Monday, October 10, 2016

MWASAPILI: ‘TULIENI’ POINTI TATU NI ZETU

dsc_0211

MLIZI wa kutumainiwa  kwenye kikosi cha Mbeya City fc, Hassan Mwasapili amewataka mashabiki wa timu yake kutulia na kutokuwa na hofu yoyote na mchezo ligi kuu ya soka Tanzania  bara  dhidi ya Simba Sc uliopangwa  kuchezwa  jumatano hii kwenye uwanja  wa Sokoine jijini hapa.

Akizungumza na mbeyacityfc.com mapema leo, Mwasapili aliweka wazi kuwa hana presha yoyote na mchezo wa jumatano kwa sababu anaifahamu vizuri Simba hasa ukizingatia kuwa huu utakuwa ni mchezo wake wa tano kucheza dhidi ya timu hiyo tangu kupanda daraja kwa kikosi cha Mbeya City.
“Huu utakuwa  mchezo wangu wa tano kucheza dhidi ya Simba Sc,naifahamu vizuri najua nguvu yao iko kwenye eneo gani la uwanja, siwezi kusema mengi juu ya matokeo yao msimu huu ni hakika wameanza vizuri  lakini kuna jambo moja muhimu kuwa mechi zote waalizoshinda wamecheza nyumbani, jumatano hii  huu ni wakati wao mgumu zaidi kwa sababau sasa wanacheza ugenini na hii ndiyo nafasi yetu sisi kupambana nao na kuwafunga” alisema.
Akiendelea zaidi Mwasapili  alitanabaisha kuwa,matokeo ya pointi nne kwenye michezo miwili ya City iliyopita yametosha kuhifadhi nguvu za kutosha kukabiliana na kikosi cha Simba Sc hivyo hakuna shaka yeyote kuwa nafasi ya ushindi ipo kwa timu yake amabayo itakuwa ikicheza  kwa nguvu zote  kutokana na uwepo wa sapoti ya mashabiki.
“Tumekuwa na matokeo mazuri michezo miwili iliyopita, hakunaa shaka bado tuna morali ya kutosha, tuko tayari kukabiliana nao na tutawasimamisha,kitu muhimu naomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya sapoti, nasi tutacheza kwa uwezo wetu wote imani yangu kuwa hatutawaangusha  hivyo  watulie na wasiwe na hofu yoyote”, alimaliza.

No comments: