Kampuni ya Tigo Tanzania imeshiriki katika kumbukumbu ya Siku ya Mtoto wa Afrika 2016 kwa kuchangia zaidi ya shilingi 26.4m/-($12,000) kwa asasi isiyo ya kiserikali ya C-Sema ambayo inaendesha kituo cha kupokelea simu cha Huduma ya Simu kwa Mtoto (Child Helpline Call Centre) mjini Zanzibar ambacho kinatoa ushauri na kuwaunganisha watoto kupata huduma sahihi za kijamii kikishirikiana na serikali.
Tigo na asasi ya C-Sema watafanya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu katika Kituo cha Michezo cha JMK Park jijini Dar es Salaam Alhamisi Juni 16. Siku ya Mtoto wa Afrika ni tukio linalofanyika duniani kote kila Juni 16 ya kila mwaka.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Meneja wa Huduma za Jamii wa Tigo, Woinde Shisael alisema msaada huo ni sehemu ya mkakati wa kampuni wa kuwekeza katika ajenda ya kumlinda mtoto iwe kwa njia ya mtandao na hata nje ya mtandao.
Akitoa shukrani kutokana na msaada, huo Ofisa Mtendaji Mkuu wa C-Sema, Kiiya JK aliishukuru kampuni hiyo ya simu kwa kutoa mchango sahihi katika kuwekeza rasilimali zake ili kuhakikisha kwamba watoto na wazazi wanakuwa na uhakika wa kupata jukwaa ambalo wanaweza kutoa taarifa kuhusu aina yoyote ya ukatili dhidi yao.
“Ninaishukuru Tigo kwa msaada huu wakati leo tunasherehekea watoto wa Afrika kwa kuzisikiliza sauti zao wakati wakitueleza kile wanachokifikiria kuhusu masuala mbalimbali yanayowasibu na nini kitu gani kifanyike kutokomeza matendo mabaya ambayo yanaweza kukwamisha maendeleo yao.”
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Nape Nnauye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio la mwaka huu la Siku ya Mtoto wa Afrika.
Kituo cha taifa cha kupokelea simu za huduma ya simu kwa mtoto (Child Helpline call centre) kilianzishwa rasmi Juni 15, 2013 kikiwa na kituo cha Dar es Salaam na Zanzibar.
No comments:
Post a Comment