Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Ziwa kimetangaza kufanya maandamano katika kanda hiyo huku wakidai kuyafungia katika mji wa Chato ambao ni nyumbani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli.
Tamko la Chadema limetolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho Kanda ya Ziwa Magharibi, Meshack Micus alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake.
“Sisi kama Chadema kanda ya Ziwa hasa kanda ya Victoria tayari tumeshawaelekeza wanachama wetu wote, viongozi wetu wote na tayari mwitikio ni mzuri. Na hadi leo tayari viongozi wetu wa vitongoji 1973 wameshajiandaa wako tayari kwa ajili ya kufanya maandamano na kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao,” alisema.
“Tutaandaa maandamano kutokea Kyelwa, tutaelekea Misenyo, Bukoba vijijini na tutakuja moja kwa moja mpaka Chato. Na wa Mwanza tayari nimeshawaagiza kwamba maandamano yetu tunaenda kuyafungia Chato,” aliongeza.
Tamko hilo limekuja ikiwa ni siku moja baada ya Rais John Magufuli kuwaonya Chadema kutomjaribu kwa kufanya maandamano bila kufuata utaratibu kwani hatawavumilia.
Rais Magufuli aliwataka wananchi kutokubali kudanganyika na kufanya maandamano na badala yake wajikite katika kufanya kazi itakayowaletea maendeleo.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza kile walichokiita ‘Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (UKUTA)’, akiwaalika wafuasi wake kufanya maandamano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi mwaka huu.
No comments:
Post a Comment