Sunday, June 12, 2016

MALINZI AMPONGEZA MANJI, YANGA




Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amempongeza Yussuf Manji kwa kuchaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Young Africans SC baada ya kupata kura 1,468 kati ya 1,470 zilizopigwa. Kura mbili ziliharibika kwa nafasi hiyo.

Kadhalika Rais Jamal Malinzi amempongeza Clement Sanga kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti  baada ya kupata kura 1,428 wakati mpinzani wake Titus Osoro alipata kura 80. Kura 1,508 zilipigwa katika nafasi ya kuwania makamu mwenyekiti.

Kadhalika wajumbe wanane wanaounda Kamati ya Utendaji kwa kuchaguliwa kuongoza Klabu ya Young Africans kwa miaka minne ijayo kwa mujibu wa katiba.
Wajumbe waliochaguliwa ni Omary Said (1,069), Siza Lyimo (1,027), Salum Mkemi (894), Thobius Lingalangala (889), Ayoub Nyenzi ((889), Samwel Lukumay (818), Hussein Nyika (770) na Hashim Abdallah (727.

Katika salamu hizo za pongezi, Rais Jamal Malinzi pia amewapongeza wanachama wa Young Africans kwa kufanya uchaguzi wa amani na utulivu.

Kutokana na hali hiyo, Rais Jamal Malinzi amewataka uongozi huo wa Young Africans kufungua ukurasa mpya wa kuendesha klabu hiyo na kuiletea mafanikio klabu hiyo kongwe na maarufu katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati hasa wakati huu ambako Young Africans inashiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC).

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments: