NI zaidi ya kujikuta juu ya kitanda na msichana unayempenda kuliko wote duniani. Ni zaidi ya kutazama bao la ushindi la timu yako katika dakika za majeruhi katika mechi muhimu. Yote haya hayazidi starehe ya kubwia unga.
Sahau kuhusu bia, sigara, Sahau kuhusu kila starehe. Inatajwa kuwa hakuna starehe kama unga. Na sasa Watanzania wanaendelea kumshangaa mtu anayeitwa Chid Benz. Mwanamuziki hodari wa kizazi hiki katika zile staili za vijana za muziki wa kufokafoka.
Chid anateketea. Mwili wake kwa sasa ni kama mahindi ya shambani yaliyoliwa na nzige. Mwili wake ni kama kama gari lililoungua likaisha. Amebaki mifupa tu. Unaweza kupishana naye bila ya kumfahamu kama bado kichwani unatembea na taswira ya yule Chid Benzino mwenye mashavu manene, miwani usoni, na taulo shingoni.
Wasichofahamu watu wengi ni ukweli kwamba wakati sisi tukiendelea kumshangaa Chid, kumbe yeye ndiye anatushangaa zaidi sisi. Anatushangaa kwanini hatuungani naye katika starehe yake tamu. Anatushangaa kwanini hatupo katika safari yake ya kubembea.
Kwanini anatushangaa? Ninesema hapo juu hakuna starehe tamu zaidi ya unga. Kitu cha muhimu hili ni kutoonja starehe yenyewe. Ukionja hautabaki. Hata Chid si ajabu zamani alikuwa analaani wala unga. Kosa kubwa alilifanya katika kuonja tu. Ukionja ni vigumu kutoka katika mtego.
Ni hapo ndipo lilipo tatizo la Chid na watumiaji wengine. Kikubwa wanachotakiwa kukifanya kuachana na unga hawawezi kukifanya. Kitu cha kwanza kabisa ni kuukana utamu wake. Kuukana utamu wake ni kama kuikana nafsi yako. Hapa ndipo ilipo vita kubwa ya kuacha.
Kwanza inabidi uone mapungufu makubwa ya unga lakini kama ukilegeza moyo kamwe hauwezi. Kwa mfano, leo Chid hajioni mchafu, hajioni amekonda, hajioni amepoteza nuru. Utamu wa unga umezidi akili ya kujitafakari (self assessment). Ikifika hapo kazi inakuwa nzito zaidi.
Kumpeleka Chid katika vituo vya matibabu (rehabilitation centres) ni kupoteza muda mpaka pale moyo wake utakapoanza kujifanyia self assessment kuwa amepotea, anahitaji msaada na anachukia unga. Akifika hapo atashinda vita.
Chukulia kwamba familia yako imekuomba mtoke out na uwape muda wa kuwa na wewe. Wanaweza na tabia yako ya kupenda mpira kuliko wewe. Unawakubalia walichokuomba. Lakini wanakupeleka katika hoteli ambayo watu wanatazama mpira. Lazima moyo wako utakuwa unafuatilia kwa karibu matokeo huku mwili wako ukiwa mezani na familia.
Kitu cha aina hiki kinaitwa addiction. Ndipo alipofika Chid. Kama ambavyo wewe unashangaa kwanini mtu hapendi mpira au muziki, basi na ndivyo Chid anavyotushangaa kwanini na sisi wengine hatupendi unga. Alipofikia yeye na sisi wengine wote tumefika ingawa sisi tuna starehe tofauti na yeye.
Kabla ya matibabu kitu cha msingi kwa Chid ni kukutana na mwanasaikolojia wa kumshawishi aelewe kwamba kitu anachokiona kitamu kumbe sio kitamu. Nani anaiweza kazi hii? Ni kazi ngumu. Ndio maana washkaji zake walipompeleka Bagamoyo alitoroka na kuendelea na starehe yake kwa sababu hakuwa tayari kuona utamu wake unaitwa uchungu.
Mwisho wa Chid? Sitaki kuingilia kazi ya Mwenyezi Mungu lakini mwisho wake unatabirika kiurahisi zaidi pengine kuliko mwisho wa watu wengi tunaomshangaa. Sisi tuna siku zetu za ahadi na tunaweza kuondoka mapema hapa duniani kuliko yeye, hata hivyo tutaondoka kwa vifo visivyotabirika.
Chid anaweza kufuata njia za akina Whitney Houston tu. Watu wengi wa aina yake huwa inatokea tunawaokota mtaroni au chumbani wakiwa wametangulia Mbele ya haki. Inatokea huwa wanajidunga kupitiliza, au kuliko miili yao inavyoweza kuhimili uzito wa dawa aliyotumia siku hiyo. Kwa kiingereza cha matumizi ya unga wanaita overdosing.
Hili sio la kuombea lakini maisha ya kufichana yamepita zamani jamani. Kama tunahitaji lisitokee basi ni kwa Chid mwenyewe kumjua adui yake na kupambana naye. Adui wa Chid sio unga. Adui wa Chid ni akili yake mwenyewe. Unga upo tu, lakini mbona wengi hatutumii?
Ana bahati mbaya ameangukia katika starehe ambayo inammaliza. Sisi wengine tuna matatizo kama yake ya kuendekeza starehe lakini bahati nzuri huwa hazitumalizi. Starehe ya kubishana nani zaidi ya Lionel Messi na Ronaldo haiwezi kutumaliza kwa urahisi.
MAKALA HII IMEANDIKWA NA MCHAMBUZI EDO KUMWEMBE