Sunday, January 1, 2017

ASKOFU MOKIWA AWAONGOZA WAUMINI WAKE KUTOA MSAADA NA KUFANYA USAFI HOSPITALI YA MWANANYAMALA JIJINI DAR ES SALAAM


 Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dk.Valentino Mokiwa (katikati), akiwaongoza waumini wa kanisa hilo Archidikonari ya Kinondoni kufanya usafi katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala Dar es Salaam leo asubuhi wakati kanisa hilo lilipotoa msaada wa vitanda na magodoro katika hospitali hiyo vyote vikiwa na thamani ya sh.milioni 12.
 Waumini wa kanisa hilo wakiendelea na kufanya usafi.
 Takataka zikipelekwa eneo maalumu.
 Takataka zikipelekwa kutupwa.
 Waumini wa kanisa hilo wakipiga picha mbalimbali za tukio hilo.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk.Valentino Mokiwa (kulia), akipanda mti nje ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala, wakati alipowaongoza waumini wa kanisa hilo  kutoa msaada wa magodoro na vitanda vya wagonjwa pamoja na kufanya usafi wa mazingira Dar es Salaam leo asubuhi. Kushoto anayemsaidia kupanda mti ni Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dk.Daniel Nkungu na wengine ni waumini wa kanisa hilo.  

 Kiongozi wa  kanisa hilo wilaya ya Kinondoni Achidikin Con Mathew Maigwa (kulia), akipanda mti.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dk. Daniel Nkungu (kulia), akipanda mti.
 Ofisa  Afya wa Hospitali hiyo, Amina Pole (kushoto), 
akipanda mti.
 Waumini wa kanisa hilo na viongozi wao wakiwa kwenye 
tukio hilo.
 Askofu Dk. Valentino Mokiwa akimkabidhi moja ya kitanda kati ya 15,  Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Daniel Nkungu.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Daniel Nkungu akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Serikali baada ya kupokea msaada huo.

Na Dotto Mwaibale

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Angilikana Tanzania, Dk Valentino Mokiwa amesema migogoro ya kisiasa inayoibuka hivi sasa inaweza kuhatarisha hali ya amani nchini.

Dk. Mokiwa ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam leo wakati akiwaongoza waumini wa  kanisa hilo Archidikonari ya Kinondoni kutoa misaada ya vifaa tiba na kufanya usafi wa mazingira katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala.

"Migogoro ya kisiasa ambayo imeanza kuzuka hivi sasa inaweza kuhatarisha amani ya nchi ni vizuri viongozi wanaovutana wakutana na kuweka mambo sawa" alisema Mokiwa.

Alisema migogoro ya kisiasa inayoendelea inaweza kusababisha kutoweka kwa amani hivyo ni jukumu la viongozi husika kuliangalia jambo hilo kwa karibu na kulitafutia ufumbuzi.

Alisema nchi yetu inahitaji amani na utulivu na kuondokana na matukio ya kuogopesha akitolea mfano miili ya watu saba iliyokutwa ndani ya viroba vilivyotupwa mto Ruvu Bagamoyo mkoani Pwani.

Alisema matukio kama hayo yanaweza kuwafanya wananchi kukimbia nchi yao kwa hofu hivyo inatakiwa kila mmoja wetu kuwa na hofu ya mungu.

Akizungumzia msaada uliotolewa na kanisa hilo katika hospitali hiyo  ambao ni  vitanda 15,magodoro 20, mashuka 40 na viatu vya tahadhri jozi 30 vyenye thamani ya Sh12 milioni alisema kanisa hilo kwa muda mrefu limekuwa likifanya maombi ya kuwaombea viongozi wa nchi na kutoa misaada ya kijamii hususan katika sekta ya afya, elimu na maeneo mengine.

Mokiwa alisema wananchi wanapokuwa katika afya bora ndipo wanapoweza kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo hivyo kuinua uchumi wao na taifa kwa ujumla.

Mkuu wa  kanisa hilo wilaya ya Kinondoni Achidikin Con Mathew Maigwa alitoa mwito kwa wadau wa maendeleo kote nchini kuwa na moyo wa kusaidia watu wenye uhitaji kama wanavyotoa michango ya harusi na sherehe nyingine.

Alisema ni jukumu la kima mmoja wetu wa kusaidia jamii na si kuiachia serikali pekee na ndio maana kanisa hilo limekuwa likifanya hivyo kama neno la mungu linavyoelekeza kuwa tupendane kwani unapokwenda kumfariji mgonjwa inasaidia kumpa hali ya unafuu.


Akizungumza kwa niaba ya serikali na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dk. Daniel Nkungu alilishukuru kanisa hilo kwa msaada huo na kusema inazidisha ari ya kazi kwa wafanyakazi na kuwafariji wagonjwa ikiwa na kuwafanya wapate nafuu na kupona  haraka.

No comments: