
Kadhalika Rais Malinzi amezikumbusha na kuhamamisha klabu
zitakazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2016/17 kutoa maoni,
mapendekezo, marekebisho ya ili kuboresha kanuni za uendeshaji wa ligi
hiyo kwa msimu ujao. Maoni hayo yapelekwe kwa njia ya maandishi moja kwa
moja kwenye ofisi za Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) au kwa njia
ya barua pepe tplb.tplb@yahoo.com
Young Africans imefikia rekodi hiyo baada ya kutwaa ubingwa katika
miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987,
1989, 1991, 1992,1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006 na misimu ya
2007-2008, 2008-2009, 2010-2011, 2012-2013, 2014-15 na 2015-16.
Pamoja na kutangazwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa
2015/2016, kikosi cha timu ya Young Africans kwa sasa kimebakiza michezo
miwili ambayo ni dhidi ya Ndanda unaotarajiwa kupigwa Jumamosi Mei 14,
2016 kadhalika dhidi ya Majimaji Mei 22 ambayo itakuwa ni siku ya
kufunga pazia la Ligi Kuu msimu huu wa 2015/16.
No comments:
Post a Comment