Tuesday, January 31, 2017

DKT. MWAKYEMBE AZINDUA RASMI OFISI ZA WIZARA YAKE MKOANI DODOMA

Katibu Mkuu Prof sifuni Mchome akitoa maelezo mafupi kwa Mhe. Waziri Dkt Mwakyembe mara baada ya kukata utepe na kuzindua rasmi ofisi za wizara mjini Dodoma

Mhe. Waziri Dkt Mwakyembe akitia saini kitabu cha wageni mara baada ya kukata utepe na kuingia ndani ya jengo la Wizara ambako alizindua rasmi ofisi za wizara mjini Dodoma

Mhe. Waziri Dkt Mwakyembe katika picha ya pamoja na watumishi na wageni wake mara baada ya kuzindua rasmi  ofisi za wizara mjini Dodoma
ambako wizara imehamia rasmi mkoani Dodoma


Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akikata utepe kuzindua rasmi Makao Makuu ya Wizara yaliyopo katika jengo la Masomo ya Biashara na Sheria katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambako Wizara imehamia rasmi makao maku ya Serikali mkoani Dodoma


DODOMA.
Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe amezindua rasmi Ofisi za wizara yake mkoani Dodoma na kuwataka Watumishi wa wizara waliohamia Makao Makuu ya Serikali, Dodoma kutekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa.

Dkt Mwakyembe amezindua rasmi makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria yaliopo mkoani Dodoma katika viunga vya Chuo Kikuu cha Dodoma baada ya wizara hiyo na watumishi wake 31 kuhamia rasmi makao makuu ya Serikali mkoani Dodoma.

Baada ya uzinduzi huo Mhe. Mwakyembe alisema kitendo cha kuhamia mkoani DODOMA ni utekelezaji wa agizo la kuhamia makao makuu ya Serikali ambalo lilitolewa mwezi Julai mwaka 2016 na hivyo watumishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao na kuwahudumia wananchi kama walivyokuwa Dar es salaam.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Jaji Mfawidhi Kanda ya Dodoma, Mkuu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kanda ya Dodoma, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Dodoma, Prof Kikula na watumishi 31 wa wizara ambao wamehamia Dodoma katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa agizo hilo la Serikali.

Awamu ya Kwanza yenye watumishi 31 wa wizara wakiongozwa na Waziri Dkt Dkt. Harrison Mwakyembe, Katibu Mkuu Prof. Sifuni Mchome na Naibu Katibu Mkuu Bw. Amon Mpanju imehamia rasmi mkoani Dodoma. Awamu ya pili na ya tatu zitafuata utaratibu ambao umewekwa na zoezi hilo linatarajiwa kukamilika mapema mwaka 2018.

Kufuatia kuhama rasmi kwa ofisi za wizara sasa mawasiliano yote yatafanywa kupitia anuani ya Katibu Mkuu Sanduku la Posta 315 Dodoma, namba ya simu ni 026 2321680, nukushi ni 026 2321679 na baru pepe ni ile ile ya km@sheria.go.tz


No comments: