Friday, January 27, 2017

TAMKO KUTOKA LHRC KUKEMEA MAUAJI YA RAIA NA UKIUKWAJI WA MISINGI YA HAKI ZA BINADAMU

 
Ndugu Wanahabari,
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni shirika lisilo la kiserikali ambalo si la kisiasa wala kibiashara lenye kujibidiisha katika kutetea, kulinda na kuendeleza haki za binadamu na utawala bora nchini. Kimekuwa kikifuatilia na kukusanya taarifa mbalimbali za matukio ya ukiukwaji wa haki za Binadamu na mwenendo wa serikali na taasisi zake ili kuhakikisha ulinzi wa haki hizo na  utendaji wa serikali unafuata misingi ya sheria na haki za Binadamu.


Ndugu wana Habari
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tumekuwa tukifuatilia kwa ukaribu taarifa nyingi za matukio ya kujichukulia sheria mkononi yanayo endelea nchini kote na kukemea bila kuchoka vitendo hivyo vya uvunjifu wa haki. Hivi karibuni tumefuatilia kwa umakini shambulio lililofanywa na  walinzi wa Shamba la Meru USA  Plant ambao wanatajwa kuwa waajiriwa wa  kampuni ya ulinzi ya Suma JKT katika kijiji cha Kandaskirieti Kata ya Oldonyosambu na  kusababisha  kifo kwa watu wanne na wengine watano kujeruhiwa siku ya Tarehe 24/1/2017.

Katika taarifa maalumu ya Jeshi la Polisi iliyotolewa Siku ya Tarehe 25/1/2017  imefafanua  kuwa katika siku ya  tukio walinzi hao walikamata mifugo  iliyoingizwa kwenye shamba la  serikali kinyume na taratibu ikijumuisha ng'ombe 46 na mbuzi 65 na kuhifadhi ndani ya boma lilopo ndani ya shamba hilo. 
Taarifa hiyo inasema zaidi kuwa, ghafla lilitokea kundi la wafugaji  wakiwa na silaha  mbalimbali za jadi na kuanza kuwashambulia  ndipo walipo jaribu kuwatawanya na jitihada zao zilipo shindikana walirusha risasi za moto zilizo sababisha kifo kwa watu wa nne na kujeruhi wengine watano.

Ndugu Wana Habari
Kituo Cha Sheria kimepitia vizuri taarifa ya Jeshi la Polisi na taarifa zingine za ziada kutoka kwa waangalizi  wa Haki za Binadamu  na wananchi walio shuhudia tukio hilo wakiwemo majeruhi walionusurika na hivyo kuliomba jeshi la Polisi kutoa ufafanuzi wa  maswali  yafuatayo ambayo yanaweza kuondoa wasiwasi  katika kuitafakari taarifa walioitoa: 

1.      Walizi  waliokuwa Lindo wanasema walivamiwa na kushambuliwa na wananchi walio kuwa na mapanga na fimbo na silaha nyingine za jadi, kwa hiyo walikua katika hatari ya kuuawa au kujeruhiwa, hivyo iliwalazimu kujihami. Je inakuwaje katika shambulio hilo   ambalo askari wanadai kuzidiwa nguvu asiwepo Askari hata mmoja aliyejeruhiwa na taarifa yake kutolewa?.

2.      Je Walinzi hao kama walikuwa wachache isingewezekana kujiokoa kwa kukimbia na kisha kuita usaidizi wa jeshi la polisi ambalo lina utaalamu wakushughulikia wananchi katika mazingira hayo, jambo ambalo lingeepusha vifo na majeruhi?

3.      Je nguvu iliyo tumika kusambaratisha wananchi na kusababisha vifo na majeruhi inalingana na nguvu ya wananchi wanao lalamikiwa? 

4.      Katika tukio hilo mtoto wa miaka 13 amejeruhiwa vibaya je na yeye alikuwa ni sehemu ya kundi lililokua linafanya shambulio hilo?

5.      Kwa nini taarifa ya awali jeshi la Polisi iko katika mfumo ambao ni utetezi badala ya kuwa taarifa inayo elezea tukio na kuacha sehemu iliyo baki kufuata utaratibu wa kisheria  ikiwemo watuhumiwa  kufikishwa mahakamani kujibu hoja wao wenyewe? 

6.      Tunafahamu kabisa Walinzi nao wana haki ya kujihami na hawapaswi kuuawa na wananchi wanaotaharuki lakini kwa weledi wao kujihami si lazima iwe kwa kutumia nguvu kiasi hiki cha kupotea maisha ya watu .

Ndugu Wana Habari
Kituo Cha sheria na Haki za Binadamu kama watetezi wa haki hizo, kimetafakari  mazingira yaliyo sababisha vifo vya watanzania wenzetu wanne na   kujeruhiwa wengine watano na tumebaini  mambo yafuatayo: 

1.      Kumekuwa na matumizi mabaya ya nguvu zisiso kuwa za lazima katika kusuluhisha migogoro mbalimbali baina ya wananchi wenyewe au wananchi na serikali na kuhatarisha haki ya kuishi ambayo serikali imeapa kuilinda kwa mujibu wa katiba. 
2.      Migogoro baina ya wakulima na wafugaji inazidi kukua na jitihada za serikali  kupata suluhisho la kudumu  hazilingani na hali halisi. 
3.      Matukio ya majeshi kujeruhi au kuua wananchi hayapewi uzito unao stahili zaidi yamekuwa yakitangazwa hadharani kama mafanikio ya majeshi hayo katika kutekeleza  majukumu yao.
4.      Kauli mbalimbali za viongozi wa nchi katika ngazi zote. Ikiwemo kauli ya Rais mwenyewe ya Tarehe 25/1/2016 wakati wa uzinduzi wa mradi wa mabasi ya Mwendo Kasi  kwamba,“ sa nyingine ukitumia sheria tu watu hawajifunzi lazima utumie nguvu za ziada” ni moja ya kauli ambazo zinahamasisha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi pamoja na kuvunja haki za binadamu kinyume na katiba ambayo viongozi hao wameapa kuilinda.
5.      Vyombo vyenye mamlaka vimeshindwa kusimamia vyema migogoro ya ardhi inayoendelea ikiwemo Wizara ya Ardhi ambayo mpaka sasa haitoi taarifa yoyote kuhusu mpango wa taifa wa kutenga maeneo ya ufugaji, jambo ambalo linachelewesha kupatikana mwarobaini wa migogoro iliyopo.
Ndugu Wana Habari
Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa wito kwa Serikali na  mamlaka husika kuchukua hatua madhubuti na za kisheria kuboresha ulinzi wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho ya lazima katika maeneo yaliyo fafanuliwa ndani ya tamko hili ili kujenga jamii yenye Haki na usawa.
Kwa wahusika wote walisababisha vifo na kuwajeruhi watanzania wenzetu hatua za kisheria zichukue mkondo wake ili haki iweze kutendeka.

Dr Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)



No comments: