MKAKATI wa kuteka nchi unapangwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),anaandika Happiness Lidwino.
Ni kwa kufanya ziara nchi nzima kwa lengo la kukukumbusha wananchi kwamba, nchi inapaswa kuendeshwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri.
Kumekuwepo na malalamiko kwamba, Rais John Magufuli anaendesha nchi kinyume na taratibu pia Katiba ya Nchi na kwamba, ziara hiyo imepangwa ili kuzindua wananchi wajibu wa kudai viongozi waongoze kwa mujibu wa Katiba ya Nchi.
Ziara hiyo imepangwa kuanza kutekelezwa tarehe 7 Juni mwaka huu. Ziara hiyo itaanzia mkoani Shinyanga, Wilaya ya Kahama.
Baada ya hapo kutakuwa na timu mbili zitakazozunguka katika mikoa yote nchini ikiwemo ya Chato, Bukoba, Geita, Sengerema, Muleba, Meatu, Bunda, Bariadi na kumalizika Mwanza ambapo timu hizo mbili zitakutana.
Akizungumza na waandishi leo Jijini Dar es Salaam Mkurungenzi wa Oganezesheni na Mafunzo wa CHADEMA, Kigaila Benson amesema, timu hizo mbili pia zitafika katika nyanda zote nchini zikiongozwa na viongozi wote wa chama pamoja na wajumbe wa kamati kuu ya chama na kisha ziara hiyo kumalizikia Dar es Salaam.
Benson amesema, kwa kuwa Chadema ni chama kikubwa cha upinzani kina haki ya kufanya ziara hiyo ya kuwafumbua macho na kuwaelimisha wananchi juu ya uongozi anaodai wa kidikteta unaofanywa na Rais Magufuli.
“Tangu kuingia madarakani Rais Magufuli kumekuwa na ukiukwaji wa sheria na katiba, serikali imekuwa ya mtu mmoja na maamuzi ya mtu mmoja kana kwamba, hakuna wizara husika kitu ambacho kinawakandamiza wananchi na kushindwa kupata haki zao,” amesema.
“Hatuta choka kupiga kelele anapoenda kinyume na kupuuza Katiba ya nchi na tunataka wananchi wa mtambue na wajue namna ya kudai haki zao. Tangu kuingia kwake madarakani hakuna maendeleo zaidi ya kulipiza visasi kwa watu ambao hawakumuunga mkono wakati wa kampeni.
“Rais Magufuli amevunja na kuvuruga vitu vingi vilivyopo kwenye Katiba ikiwepo sikukuu, kupanga matumizi ya fedha wakati wizara husika zipo, uvurugaji wa bunge na mengine mengi yasiyomuhusu,” amesema.
Aidha Benson amesema kuwa, wananchi nchini wajiandae kupewa elimu ya utambuzi na kuanza kuchukua hatua juu ya utendaji wa mtu waliyempa dhamana ya kuwaongoza. Pia amesema tayari wameshatoa taarifa katika vyombo vya usalama na hivyo wananchi wasiwe na shaka
No comments:
Post a Comment