KADA wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoani Shinyanga ambaye kwa sasa yupo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Khamis Mgeja amesema mabadiko yaliyofanywa na CCM hayana jipya.
Akiongea na waandishi wa habari mkoani Tabora jana alisema mabadiko hayo hayana jipya kwani CCM ni ile ile,watu ni wale wale na mambo yake ni yale yale hivyo wananchi na wanachama wa CCM wasitegemee mabadiliko yoyote.
Alisema hayo baada ya kuombwa kutoa maoni na waandishi wa habari juu ya mabadiko yaliyofanywa na CCM hivi karibuni.
Mgeja alisema pamoja na madai ya CCM kuwa imefanya mabadiliko hali hiyo ni kama CCM wanajidhoofisha wenyewe.
“Kama mchambuzi wa masuala ya kisiasa hapa nchini naona CCM inajidhoofisha yenyewe bila wao kujua na ninawapa pole sana wajumbe wa NEC-CCM waliopitisha maazimio ya kupunguzwa kwa wajumbe wa kikao hicho kutoka 388 hadi 158",alieleza Mgeja
“Sisi wanachama tuliokuwemo ndani ya CCM muda mrefu tunaweza kufananisha maazimio hayo na kuku kujinyonyoa manyoya yake mwenyewe,ni mabadiliko ya ajabu ambayo hayajawahi kutokea tangu wakati wa TAA na TANU,” alisema Mgeja.
Alisema haoni sababu za msingi za mabadiliko hayo ikiwemo kufuta nafasi ya mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM na makamanda wa vijana wa CCM pia na walezi wa akina mama lakini pia panga la maumivu na kuwapunguza wajumbe wa NEC.
Alisema mabadiliko hayo hajaonyesha sababu za msingi kuwaondoa na kwamba zilikuwepo sababu za msingi za kuwepo kwao zilizopitishwa wakati wa aliyekuwa mwenyekiti wa CCM Dkt. Jakaya Kikwete.
Alisema wamefutwa bila sababu mbadala na hata jumuiya zenyewe za chama hazikushirikishwa kwani watanzania walitegemea mabadiliko makubwa hayo demokrasia ndani ya chama ingetumika kushirikisha maoni ya wanachama na jumuiya zenyewe.
Alisema hali hiyo imeonyesha ukandamizaji wa demokrasia ndani ya chama chao na kudhihirisha kuwa CCM ina wenyewe.
Aliongeza kuwa mabadiliko ni sawa na chama hicho kuwa ni cha watu wachache na saa nyingine wengine hawajulikani kimetoa maamuzi kwa niaba ya wengi.
“Watanzania walitegemea waone mabadiliko ya tunaenda wapi kisiasa na kiuchumi, msimamo halisi ni ujamaa au ubepari? Je, uchumi tunaojenga wa viwanda ni wa kijamaa au wa kibepari? lakini pia suala la Katiba mpya na ugumu wa maisha ya watanzania.
Wanafunzi wengi wa vyuo kukosa mikopo, mikataba ya madini, gesi na mafuta kufumuliwa na kuwekwa waziHaya ndiyo mambo ya msingi tulitegemea yazungumzwe na chama tawala na watoke na dira ya utekelezaji pamoja na maazimio,” alisema.
Kuhusu uteuzi wa Humphrey Polepole Katibu wa NEC- Itikadi na Uenezi Mgeja alisema hajui wamemtoa wapi na kudai ni mwanachama mchanga wa chama hicho na labda sifa aliyonayo ni ile ya kuwahi kumtukana waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa.
“Vijana tangu zamani ndani ya CCM kila aliyemtukana Lowassa alipewa cheo, nadhani Polepole naye amejipatia nafasi hiyo kutokana na juhudi kubwa za kumshambulia Lowassa katika uchaguzi wa mwaka jana,” alisema.
"Sisi wadau wa kisiasa nchini tumeishangaa CCM kumteua ndugu
Polepole tunashangazwa sijui wamemtoa wapi kwani katika siasa za Tanzania ni mchanga mno tunamuona kama nyoka asiye kuwa na sumu ndani ya CCM",aliongeza.
Aidha Mgeja alisema Polepole amejipambanua katika msimamo wa serikali tatu na bado amekubali kuwa mtumishi wa CCM, ambayo msimamo wake ni serikali mbili. Mtu huyu kukubali kuwa mtumishi wa CCM ni kusaliti watanzania kwani alikuwemo katika Tume ya Jaji Joseph Warioba na alipinga CCM kwa kuchakachua maoni ya wananchi.
Alisema Polepole hatoshi kushikilia nafasi hiyo na kwamba pengine nafasi hiyo ingemfaa Charles Mwijage, waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko.
Na Mwandishi wa Malunde1 blog Tabora
No comments:
Post a Comment