Wednesday, October 26, 2016

BABA AMUUA MTOTO WAKE KWA KUMCHOMA KISU KISA KAFUNGUA RADIO KWA SAUTI YA JUU

BABA mmoja mkazi wa Kijiji cha Maji ya Moto, Wilaya ya Arumeru mkoani hapa, Wilfred Kivuyo amemuua mtoto wake baada ya kumchoma kisu tumboni, kwa kosa la kufungulia redio kwa sauti ya juu.


Kabla ya tukio hilo inadaiwa yalitokea mabishano ya kugombea kupunguza sauti ya redio kati ya baba na mtoto, ambapo baba aliamua kumchoma kisu tumboni mtoto wake na utumbo kutoka nje. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema, tukio hilo lilitokea Oktoba 23, mwaka huu saa tatu usiku katika Kijiji cha Maji Moto na kumtaja marehemu kuwa ni Abraham Wilfred (22), ambaye kabla ya mauti alikuwa nyumbani akiendelea na shughuli zake huku akiwa amefungulia redio. 

Alisema siku ya tukio mtuhumiwa huyo alifika nyumbani akiwa amelewa na kumkuta mtoto wake amefungulia redio kwa sauti ya juu, ambapo alimtaka kupunguza sauti hiyo lakini mtoto huyo aligoma. 

“Baada ya hapo mabishano na kutoelewana kulijitokeza baina yao wakaanza kupigana, baba alipozidiwa nguvu na mtoto wake alichomoa kisu cha kukunja kwenye mfuko wa suruali kisha akamchoma tumboni na kumsababisha utumbo kutoka nje. 


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo

“Mara baada ya tukio hilo mtoto huyo alichukuliwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu, lakini hata hivyo alifariki wakati madaktari wakiendelea kuokoa maisha yake,” alisema Kamanda Mkumbo. 

Kamanda Mkumbo alisema Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka mtuhumiwa huyo ambaye baada ya tukio alikimbia ili hatua zaidi za kisheria zisichukuliwe dhidi yake. 

Na ELIYA MBONEA-MTANZANIA ARUSHA

No comments: