Saturday, August 27, 2016

MKUU WA WILAYA TEMEKE APIGA MARUFUKU GEREJI BUBU,APONGEZA WANAJESHI KUFANYA USAFI MITAANI

Kufuatia matukio yakutishia amani yanayo endelea nchini ikiwemo tukio la kuuawa kwa askari wanne katika Benki CRDB Tawi la Mbande Jijini Dar es Salaam, limempelekea Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva kuamua kupiga Marufuku uwepo wa Gereji Bubu.

Akizungumza na wakazi wa Mbagala ikiwa ni siku ya usafi inayofanyika kila jumamosi ya mwisho wa mwezi, Mkuu wa wilaya huyo ameeleza kuwa sio kwamba hapendi uwepo wa gereji ila anahitaji ziwepo katika utaratibu maalum kwa kusajiliwa na kutambulika, kwani hofu yake zinaweza kutumika kuhifadhia wahalifu ambao baadae wanaleta athari kwa taifa.

Pia Mkuu wa wilaya huyo Lyaniva amepongeza uwepo wa wanajeshi katika zoezi la usafi na kushirikiana na wakazi wa Mbagala, ambapo Mkuu wa Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi (GOC), Brigedia Jenerali Dominic Basil ameeleza kuwa ushiriki wa wanajeshi katika usafi ni moja ya shughuli wanazozifanya kuelekea kilele cha miaka 52 ya Majeshi nchini inayotaraji kufanyika Septemba Moja,ambapo hufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kuhamasisha wengine kushiriki zoezi la usafi kwani ni la kila mmoja.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Hashimu Komba ameahidi kuendelea kuhamasisha suala la usafi na kuwachukulia hatua wale watakao kaidi, kwani anaamini Temeke Mpya inawezekana, huku Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Nassib Mbaga akiwataka wafanya biashara kuacha kuuza chakula juu ya Mitaro ya Maji kwani ni hatari kwa afya inaweza sababisha mlipuko wa magonjwa, na kuahidi kukutana na wafanyabiashara hao kujua kero zao na namna ya kuzitatua.

No comments: