Tuesday, January 3, 2017

LIGI KUU SOKA YA WANAWAKE TANZANIA BARA


Duru la Pili la Ligi Kuu soka ya Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linatarajiwa kuanza kesho Jumatano Januari 4, 2017 kwa michezo minne itakayofanyika kwenye viwanja mbalimbali.


Kwa mujibu wa ratiba, katika kundi ‘A’ pekee litakuwa na mchezo mmoja wakati kundi ‘B’ litakuwa na michezo mitatu kwa siku ya kesho Jumatano.
Mchezo pekee wa kesho wa kundi ‘A’ utakuwa kati ya Mburahati Queens ya Kinondoni, Dar es Salaam na Viva Queens ya Mtwara – mchezo utakaofanyika Uwanja wa Karume jijini katika mzunguko wa sita wa ligi hiyo.
Michezo mingine mitatu itakuwa ni ya Kundi B ambako Mejengo FC itacheza na Marsh Academy ya Mwanza kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida wakati Panama ya Iringa inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Sisterz ya Kigoma kwenye Uwanja wa Samora huku Victoria Queens ikiikaribisha Baobab ya Dodoma kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera.
Kabla ya michezo ya juma lijalo, upande wa Kundi A michezo yake miwili ya mzunguko wa sita itafanyika Alhamisi Januari 5, mwaka huu ambako Evergreen ya Temeke, Dar es Salaam itacheza na Fair Play ya Tanga kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Mlandizi ya Pwani inatarajiwa kuikaribisha JKT Queens ya Dar es Salaam, katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Mabatini.
..…………….…………………………………………………………………..............
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)   

No comments: