HATUA ya Mahakama ya Rufaa, Kanda ya Tabora
kutupilia mbali maombi ya kufutwa rufaa ya Davidi Kafulila iliyowasilishwa na
mawakili wa Hasna Mwilima, Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jimbo la Kigoma
Kusini, inainua matumaini mapya kwa mdai, anaandika Pendo
Omary.
Mdai katika kesi hiyo ya uchaguzi mkuu wa
mwaka jana ya kupinga matokeo kwenye jimbo hilo yaliyotangazwa kumpa ushindi
Mwilima ni Kafulila. Kafulila alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka mitano
(2010-15).
Swali linaliobuka hapo ni je, uamuzi huo
unaweza kuwa hatua nzuri kwa Kafulila (NCCR-Mageuzi) kufikia malengo yake ya
kutangazwa mshindi kama anavyoiomba mahakama kutokana na ushahidi wake ambao
tayari ameuwasilisha?
Mahakama hiyo kupitia Majaji Luanda, Mbarouk
na Mziray tarehe 12 mwezi huu walitengua hati iliyowasilishwa na
mawakili wa serikali ya kuitaka mahakama hiyo kufuta rufaa iliyofunguliwa na
Kafulila dhidi ya Mwilima kwamba, hati hiyo ilikuwa na kasoro za kiufundi.
Majaji hao kwa pamoja waliamua kwamba,
Kafulila anaweza kurejesha rufaa hiyo baada ya kurekebisha kasoro tajwa kwa
hoja kuwa, mahakama haiwezi kuifuta moja kwa moja wakati haijafikia kusikiliza
hoja za msingi wa rufaa yenyewe.
“Kufuatia uamuzi huo niliiomba mahakama
kurekebisha kasoro hizo ili kesi ya msingi isikilizwe kuamua nani aliyeshinda
uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Kusini mwaka 2015 kwa mujibu wa fomu za matokeo 21B
ambazo ingawa ziliwasilishwa na tume ya mahakama huku kila upande ukidai
umeshinda.
“Lakini Jaji anayesikiliza shauri hili ngazi
ya Mahakama Kuu, Jaji Wambali ambaye siku chache baada ya hukumu hiyo
aliteuliwa kuwa jaji kiongozi, alikataa fomu hizo kuhesabiwa ili kuamua mvutano
huo,” amesema Kafulila kwenye mahojiano na MwanaHALISI Online leo.
Kutokana na hatua ya Kafulila kufikisha maombi
ya kutaka kesi ngazi ya rufaa iendelee, mahakama leo imeagiza pande husika za
kesi kufika mbele ya Jaji Mrangu tarehe 3 Novemba, 2016 Tabora kwa ajili ya
ombi hilo lilowasilishwa na Kafulila ili rufaa iweze kuendelea.
Kafulila aliamua kwenda mahakamani kwa lengo
la kutafuta haki yake baada ya kutoridhishwa na matokeo ya kushindwa na kwamba,
matokeo yaliyotangazwa katika nafasi hiyo jimboni kwake ni tofauti na yale
aliyonayo ya vituo 382 kwenye jimbo hilo ambayo yanampa ushindi.
Alisema kusudio kubwa la kwenda mahakamani ni
kuiomba mahakama kuhesabu upya matokeo ya kura zilizopigwa ambazo nakala zake
kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) anazo mkononi kama ushahidi na kisha
mahakama kutangaza upya mshindi wa jimbo hilo bila kurudia tena uchaguzi.
Kafulila amedai kuwa, yeye ndiye alipaswa
kuibuka mshindi katika uchaguzi huo kwa kura 34,149 huku mpinzani wake (Mwlima)
akipata kura 32, 982 lakini badala yake kura zilizotangazwa kuwa amezipata ni
elfu 33 pekee ambazo hakubaliani nazo.
Hata hivyo baada ya matokeo hayo kutangazwa
Kafulila alishindwa kusaini fomu ya kukubali matokeo ya kushindwa katika
uchaguzi huo. Katika kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2015.
Walalamikiwa katika kesi hiyo ni pamoja na
Mwilima na mwanasheria wa serikali anayewakilisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Katika kesi hiyo wakili Kenedy Fungamtama
anamtetea Mwilima huku Kafulila akitetewa na mawakili watatu Prof. Abdallah
Safari, Tundu Lissu na Daniel Rumenyela.
No comments:
Post a Comment