Sunday, January 1, 2017

HOTUBA YA ZIITO KABWE MTONI KIJICHI UZINDUZI WA KAMPENI

HERI YA MWAKA MPYA 2017

Namwomba Mungu, muweza wa yote atupe baraka tele kwenye mwaka huu mpya na kutupunguzia mitihani ya mwaka uliomalizika jana. Tuendeleze Dua na Maombi nchi yetu iendelee kuwa na amani na ustawi katika mwaka huu unaoanza leo.


Tumekuja hapa Katani Kijichi kwa sababu maalumu, nayo ni kuwaomba mtuchague kuwawakilisha kwenye Baraza la Madiwani la Manispaa ya Temeke. Chama chetu hakina uwakilishi katika Baraza hilo kwani katika Madiwani 23, CCM wana madiwani 14, UKAWA madiwani 9. Hawa nimadiwani wa kuchaguliwa. Katika madiwani waUKAWA, CHADEMA ina madiwani 6 na Chama cha CUF madiwani 3. Kwa unyenyekevu kabisa tunaomba nasi Chama chetu cha ACT Wazalendo kipate uwakilishi ndani ya Manispaa ya Temeke baada ya Uchaguzi mtakaoufanya tarehe 22 Januari 2017. 

Uchaguzi huu hautabadilisha uongozi wa Manispaa ya Temeke kwani tayari Meya anatoka CCM kutokana na wingi wa madiwani wa Chama hicho. Hata hivyo jinsi mtakavyopiga kura na kuamua diwani atoke chama gani kutabadilisha kwa kiwango kikubwa sana uendeshaji wa Manispaa yenu kwani mtakuwa na Diwani mahiri kutoka chama makini kisera na hivyo kuweza kubadili namna ya kushughulika na shida zenu wananchi wa Kijichi. Mtapata Diwani Huru ambaye hatafungwa na itikadi za kivyama katika kuwawakilisha. Atashirikiana na Wabunge wote 2 wa Manispaa yenu na Meya wa Manispaa yenu ili kuleta maendeleo katika kata yenu. Mkichagua Diwani kutoka vyama ambavyo tayari vina uwakilishi ndani ya Manispaa mtakuwa mnaendeleza siasa za vyama hivi kushindana bila kujali maendeleo yenu. Mwaka mmoja unatosha sana kupima na kuamua kama mnataka uwakilishi wa dhati ama tambo za kisiasa.

Chama cha ACT Wazalendo na Mgombea wetu wa Udiwani katika Kata yenu ya kijichi tunajua changamoto zenu. Mgombea wetu ni mkazi wa kata hii katika mtaa wa Mgeni Nani. Ni mwenzenu na amejiandaa vya kutosha kutoa uwakilishi uliotukuka. Manispaa yenu inahitaji sauti mpya iliiweze kutatua changamoto za wananchi katika sekta ya Afya, Elimu na Uchumi wenu kwa ujumla.

Afya
Utafiti tuliofanya unaonyesha kuwa kuna changamoto kubwa sana ya Afya katika Kata yenu. Hakuna Kituo cha Afya wala Zahanati katika kata yenu na hivyo kuwafanya mtembee umbali mrefu sana kupata huduma husika na kwa gharama kubwa za usafiri. Kwa ujumla hili ni tatizo la Manispaa nzima ya Temeke. Manispaa yenu ina Vituo vya Afya 2 tu na Hospitali moja ya Temeke. Wakati Sera ya Serikali ni kuwa na kituo cha Afya kila kata, Kata zote 23 za Temeke zina vituo vya Afya 2 tu. Hii ni changamoto kubwa hasa ukizingatia idadi kubwa ya watu wa Manispaa yenu wanaofikia takribani laki 8.
Iwapo Mtamchagua Diwani, ndg. Edgar F. Mkosamali kutoka ACT Wazalendo tunawahakikishia kuwa tunashirikiana nanyi kutatua tatizo la huduma za Afya katika Kata hii kwa kuhamasisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kijichi. Mimi kama kiongozi wa chama, ninawaahidi kushirikiana na Diwani wenu ili kumaliza changamoto hii mara baada ya kuwa tumechaguliwa kushika nafasi hii.

Elimu 
Tumeambiwa kuwa kuna changamoto kubwa ya elimu katika Manispaa ya Temeke. Wakati Fulani nilikuwa naongea na Mbunge wa Jimbo la Temeke akawa anaeleza namna Shule za Sekondari zilivyo mbali kwa sababu Shule za Kata zilijengwa mbali huko Pemba Mnazi na Somangila kipindi Kigamboni bado ni sehemu ya Manispaa ya Temeke. Hii inapelekea watoto wenu kutembea mwendo mrefu kwenda shuleni na hivyo kuwa ni kikwazo kikubwa kwa mahudhurio na kadhalika. Watu wa Kijichi hamna budi kumtuma Diwani mwenye uwezo wa kujenga hoja ili kupata suluhisho la pamoja la changamoto hii kwa wakazi wa Manispaa nzima ya Temeke. Ndg. Mkosamali, naona ndio mgombea pekee katika wagombea wote wanaogombea hivi sasa kuweza kuja na majawabu ya Elimu katika Manispaa ya Temeke. Ninawasihi watu wa kijichi mumpe kura nyingi sana Mkosamali ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto hii nzito inayowakabili watu wa Manispaa ya Temeke kwa ujumla wake.

Hali ya Uchumi
Tumeambiwa katika utafiti tuliofanya kuwa hali ya wananchi kiuchumi ni mbaya siku hadi siku. Vijana hawana ajira na hata mikopo inayopaswa kutolewa kwa vijana hugawiwa kwa kufuata misingi ya itikadi za vyama. Manispaa ya Temeke ina Bajeti ya zaidi ya shilingi bilioni 40 kwa makusanyo ya ndani. Hivyo mikopo ya Wanawake na Vijana inapaswa kuwa takribani shilingi 4 bilioni kila mwaka. Hizi ni fedha nyingi na zikitumika vizuri zinaweza kumaliza changamoto ya ajira kwa wanawake na vijana.
Sisi ACT Wazalendo, tukishinda kata hii tutatumia mfumo ambao unatumika katika Manispaa ya Kigoma Ujiji inayoongozwa na chama chetu katika kukabili tatizo la mikopo kwa wanawake na vijana. Kule Kigoma tumeanzisha skimu ya Hifadhi ya Jamii ya Manispaa ambapo tunatumia fedha hizi kulipia michango 50% kwa kila mwananchi anayechangia kwenye hifadhi ya jamii na hivyo kuwawezesha kupata mikopo ya gharama nafuu na vile vile bima ya afya kwa Vijana na Wanawake kupitia vikundi vyao za uzalishaji mali. Tunaomba mumchague Diwani kutoka ACT Wazalendo ili kuwezesha Vijana na Kinamama kupata bima ya afya, mikopo na kujiwekea akiba ya pensheni kupitia fedha za mifuko ya wanawake na vijana. 

Hali ya Nchi yetu kwa ujumla
Ndugu Wananchi, tumemaliza mwaka 2016 chini ya utawala wa awamu ya Tano. Kwa Kiwango kikubwa tunaweza kusema ulikuwa ni mwaka wa kupambana na ufisadi. Sisi kama Chama tunapongeza sana juhudi kubwa za kuondoa hali ya ‘kutoshikika’ (impunity) iliyokuwa imezagaa nchini kiasi cha kufanya ufisadi kuwa sehemu ya maisha yetu. Hivi sasa ni dhahiri kwamba ufisadi umekuwa ni gharama na hivyo ufisadi mkubwa kupungua sana. Itakuwa ni wendawazimu kutotambua juhudi hizi za makusudi zinafanywa na Rais John Pombe Magufuli dhidi ya donda ndugu hili la ufisadi.
Chama chetu siku zote tumekuwa mstari wa mbele kabisa kuunga mkono juhudi hizi na hata kushauri namna bora zaidi ya kumaliza ufisadi ikiwemo kurejesha Miiko ya Uongozi kwa kuhakikisha Viongozi wa Umma wanaweka wazi Mali, Madeni na Maslahi yao ili kuondoa mgongano wa kimaslahi katika utendaji wao wa kazi. Tunasisitiza Rais aone jema hili kwani atakuwa anarejesha Tanzania ya Mwalimu Nyerere ambapo Miiko ya Uongozi ilikuwa ni nguzo ya Siasa ya Azimio la Arusha la Chama cha TANU. Sisi ACT Wazalendo tulihuisha Azimio la Arusha kwa kutangaza Azimio la Tabora. Mwaka huu mwezi Februari tutaadhimisha miaka 50 ya Azimio la Arusha kwa kufanya Mkutano Mkuu wa kidemokrasia huko Jijini Arusha.

Wananchi, tunatarajia kwamba vita dhidi ya ufisadi sasa itaenda sambamba na kuboresha hali ya maisha ya wananchi. Ni lazima sasa Serikali ijipange upya katika kuchochea uwekezaji na kuhamasisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa kawaida. Juzi tumesikia Waziri wa Fedha anasema, katika kipindi cha miezi 3, kati ya Julai na Septemba, biashara 2000 zilizokuwa zinaajiri maelfu ya Watanzania zimefungwa. Vile vile taariza zinaonyesha kuwa Biashara ya usafirishaji imeporomoka ambapo zaidi ya watu 30,000 wamekosa kazi za moja kwa moja katika uendeshaji wa malori kwenda nchi jirani.
Baadhi ya Viongozi wa Serikali wanasema hawa wanaolalamika wote walikuwa wapiga dili. Hapana. Serikali haiwezi kuhukumu wananchi wake wote kuwa ni wapiga dili. Kuna ambao wamekosa kazi kutokana na sera mbaya ama utekelezaji mbaya wa Sera za Serikali. Huwezi kusema mama lishe aliyekuwa anauza chakula kwa madereva na matingo wa malori na sasa hana biashara, na anashindwa kulipa mkopo SACCOS/VICOBA kwamba ni mpiga dili. Nini maana ya Serikali hii kujiita ya wanyonge kama wanaoumia na sera zake ni hao hao wanyonge?
Tunashauri Serikali kujitazama upya na kuanza kustawisha uchumi kwanza kupitia matumizi yake ikiwemo kulipa wazabuni wa ndani ambao wakitumia ndani wanachochea shughuli za uchumi. Serikali ni mtumiaji mkubwa hivyo isipotumia vya ndani wananchi hawatumii pia. Ili wananchi wale ni lazima Serikali ile. Hatuzodoi kununua ndege, kwamfano, lakini Serikali ikila ndege Canada, wanaofaidika ni wananchi wa Canada ambao watalipwa mishahara kutokana na fedha kutoka Tanzania zilizonunua Bombadier. Matumizi ya Serikali yawianishe nia ya maendeleo ya haraka ya vitu na maendeleo ya watu. Mwaka 2017 uwe wa kujenga uchumi wa ndani kwa kuifanya Serikali itumie na kulipa wakandarasi wa ndani ili kupata kinachoitwa ‘multiplier effect’. 
Njia nyepesi sana ya kupima kama jamii inaendelea ni kuangalia mambo makuu 3; Umasikini umepungua? Kukosa Ajira kumepungua? Pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho limepungua? Ukisoma Taarifa zote za Serikali na Benki Kuu utaona kuwa jibu ni moja kwa maswali yote hayo matatu. Licha ya kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi nchini mwaka 2016, Umasikini umeongezeka, ukosefu wa Ajira umeongezeka na Pengo la wenye nacho na wasio nacho limeongezeka. Kwanini?

Kwa sababu juhudi za Rais kupambana na ufisadi hazikuendana na juhudi za wasaidizi wake kumsaidia kupambana na Umasikini, ukosefu wa Ajira na kupunguza pengo la kipato kati ya wenye nacho na wasio nacho. Badala ya Mawaziri kuwa wanakimbizana na Rais kutumbua wangekuwa wanamsaidia Rais kuondoa vikwazo vya ukuaji wa uchumi ili kutengeneza ajira nyingi na bora. Ni dhahiri huwezi kutengeneza ajira kwa kutukana sekta binafsi kila siku bali kwa kufanya kazi pamoja na sekta binafsi.

Wananchi, jambo la pili ni demokrasia. Sisi tunaamini kwamba ilikuwa ni makosa makubwa ya mwaka 2016 kuzuia mikutano ya vyama vya siasa. Wanaomshauri Rais wanadhani kuwa ili Rais atawale vizuri anahitaji upinzani dhaifu, la hasha. Mwaka mzima wa 2016 umeonyesha kuwa bila upinzani madhubuti CCM imeyumba. Mwaka mzima uligubikwa na mijadala kuhusu masuala ambayo hayawahusu wananchi moja kwa moja kama wanasiasa kuitana majina ya udikteta uchwara, dikteta mamboleo nk. Hata sisi ACT Wazalendo tulipojaribu kuingiza hoja nzito kama vile hali mbaya ya maisha ya wananchi hazikufua dafu mbele ya vibwagizo vya kisiasa. Mwaka mzima CCM haikufanya kazi ya siasa, imeyumba.Sababu ni kudhibiti upinzani.
Serikali yeyote mahiri inahitaji upinzani mahiri, na ndio maana sisi tulianzisha chama hiki ili kujenga upinzani mahiri. Rais aondoe zuio lake la vyama kufanya mikutano ya hadhara ili kutoa changamoto kwa Serikali kuwezesha nchi kusonga mbele. Mikutano ya hadhara ni haki ya kikatiba na kisheria ya vyama, hivyo ni hatari sana haki hii kuzuiwa kwa kauli za viongozi na kutekelezwa kinyume na katiba ya nchi na sheria zake.

Mwaka 2017 uwe ni mwaka wa kuachia demokrasia ifanye kazi yake ikiwemo kuacha watu wanaokosoa Serikali kuendelea kukosoa Serikali kwani katika kukosoa ndio Serikali huona makosa yake na kujifunza. Kwa mfano, Serikali kubana mitandao ya kijamii kama JamiiForums ni kuzuia fursa kubwa ya kupambana na ufisadi kwani kupitia mitandao hii watu huweza kupiga firimbi kuonyesha mahala ambapo kuna ubadhirifu. Kuna mifano mingi sana ya maskandali yaliyoibuliwa kupitia mitandao ya kijamii. Haki ya Kujieleza isichezewe mwaka 2017.

Wananchi wa Kijichi, nisiwachoshe kwa maelezo mengi katika siku hii ya kwanza ya mwaka 2017. Niwatakie kila kheri katika mwaka mpya na natangaza rasmi kuwa kampeni za udiwani kata ya Kijichi kwa Chama cha ACT Wazalendo zimefunguliwa rasmi. Tunaomba kura zenu nyingi kwa ndg Edgar Mkosamali ili awe diwani wa kata ya Kijichi ashirikiane nanyi kuleta maendeleo.

Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo
Kijichi –Temeke Dar es Salaam
Januari 1, 2017
da

No comments: