Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla amefanya ziara ya ghafla katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufuatia taarifa zilizoripotiwa kwenye mitandao ya Kijamii na baadhi ya Magazeti ya hapa Nchini juu ya kutelekezwa bila kupatiwa huduma kwa mgonjwa wa Sickle Cell (Selimundu) na Madaktari na manesi wa Hospitali hiyo.
Dk. Kigwangalla ameweza kufika kwenye Hospitali hiyo ya Muhimbili na kisha kwenda moja kwa moja kwa mgonjwa huyo ambaye awali picha yake ilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii na ujumbe wa kutelekezwa iliyosambazwa na Wanaharakati wa Sickle Cell ambao waliomba Serikali ichukue hatua. (Kama walivyoandika kawenye ujumbe hapa chini).
Hata hivyo, Dk. Kigwangalla baada ya kujionea hali halisi ya tukio la mgonjwa huyo kupitia mitandao na magazeti aliamua kutembelea mwenyewe katika wodi ya magonjwa ya damu (Haematology) huku akiomba kuoitia nyaraka zake zote pamoja na kupatiwa taarifa za kutelekezwa mgonjwa huyo kama ilivyoripotiwa ambapo hata hivyo hali ilikuwa ni tofauti na ilivyoripotiwa.
“Nimekuja mwenyewe na wala sikutaka kutuma wasaidizi wangu. Nimemtembelea Mgonjwa ‘KK ‘ na kukuta hajatelekezwa wala kunyanyaswa. Hajalazwa chini. Ameonwa na jopo la Madaktari bingwa lililoongozwa na Dk. Stella, kwa siku mbili mfululizo tokea alipowasili wodini.
Mgonjwa alilazwa juzi. Ni kweli anaumwa Sickle Cell, yupo kwenye 'painful crisis', lakini amepewa Antipains zote anazopaswa kupewa ikiwemo kali kabisa ya aina ya 'Morphine'! Mgonjwa hana malalamiko. Mwanzoni hakujua mimi ni nani na nilikuwa peke yangu na hivyo hakuogopa kunipa taarifa yoyote ile. Pia nimekagua faili lake neno Kwa neno, nimeridhika ametibiwa ipasavyo.
Kuzusha taarifa za uongo, kutafuta 'sympathy' (huruma) Kwa kusingizia watu kunakatisha tamaa, Hivyo naagiza Hospitali zote nchini kudhibiti wageni kupiga picha wodini hii ni pamoja na kuzuia simu zote za camera kuingizwa mawodini pamoja na camera za aina yoyote ile na kwa atakayekihuka kuna sheria na kanuni zitafanya kazi” alieleza Dk. Kigwangalla.
Kwa upande wake mgonjwa huyo Mwanadada, K. Kasongo ambaye alikiri kufika hapo siku tatu zilizopita na kupokelewa vizuri na wahudumu pamoja na Madaktari ambapo na kupatiwa huduma stahiki.
Kwa hali hiyo, Dk. Kigwangalla aliomba jamii kuacha kuripoti mambo wasiyo yajua kwani yanaweza kuchangia upotevu wa amani.
“Nilisononeka sana awali wakati nimepata habari hizi. Bahati mbaya nilikuwa Jimboni, sikuwa na namna ya kufanya zaidi ya kurudi Ofisini kisha kufuatilia. Niliyoyakuta hayafanani hata chembe na kilichoandikwa hapa na wanaharakati hawa wa Sickle Cell (selimundu). Wakati tukihangaika kuboresha huduma za Afya nchini Kwa ajili ya watu wote, Wakati tukifanya kazi Kwa bidii zote, usiku na mchana, masaa ya ziada, Kila kona ya nchi, kutwa kucha barabarani, unakutana na watu wa aina hii, wanapotosha umma, wanaotafuta umaarufu wa taasisi yao kwa kutoa taarifa za uongo kwa umma juu ya mambo wasiyoyajua. Alieleza Dk. Kigwangalla.
Aidha, aliongeza kuwa: kutokana na hali hiyo ambayo imeonekana kukatisha sana tama, ametoa rai kwa Wanaharakati kutambua kuwa Serikali imewekwa madarakani na wananchi kwa kura na Kwa Msingi huo ina imani na Matumaini kamili ya wananchi, Na pia ina uchungu na huruma kwa wananchi walioipa mamlaka na si vinginevyo.
Na kwamba, hata siku moja wanaharakati wasidhani wanaweza kuwa mbadala kamili wa Serikali, wao ni wabia muhimu na wanaisaidia Serikali kuutumikia umma (complementary efforts) na Siyo mbadala (alternative) wa Serikali. Kama wabia wakuu wa Serikali, wanaharakati wana wajibu wa kusema ukweli bila kuegemea upande wowote ule ili kulinda heshima yao na kulinda 'relevance' yao kwenye mfumo wa uongozi na utawala wa nchi.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwasili Hospitali ya Muhimbili Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla akipitia faili za mgonjwa huyo
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwaeleza wanahabari juu ya hatua ya tukio hilo baada ya kutembelea na kujiridhisha. (Picha zote na Andrew Chale,Modewjiblog).
No comments:
Post a Comment