Tuesday, January 3, 2017

CHAWABATA CHAPINGA MANISPAA YA ILALA KUKAGUA LESENI ZA WAUZA VILEO USIKU JIJINI DAR ES SALAAM

 Mwenyekiti wa Chama cha Wahudumu wa Baa Tanzania (Chawabata), Ali Hussein (kulia), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wakati akipinga zoezi linalofanywa na Manispaa ya Ilala la kukagua leseni za wauza vileo usiku. Kushoto ni Katibu wa chama hicho, Boniface Lameck.
Katibu wa chama hicho, Boniface Lameck akitoa ufafanuzi 
katika mkutano huo.


Na Dotto Mwaibale

CHAMA cha Wahudumu wa Baa Tanzania (Chawabata) kimepinga zoezi linalofanywa na Manispaa ya Ilala la kukagua leseni za wauza vileo usiku.

Akizungumza Dar es Salaam  jana Mwenyekiti wa chama hicho,  Ali Hussein alisema zoezi hilo linawatisha wateja wanapokuwa wakipata vinywaji katika baa mbalimbali.

Hussein alisema chama hicho kimepokea malalamiko kutoka kwa wamiliki wa baa ambao ni wanachama wao.

Alisema wiki moja kabla ya kuanza kwa sikukuu za mwishoni mwaka maofisa biashara wa Manispaa ya Ilala walikuwa wakipita katika baa mbalimbali maeneo ya Ukonga na vitongoji vyake kuanzia saa mbili usiku kukagua leseni.

Alisema maofisa hao walikuwa wameongoza na askari polisi waliokuwa na bunduki jambo ambalo kiusalama sio zuri.

"Huu utaratibu wa kukagua leseni usiku na mtutu wa bunduki unaweza kutoa fursa kwa wahalifu nao kwenda kwenye mabaa na kujifanya ni maofisa biashara na kufanya uporaji tunaomba serikali kuliangalia jambo hili" alisema Hussein.

Alisema hali hiyo imejitokeza baada ya serikali kuzuia baa kufunguliwa asubuhi kama ilivyokuwa awali ambapo chama hicho oktoba mwaka jana kiliiomba serikali kupitia mtandao huu na katika vyombo vya habari  kuruhusu kufunguliwa kwa baa wakati wote ili kutoa nafasi ya wauza vileo kufanya biashara na kuweza kukusanya fedha za kulipa kodi ya serikali.

Alisema kwa nyakati za mchana ni vigumu kukuta baa zikiwa wazi na ndio maana maofisa hao wameamua kwenda usiku kukagua leseni hizo jambo ambalo ni hatari kwa wateja na maofisa hao

"Muda wa kufungua baa kuanzia saa 10 jioni unawaathiri wateja wetu kwani kwa masaa matano ya kufanyabiashara ya vileo na vinywaji vingine ni mchache mno" alisema Hussein.

Alisema hatua hiyo ya serikali ya kuamuru baa kufunguliwa kuanzia saa 10 imeathiri wahudumu wa baa ambao wengi wao wamepunguzwa kazi ambapo wanaiomba serikali kuangalia jambo hilo.

Meneja wa Baa ya Serengeti iliyopo eneo la mabaa Banana katika manispaa hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Emanuel alisema kitendo cha maofisa hao kukagua leseni za biashara usiku ni kigeni kwao na kinawatisha wateja wao ambapo ameomba manispaa kuangalia upya muda wa kufanya ukaguzi huo.

 Ofisa Habari wa Manispaa ya Ilala, Neema Njau alisema zoezi hilo lipo kisheria na linafanywa na kamati maalumu iliundwa na manispaa hiyo ambayo ipo chini ya wakuu wa polisi wa wilaya hiyo.

"Ukaguzi wa leseni hizo hauwezi kufanyika mchana kwa kuwa baa nyingi zinakuwa zimefungwa lakini wasiliana na ofisa biashara wa manispaa atakupa maelezo mazuri zaidi" alisema Njau. 


No comments: