Monday, June 20, 2016

Wananchi wa Kata ya Nanyanga kwa kushirikiana na mbunge wa jimbo la Tandahimba,Katani katani waanzisha ujenzi wa zahanati.

Mbunge wa jimbo la Tandahimba,Katani Katani akishirikiana na wakazi wa kata ya Nanyanga wilayani humo kuchimba msingi kwaajili ya kuanzisha zahanati.Mbunge huyo amechangia mifuko 400 ya saruji na wananchi walichangia Sh 10 kwa kila kilo moja ya korosho baada ya kuridhiana. (Picha zote na Haika Kimaro)
Tandahimba.Tatizo la wakazi wa kata ya Nanyanga na vijiji vya kata za jirani kutembea umbali wa kilometa 15 kutafuta huduma za afya huenda likapungua ama kumalizika baada ya wananchi wa Kata ya Nanyanga kwa kushirikiana na mbunge wa jimbo la Tandahimba,Katani katani kuanzisha ujenzi wa zahanati.


Akizungumza mkazi wa kata hiyo, Mwajuma Liumbe alisemujenzi wa zahanati hiyo utawapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta hospitali ya wilaya ama kujifungulia kwenye chumba kimoja walichokuwa wakichanganyw na wanaume.


 "Tuna furaha kubwa kuanza kwa ujenzi wa zahanati hii kwasababu tulikuwa tunateseka sana hasa  jinsi ya kujifungua zahanati ya jirani kwasababu tulikuwa wanawake na wanaume tunalala hapo hapo na ni mbali kufika ilipo, "alisema Liumbe


 Diwani wa kata hiyo,Mbombenga Mawazo alisema baada ya kuonekana kata hiyo na kata za jirani hazina vituo vya afya alipeleka wazo kwenye vikao vya halmashauri ambapo walikubaliana kuhamasisha wakulima wa korosho kuchangia Sh 5 kwa kila kilo moja ya korosho ili kuanzisha zahanati.


 Alisema baada ya wakulima wa kata hiyo  kuridhia zilipatikana 17.7milioni ambapo 5milioni zilipelekwa shule za sekondari na nyingine kununua eneo la hekari 14 kwa gharama ya 14.2 milioni kwaajili ujenzi wa zahanati.

"Nilipeleka wazo kwenye vikao vya halmashauri na viliridhia ambapo kila mkulima alikatwa Sh 5 kwa kila kilo na kupatikana 17.7 milioni na mbunge wetu alichangia mifuko 400 ya saruji ambayo imeweza kufyatua matofali na wafanyabiashara walichangia kiasi kuongezea pesa ya kununua eneo, "alisema Mawazo


Mbunge wa jimbo hilo, Katani Katani alisema katika bajeti ya mwakani watalipa suala la afya kipaumbele na kuwashirikisha wananchi kuona ni kwa namna gani wataboresha sekta ya afya.


"Bajeti ya mwakani kwenye halmashauri tutawekeza kwenye afya na tutawashirikisha wananchi kuona namna ya kuboresha sekta ya afya kwa kuchangia wenyewe walau tuone Tandahimba inakuwa ya kwanza kuwa na huduma bora za afya kwa Tanzania,"alisema Katani


Hata hivyo Katani alikabidhi mifuko mingine 100 ya saruji kwaajili ya ukarabati wa soko la Tandahimba ikiwa ni mwendelezo wa kutekeleza ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni

No comments: