TAMKO KWA VYOMBO
VYA HABARI
MUINGILIANO WA
MADARAKA BAINA YA MIHIMILI YA SERIKALI
Ndugu Wanahabari,
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu ni shirika lisilo la kiserikali ambalo si la
kisiasa wala kibiashara lenye kujibidiisha katika kutetea, kulinda na
kuendeleza haki za binadamu na utawala bora nchini. Kituo kwa kupitia dawati la
uangalizi wa haki na maboresho kwa mahakama limekuwa likifuatilia mwenendo wa
dhana ya uhuru wa mahakama katika mgawanyo wa madaraka wa mihimili mitatu ya
dola yaani serikali, bunge na mahakama.
Mahakama ni muhimili wa dola ulioundwa
na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977. Ibara ya 107A (1) inasema kwamba mamlaka yenye
kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa
ni mahakama. Pia katika Ibara ya 107B ya Katiba imeipa mahakama mamlaka ya kuwa
chombo huru, ibara hii inasema kwamba katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki,
mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya katiba na
yale ya sheria za nchi.
Ndugu Wanahabari
Katika
siku za hivi karibuni tumeshuhudia mhimili wa serikali ukiingilia utendaji kazi
wa mhimili mwingine wa dola yaani mahakama. Kumekuwepo na kutolewa na matamko
mbalimbali ambayo yanaashiria mhimili wa utawala/serikali ukiingilia uhuru wa
mahakama. Mnamo tarehe 4 Februari, 2016 katika maadhimisho ya siku ya sheria
‘Law Day’ katika hotuba ya mheshimiwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliitaka mahakama kuamua kesi za kodi
zipatazo 400 zilizopo mahakamani ambazo alidai zikiendeshwa ipasavyo basi serikali
inaweza kujipatia kiasi cha trilioni moja. Agizo hili linaonyesha kuwa kesi
zote hizo lazima zishinde bila kujali kuwa mahakama inaongozwa na mambo mengi
kufikia uamuzi na hasa ushahidi ulioko mbele yake.
Pia
tumesoma katika gazeti la Mtanzania la tarehe 11 Julai, 2016 Mkuu wa Wilaya ya
Mwanga akidaiwa kumwandikia barua yenye kumbukumbu namba CAB 40/229/01/25 ya
tarehe 8 Julai, 2016 Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Mwanga kutaka taarifa
mbalimbali za kesi zinazoendeshwa mahakamani kila mwezi. Barua hiyo ilitaka taarifa mbalimbali za
mahakama zikiwamo idadi ya kesi zilizopo, zilizosikilizwa na changamoto
zilizojitokeza zikiwamo za sheria, fedha na vitendea kazi kinyume na Ibara ya
107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayosema katika kutekeleza mamlaka ya
utoaji haki, mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti
ya Katiba na yale ya sheria za nchi. Agizo hili ni kinyume na Katiba na ni
kuingilia uhuru wa mahakama.
Katika
tukio jingine tarehe 12/10/2016 tumeshuhudia mkuu wa wilaya ya Kinondoni
akimwamuru mwenyekiti wa baraza la ardhi la wilaya Kinondoni kwamba shauri no
331/2014 lisikilizwe upya baada ya mlalamikaji katika shauri hilo kutoridhishwa
na maamuzi ya baraza la ardhi la wilaya. Iwapo mlaalmikaji hakuridhika na
uamuzi wa mahakama anapaswa kukata rufaa au kufuata taratibu nyingine za
kumahakama na si mtawala wa seriakali kutoa maagiza kwa mahakama.
Ndugu Wanahabari
Kituo cha sheria na haki za binadamu kinatoa
mapendekezo yafuatayo.
i.
Mhimili
wa serikali katika kutekeleza majukumu yake izingatie sheria na katiba ya nchi
na kusiwepo na kuingilia uhuru wa mahakama kama ilivyoanishwa katika Ibara ya
107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
ii.
Serikali,
Bunge na Mahakama kuheshimu na kuzingatia dhana ya mgawanyo wa madaraka na
pasiwepo mhimili mmoja kuingilia mhimili mwingine.
iii.
Ibara
ya 107A ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 imeipa mahakama
mamlaka ya mwisho ya utoaji haki hivyo kusiwepo na chombo chochote
kitakachoingilia kazi ya mahakama. Masual ya kimahakama yafuatiliwe kimahakama
na si vinginevyo
iv.
Tungetegemea
Jaji Mkuu kutoa muongozo na kuzungumazana na seriakali katika suala hili ili
kuweka msimamo katika misingi ya kisheria na kikatiba.
Imetolewa na Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu
Dkt. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji.
.
No comments:
Post a Comment