Mhe. Naibu Waziri Dkt Hamisi Kigwangalla (MB) – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Mhe. Ndugu Onesmo Buswelu, Mkuu wa Wilaya (SIHA)
Dr Said Egwaga, Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong'oto
Dr Best Magoma, Mganga Mkuu wa Mkoa.
Bwana Saimon Msuya, Katibu wa Mkoa (TUGHE)
Wadau wa Maendeleo (WHO, USAID, CDC-EGPAF, KNCV) mliopo hapa
Viongozi kutoka KCMC, Chuo Kikuu cha Nelson Mandela na CEDHA
Mwenyekiti wa CCM (Wilaya) na viongozi wote wa chama Tawala na Serikali
Viongozi wa vyama vya upinzani
Wageni waalikwa
Wanahabari
Mhe. Mgeni Rasmi,
Awali ya yote kwa niaba ya Wafanyakazi wa Taasisi ya Magonjwa ya Kuambukiza ya Kibong'oto napenda kukukaribisha wewe pamoja na wageni wote mliopo hapa katika viwanja hivi vya Taasisi. Tunashukuru sana kwa kutenga muda wako adhimu kukubali na kuhudhuria hafla hii muhimu kwa Taifa letu na safari ya kuboresha sekta ya Afya nchini.
Tunakupongeza kwa dhati kwa juhudi zako ambazo zinaonekana wazi tangu ulipokabidhiwa Wizara hiikwa kubuni njia mbali mbali ambazo zimeendelea kuboresha utoaji wa huduma za Afya nchini likiwemo suala la uhakiki ubora wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Hongera sana
UTANGULIZI:
Hospitali Maalumu ya Taifa ya kutibu Magonjwa ya Kuambukiza ya Kibong'oto (zamani Hospitali ya Taifa ya Kifua Kikuu Kibong'oto) ilianzishwa mwaka 1926 na Dr Norman Davis (Mwingereza) ikiwa ni Kituo cha kutunza wagonjwa - waliogunduliwa kuwa na Kifua Kikuu (Sanatorium) wakati dunia ilikuwa bado haina dawa za kutibu vimelea vinavyosababisha Kifua Kikuu. Mwaka 1952 hospitali ilizinduliwa rasmi kama kituo cha kutibu Kifua Kikuu nchini Tanganyika pamoja na nchi zingine za Afrika Mashariki, Somalia, Eritrea na Ethiopia.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Mwaka 2009 Hospitali ilipewa hadhi ya kuwa Kituo Bora cha utoaji wa Huduma za Kifua Kikuu Sugu nchini – yaani “Center of Excellence for Management of Drug Resistant TB in Tanzania” ikiwa na jukumu la kutibu wagonjwa wote wanaogunduliwa na kifua kikuu sugu kitaifa.
Tarehe 12 Novemba 2010, Serikali ilitangaza rasmi kupitia tangazo la Gazeti la Serikali namba.828 kuwa Kibong'oto imekuwa Hospitali Maalumu ya Taifa ya Kutibu Magonjwa ya Kuambukiza (Super specialized Infectious Diseases Hospital – Kibong'oto). Aidha hospitali ilikamilisha mpango Mkakati wa wa muda mfupi na mrefu mwaka 2013 kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID).
Mhe. Mgeni Rasmi,
Kuanzia Mwaka 2013, Hospitali ilianza kutekeleza malengo yaliyomo kwenye mpango mkakati wa Hospitali. Juhudi kubwa imeelekekezwa kutekeleza lengo linalohusu kuimarisha utawala bora katika hospitali kwa kuimarisha mifumo ya uendeshaji wa Hospitali ikiwemo kuunda upya mfumo wa utawala (organizational structure), kuanzishwa Bodi ya Udhamini, Kamati za Uendeshaji (Executive Management Committee), Kamati ya ukaguzi wa ndani (Internal Audit committee), vitengo mbalimbali kama vile kudhibiti ubora, usimamizi shirikishi, mifumo ya taarifa na kitengo cha mwanasheria wa taasisi.
Aidha, katika kipindi hicho, Hospitali kwa kushirikiana na Wizara na wadau wengine iliandaa andiko la kusaidia kupata mchakato wa Kisheria wa kuanzishwa kwa Taasisi hii. Tuna imani kuwa andiko hilo litakamilika katika siku za karibuni.
Napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru Mgeni Rasmi kwa kuwa leo hii utakamilisha na kuhitimisha moja ya nguzo muhimu katika maendeleo na ustawi wa Taasisi yetu ambayo ni utawala bora “Good governance” kwa kuzindua rasmi Bodi ya Udhamini.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Nichukue nafasi hii kukuarifu kuwa, utekelezaji wa malengo mengine yaliyomo katika mpango mkakati unaendelea katika ngazi tofauti zinazoridhisha.
Lengo namba moja linaeleza kuwa “Taasisi ya Magonjwa ya Kuambukiza itaendelea kuchangia katika juhudi za taifa za kuboresha tiba kwa magonjwa ya kuambukiza kama vile Kifua Kikuu Sugu, UKIMWI na magonjwa mengine. Kuanzia mwaka 2009 hospitali imetibu wagonjwa zaidi ya 582 wa Kifua Kikuu Sugu kati yao asilimia 40 wakiwa na maambukizi ya UKIMWI. Matibabu yao kwa sasa yanaanza ndani ya masaa 24. Matibabu yanachukua miezi 18 – 24. Tunafurahi kukutaarifu kuwa asilimia 75 ya wagonjwa hawa wanatibiwa na kupona kabisa kiwango ambacho ni juu ya kiwango cha asilimia 70 kichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Mpango wa kati ni kufupisha tiba kutoka miezi 18 – 24 na kuwa miezi 9 – 11 huku wataalam wakiendelea kusimamia tiba hiyo ili kuhakikisha matokeo mazuri yanapatikana.
Add caption |
Mhe.Mgeni Rasmi,
Lengo la pili ni kuongeza ushiriki wa jamii katika mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza kwa kuiongezea uelewa, kuzuia unyanyapaa pamoja na kuimarisha masuala yanayohusu jinsia. Baada ya kubaini ongezeko la TB katika mazingira hatarishi hasa katika mgodi wa uchimbaji madini ya Tanzanite – Mererani, Hospitali ilianzisha huduma za vikoba kwa kutumia idara ya Afya ya Jamii kuelimisha wachimbaji wadogo wadogo wa Tanzanite. Mpaka sasa wachimbaji wadogo wadogo zaidi ya 2,000 wameechunguzwa afya zao. Kati ya hao asilimia 4.5 wamekutwa na maambukizi ya TB na walipatiwa matibabu. Aidha hospitali imeshiriki katika mazungumzo kati ya wamiliki wa migodi pamoja na wizara ya Nishati na Madini ili kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kutumia maji kwenye mashimo ili kuzuia vumbi inayowaathiri wachimbaji na kuathiri mapafu (Pneumoconiosis).
Mhe. Mgeni Rasmi,
Lengo la tatu la Mpango Mkakati wa Hospitali ni kujenga uwezo wa watumishi kutoa huduma za hali ya juu za tiba kwa wagonjwa pamoja na kuwafuatilia wale wote waliopo kwenye tiba. Serikali imeongeza idadi ya watumishi kwa kuajiri na mpaka sasa watumishi waliopo ni 253; Miongoni mwao Madaktari wapo 15, mmoja ana shahada ya uzamivu katika eneo la magonjwa ya kuambukiza,5 wana shahada za uzamili katika utaalam mbalimbali, 3 wanaendelea na masomo ya uzamili katika taaluma mbalimbali (Microbiologia, Mionzi na magonjwa ya ndani). Pia tuna wauguzi 67, kumi kati yao ni maafisa wauguzi, Wafamasia wawili, Wataalam wa maabara ni 12, sita kati yao ni wataalamu wa teknologia maabara (Lab scientists), Makatibu wa Afya 2, wahasibu 3, Afisa manunuzi 2 na wengineo.
Mhe. Mgeni rasmi,
Lengo la nne ni kuanzisha kituo cha mafunzo cha kutibu magonjwa ya kuambukiza katika ngazi ya uzamili (Post graduate courses) na fellowship programu. Kwa kuanza, tumetoa mafunzo kwa watumishi zaidi ya 1,000 kutoka hospitali mbalimbali nchini juu ya tiba sahihi ya Kifua Kikuu Sugu. Lengo ni kuwawezesha kusimamia tiba ya kifua kikuu sugu kwa wagonjwa wanaotoka hospitali ya Kibong'oto.
Pia kuna mazungumzo yanaendelea baina yaChuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela ili Hospitali iwe kituo cha mafunzo kwa wanafunzi wa shahada ya uzamili katika sayansi ya magonjwa ya binadamu.
Aidha tulianzisha mafunzo ya muda mfupi ya Mawasiliano Bora kwa wagonjwa na watumishi wa Afya “Health Communication skills” kwa kuwajengea uwezo wa kuwasiliana vizuri na wagonjwa ili kuimarisha mahusiano na ufuasi wa dawa za Kifua Kikuu Sugu ambayo tiba ni ya muda mrefu
Matokeo ya hili lengo ni kuwa na wataalamu bingwa katika Nyanja ya magonjwa ya Kuambukiza
Mhe. Mgeni Rasmi,
Lengo la tano ni kuanzisha kituo cha utafiti wa magonjwa ya kuambukiza Kibong'oto. Hospitali –ikishirikiana na wadau kama NIMR, KCMC, Chuo Kikuu cha Virginia (USA) na Shirika la Afya Duniani kitengo cha utafiti magonjwa ya nchi joto (WHO – TDR kufanya tafiti mbalimbali zenye kuimarisha utambuzi wa magonjwa ya TB na magonjwa mengine ya kuambukiza. Aidha kuna machapisho ya kisayansi yamefanyika kutokana na tafiti hizi.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Lengo la sita ni kuendeleza Hospitali ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong'oto kuwa Taasisi Bora katika kutibu magonjwa ya Kuambukiza na kufanya iwe ya mfano nchini.
Katika lengo hili hospitali imeendelea kutoa ushauri kwa vituo vilivyogatua huduma hizi na kuvifanyia usimamizi shirikishi katika mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia Hospitali imeendekea kufanya vikao vya robo mwaka kwa wataalam wa Tiba ya Kifua Kikuu Sugu ili kujua ufanisi wa tiba baada ya wagonjwa kuruhusiwa, lengo likiwa ni kuendelea kufuatilia ubora wa huduma zinazotolewa kwa kuzingatia viwango na miongozo ya Taifa. Hospitali inashirikiana na vituo hivi kutatua changamoto zinazowakabili watoa huduma.
Pamoja na huduma za moja kwa moja, Hospitali imeendelea kusambaza dawa za za kifua kikuu sugu kwa wagonjwa wote ambao wanaendelea na matibabu katika vituo vya tiba nchi nzima.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Lengo la saba la mpango mkakati ni kuanzisha na kuboresha mifumo ya utawa bora katika Hospitali hii likiwa na shabaha ya kuifanya taasisi. Uwepo wa Bodi ya Wadhamini, mfumo wa utawala wa Taasisi pamoja na usimamizi wa kazi zinazotekelezwa lilishakamilika kwa kuandika nyaraka mbali mbali. Lengo hili limekamilika kwa ushirikiano mkubwa sana na wadau wa Kimaendeleo USAID. Leo hii tunajivunia kuzindua Bodi ya Hospitali.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Lengo la nane la mpango mkakati ni kuboresha miundo mbinu ya majengo ili kuwezesha shughuli za Tiba, Mafunzo pamoja na tafiti ziweze kufanikiwa. Katika lengo hili tunaishukuru Serikali kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika kuboresha majengo kuanzia mwaka 2004. Mwaka 2010, kazi ziliongezeka katika Hospitali na kusababisha wao kufanya utafiti na kujua uhitaji mkubwa uliopo wa majengo.
Majengo haya yanajumuisha upanuzi wa maabara iwe ya kisasa kwa ajili ya ugunduzi wa magonjwa ya kuambukiza na kufuatilia mwenendo wa magonjwa, Hosteli kwa wanafunzi wa fellowship, Kumbi za mikutano na sehemu za kufundishia (Resource center) pamoja na nyumba za watumishi.
Mipango yetu ni kuendelea kutafuta njia mbadala ya kuingia ubia na mashirika kama vile Shirika la Nyumba la Taifa, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na mengine ili kuweza kujenga majengo ambayo yatafanyiwa tathmini ya uwekezaji (RETURN ON INVESTMENT).
Andiko (business plan) limeshafikishwa kwa mchumi wa Wizara ili afanye tathmini ya kichumi juu ya suala la uwekezaji katika majengo.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Lengo la tisa ni Kutafuta vyanzo vya fedha ambavyo ndiyo vitakavyotumika kufanikisha malengo mengine nane.
Vyanzo vikubwa vya raslimali fedha katika Hospitali hii ni Serikali (fedha za uendeshaji, miradi ya maendeleo, fedha ya uchangiaji huduma za afya), Wadau wa maendeleo (Mfuko wa Dunia , East Africa Public Health Laboratory Network Project , Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali Norway – LHL International, CDC, USAID pamoja na WHO – TDR).
Kwa kipindi chote, hospitali imekuwa ikitegemea fedha ya uendeshaji wa Hospitali kutoka Serikali Kuu ambapo kwa miaka minne mfululizo fedha hizi zimekuwa hazitoshi kuendesha shughuli za Hospitali hata kutishia wadau wa maendeleo kutokuamini kuwa fedha wanayotoa inaweza kutumika kufanya shughuli nyingine tofauti na malengo halisi yaliyowekwa. Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya muda mfupi wa kutekeleza Mpango Mkakati wa Taasisi ambao umezingatia Mpango Mkakati wa tatu na sasa wa nne wa Wizara, Matokeo makubwa sasa na Sera nyingine za Wizara, bado tuna changamoto mbalimbali ambazo tunaamini kwa kushirikiana na Bodi ya Hospitali tutaendelea kupunguza na hatimaye kuondoka kabisa. Nazo ni:
Madeni mbali mbali ya watumishi na wazabuni waliotoa huduma kuanzia mwaka 2010 mpaka Juni 2016 yanafikia Bilioni 1.068
Upatikanaji wa sheria ya kuanzisha Taasisi
Masuala yanayohusu maslahi ya watumishi kama vile upandishwaji vyeo, malimbikizo ya mishahara pamoja na ubadilishwaji wa kada za watumishi waliojiendeleza
Kuhuishwa kwa muundo wa Taasisi
Mhe. Mgeni Rasmi napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kukubali mwaliko wetu wa kuja kuzindua Bodi ya Hospitali ya Magonjwa Ambukizi Kibong'oto.
Tumefarijika sana.
Imeandaliwa na Uongozi wa Hospitali na kusomwa kwenu na
Dkt. Riziki Michael Kisonga
KAIMU MGANGA MKUU
HOSPITALI YA MAGONJWA YA KUAMBUKIZA KIBONG'OTO
No comments:
Post a Comment