Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) akimkabidhi Mbwana Samatta (kushoto) zawadi ya kitabu kinachozungumza utalii wa Tanzania na Tanzania kwa ujumla.
Mbwana Samatta (kulia) akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo baina yake na Menejimenti ya Bodi ya Utalii Tanzania katika ofisi za Bodi hiyo jijini Dar es salaam leo.
Mbwana Samatta (katikati) katika picha ya pamoja na wajumbe wa Menejimenti ya TTB wakiongozwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi hiyo Bi Devota Mdachi.
……………………………………………………………………………………………
Na: Geofrey Tengeneza
Mchezaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Ally Samatta (23) anayecheza kandanda la kulipwa katika klabu ya Genk nchini Ubelgiji amekubali ombi la Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuwa Balozi wa hiari wa Tanzania na kusaidia kuitangaza Tanzania kama eneo la Utalii nchini Ubelgiji na Ulaya kwa ujumla.
Samatta ametoa ahadi hiyo leo alipotembelea ofisi za Bodi ya Utalii jijini Dar es salaam na kuwa na mazungumzo na Menejimenti ya Bodi hiyo kuhusu kumtumia katika kutangaza vivutio vya utalii na Tanzania kimataifa.
“ Kama mtanzania ninawiwa kwa nchi yangu hivyo nina furaha na niko tayari kitangaza nchi yangu kama eneo la utalii popote nitakapokuwa” alisema. Aliongeza kwamba nchi nyingi duniani hutumia watu wao maarufu ikiwa ni pamoja na wachezaji wa kimataifa kuzitangaza nchi zao.Ameipongeza Bodi TTB kwa mkakati wa kuwatumia watanzania mbalimbali maarufu katika kuitangaza Tanzania akaahidi kufanya kila litakalowezekana ikiwemo kutumia mitandao yake ya kijamii kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya utalii.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania Bi Devota mdachi amedokeza kuwa TTB itatazama namna nzuri kabisa ya kumtumia Mbwana Samatta kutangaza utalii wa Tanzania na Tanzania kwa ujumla kama eneo zuri kwa utalii.
Mbwana Samatta amesaini mkataba wa kuichezea klabu ya Genk ya Ubelgiji utakaomalizika mwaka 2020. Sammata ambaye ni Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania Taifa star, alitwaa tuzo ya mchezaji bora Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani ya Afrika.
No comments:
Post a Comment